Cute Wife
JF-Expert Member
- Nov 17, 2023
- 1,906
- 5,000
TAARIFA KWA UMMA
KUKEMEA UDHIBITI WA UHURU WA HABARI NA UNYANYASAJI WA WAANDISHI WA HABARI
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimepokea kwa masikitiko taarifa za kukamatwa kwa mwandishi wa habari, Bi. Dinna Maningo, aliyekamatwa nyumbani kwake Tarime, mkoani Mara, Juni 13, 2024 saa mbili usiku. Bi. Dinna amekuwa akishikiliwa katika kituo cha polisi Tarime bila tuhuma zilizosababisha kukamatwa kwake kuwekwa wazi. Leo, Bi. Dinna amesafirishwa kuelekea Mwanza, na mpaka sasa hakuna taarifa zozote kuhusu tuhuma zake zilizowekwa wazi. Kushikiliwa kwa mwandishi huyu kunaenda kinyume na Katiba na sheria za nchi hii pamoja na misingi ya demokrasia na uhuru wa habari. Kushikiliwa kwake pasipo taarifa za tuhuma zinazosababisha kushikiliwa kwake kunavunja haki zake za kikatiba kama zilivyoainishwa katika ibara ya 15-17 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika jamii ya kidemokrasia, uhuru wa vyombo vya habari ni nguzo ya uhuru wetu, inayohakikisha uwazi na uwajibikaji ndani ya taasisi zetu. Kuwekwa kizuizini kwa mwandishi wa habari bila mashtaka rasmi kunavunja misingi hii muhimu na kuibua maswali makubwa kuhusu dhamira ya kufuata sheria na haki. Tunatoa wito kwa mamlaka zilizomshikilia kumwachilia huru Bi. Dinna Maningo mara moja au kumshtaki kwa kosa maalum, kama sheria inavyotaka. Kumshikilia mwandishi wa habari bila tuhuma wazi sio tu kunakiuka haki zake bali pia kunatuma ujumbe wa kutisha kwa wanahabari wengine wanaojitahidi kuwafahamisha umma.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinasimama pamoja na Bi. Dinna Maningo na waandishi wa habari wote wanaokabiliwa na unyanyasaji na vitisho visivyo vya haki katika harakati zao za kutafuta ukweli. Tunatoa wito kwa mamlaka husika kufuata misingi ya haki na uwazi, ambayo ni muhimu katika kudumisha imani ya umma kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria na kulinda maadili yetu ya kidemokrasia.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kitaendelea kufuatilia hali hii kwa karibu hadi suluhisho la haki na la kweli litakapopatikana.
Imetolewa leo tarehe 14/06/2024;
Dkt. Anna Henga
Mkurugenzi Mtendaj
====
Pia soma: MCL: Mkuu wa Mkoa adaiwa kumlawiti mwanafunzi wa SAUT