Chama cha ACT Wazalendo mkoani Lindi, wametoa malalamiko yao mbalimbali kwa Afisa mwandikishaji wa uchaguzi katika Jimbo la Mjinga pamoja na Jimbo la Lindi mjini Bwana Juma Mnwele kutokana na kutoshirikishwa katika masuala ya uandikishaji wa wapiga kura kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kutowapatia vitabu vya maelekezo kwa vyama vya siasa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Malalamiko hayo yametolewa na Katibu wa Jimbo wa ACT- Wazalendo Lindi mjini, Bw. Ahmadi Zuberi wakati akizungumza na ITV ofisini kwake huku Afisa mwandikishaji wa uchaguzi katika jimbo la Mchinga na jimbo la Lindi mjini Bw. Juma Mnwele, akitolea majibu malalamiko hayo juu yake.
Wakati Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi kupitia kwa Katibu wake wa Jimbo la Lindi Mjini Bw. Ahmad Zuberi wakitoa malalamiko juu ya kutoshirikishwa katika masuala ya uandikishaji wa wapiga kura kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ikiwemo kutowapatia vitabu vya maelekezo kwa vyama vya siasa kuhusu zoezi hilo, Katibu wa Wilaya ya Lindi wa Chama cha Wananchi CUF Shazily Mosha amesema kwa upande wao wameshiriki na kushirikishwa ipasavyo katika hatua zote.
Amesema kwamba mawakala wao wamekula kiapo cha kutunza siri kilichotanguliwa na ufafanuzi wa majukumu yao kama vyama vya siasa kwenye zoezi zima la kuboresha dafatari la kudumu la mpiga kura ikiwa pamoja na kukabidhiwa vijitabu vya maelezo.
Zoezi la uandikishaji na uboreshaji wa daftari la Kudumu la Mpiga kura limeanza Mkoani Lindi Januari 28 na hadi Februari 3,2025.