Loliondo kazi inayohitaji mseto kimbinu

Loliondo kazi inayohitaji mseto kimbinu

James Hadley Chase

JF-Expert Member
Joined
Mar 25, 2020
Posts
1,984
Reaction score
3,695
VURUGU zinazotokana na maamuzi ya kuhama na kupisha utunzaji endelevu wa hifadhi ya Ngorongoro katika wilaya ya Loliondo mkoani Arusha ni mtihani mwingine wa kiutawala ambao sasa unausumbua uongozi wa taifa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amefika huko mara kadhaa kusimamia mazungumzo na serikali ili wananchi waelewe kinachotokea, na kinachohitaji kufanyika, na kwa kiasi fulani amefaulu kufikisha ujumbe.

Hata hivyo , upinzani uliojikita katika jadi na dhana ya wanamazingira kuwa wakazi wa jadi hawaharibu mazingira, una ushawishi mkubwa.

Ikafikia mahali bunge linaahirisha majadiliano yake ya kawaida na kuangalia hali ilivyo Loliondo, kukawa na vurugu hadi kuuawa polisi , hivyo ikamlazimu Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, kwenda kukagua eneo hilo kwani limekuwa uwanja wa mapambano.

Ni kama vile kunahitajiwa kanda maalum ya polisi, endapo ulinzi na usalama kwa hali ya kawaida unaanza kuwa wa mashaka.

Mwelekeo serikalini unakuwa ni kuufuatilia 'mkono uliojificha' katika vurugu hizo, kwani huenda yapo makundi ya wadau wa nje na ndani ya nchi wasioridhika na sera hiyo.

Hadi hivi karibuni bado baadhi ya wadau hao wamekuwa wakitoa matamshi ya nguvu kuhusu suala hilo, wakati mmoja zikaja taarifa kuwa wapo wazee waliozungumza katika mkutano wa hadhara kuwa wananchi hawataondoka, tena wako tayari kupigania kuondolewa sera hiyo, yaani kuwaondoa katika ardhi yao ya jadi.

Ni moja ya maeneo ambayo yanahitaji elimu kwa kiasi fulani, ila siyo ili mtu aelewe aache mwelekeo alio nao, ila kama utangulizi wa kuelewa msingi wa hatua ya pili ambayo inalenga maslahi, kuwa iwe inakubalika na kuvumilika, na hata kuleta matamanio kwao.

Akiwa Loliondo hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, anasema kuna makundi ya watu ambayo yanatumika kuchochea na kuwasha moto wa kutoelewana kati ya serikali na wananchi, jambo analosema halikubaliki.

Hayo yanatokea baada ya Spika Dk Tulia Ackson, kuitaka serikali kueleza kilichomo katika video mitandaoni ya wakazi wa Loliondo wakiwa wameshika sime kutishia amani, wakipinga kuondolewa huko.

Anachosisitiza Waziri Mkuu ni kuwa hakuna mtu atakayelazimishwa kuhama, maelezo ambayo ni sehemu ya elimu au taarifa ya kina inayotangulizwa na serikali, zaidi kuhusu uhifadhi.

Kilichosababisha vurugu ilikuwa ni mwendelezo wa zoezi la kupiga ramani eneo hilo kwa kuweka mawe ya kisanifu kuonyesha ni wapi na kituo gani katika mpaka wa eneo husika linalopimwa.

Ni wakati ambao zoezi la kuwahamisha wakazi wa vijiji 14 vinavyozunguka eneo maalum la mapito ya wanyama na kinachoonekana ni kuwa wakazi hao wamebaki na umoja wao licha ya baadhi yao kukubali kuhamia Handeni, ambako serikali inatayarisha makazi bora, huduma jamii, eka tatu za ardhi ya kaya na eneo pana la malisho ya pamoja ya ng'ombe.

Kwa kuwa mwelekeo huo ni wa kuwahamisha kama kundi, wale wasiotaka kuhama kwa udi na uvumba wanazungumza kwa kujiamini, kwa sababu suala hilo bado ni la kundi, si la maamuzi ya mtu mmoja mmoja.

Kwa maana hiyo, zinahitajiwa mbinu tofauti za kuchanganya 'karoti'na 'fimbo' kama inavyoitwa katika fasihi, kwani 'fimbo' pekee zitaleta ugomvi mkubwa kati ya wananchi na serikali, ila 'karoti' zinazotolewa kwa jamii hiyo kwa pamoja zinaulinda umoja wao wa kijamii, kuwezesha uchochezi kujikita miongoni mwao.

'Fimbo' inayoweza kutumika bila madhara ni kukumbushana kuwa ardhi yote ni mali ya pamoja ya wananchi wa Tanzania, na serikali ndiyo yenye dhamana ya matumizi yake; kuwa hii ndiyo maana ya kuwa nchi, kuwa makabila hayana 'haki isiyohamishika' ya umiliki ardhi.

Hilo likishaeleweka, serikali itoe amri nyingine ya 'karoti,' kununua ng'ombe wote walioko pale kwa bei mara tatu ya soko, watwae, ndipo wahame.

Umuhimu wa mpango huo ni kuiyeyusha jadi ambayo inakinzana na mpango wa kuhamia katika nyumba zilizojengwa kimjini.

Hata kama kuna ardhi kubwa, na kwa maana hiyo kuna haja ya kutoa nafasi ya kila mmoja wao kupanga ni maisha gani anataka, ili mradi asiwe anafuga ng'ombe hapo Loliondo.

Ili afanye maamuzi kama hayo kwa uhuru inabidi 'kumfidia kwa kumjaza mapesa' kama alivyowahi kusema John Cheyo, kiongozi wa UDP.

Kuna msemo wa Kiswahili kuwa 'penye udhia, penyeza rupia,' kwani rupia inayeyusha udhia wote, mtu akijisikia 'hajambo' kwa pesa aliyopata.

Ni moja ya vielelezo vya mitaala ya maumbile, kuwa 'nguvu kuu' ya kisaikolojia katika maisha ni maslahi binafsi, ila 'nguvu dhaifu,' yaani maslahi ya wengi au ya pamoja, ndiyo inaunganisha watu kimaadili au kisiasa, hivyo jadi isitumike kuvuruga.

Inahitaji kuyeyushwa kwa rupia, ila siyo kwa kuwabembelezea hiyo rupia kwani nafsi itaona aibu; ni pale ambapo kuna mjeledi, 'chukua fidia ya pesa uhame, au uhame bila pesa.'

Baada ya mkakati huo kuwekwa, polisi waweke doria maeneo yote kuzuia watu wasiingize mifugo kutoka nje. Ikumbukwe kuwa kuna fedha nyingi katika mifuko ya kimataifa ya kulinda mazingira kwa jumla na hata hifadhi, hivyo 'biashara' kama hiyo haihitaji kuwa mzigo kwa serikali ishirikishe wadau wengine pia.
 
Back
Top Bottom