Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
Na. M. M. Mwanakijiji
Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani Edward N. Lowassa alitoa hotuba wiki chache zilizopita wakati anatangaza nia ya kutaka kuwa mgombea wa Urais kupitia tiketi ya CCM. Katika hotuba yake alielezea kwa kirefu kwanini yeye anafaa kupewa ridhaa hiyo. Aliainisha vipaumbele vyake. Nimejaribu kuchukua hotuba ile na kuiangalia hoja zake na kujaribu kujibu hoja hizo ili tu kuwasaidia watu wengine waone ambavyo sisi wengine tuliona miaka karibu nane huko nyuma; Lowassa hafai kupewa nafasi ya Urais.
Na ni makusudio yangu InShaaAllah, kuwa kwa kadiri atakavyojitahidi kuitafuta nafasi hii nzito na sisi wengine tutajaribu kuwapa wananchi upande ule wa pili ili waweze kufanya maamuzi wakiwa wametumia muda kutafakari matokeo ya maamuzi hayo badala ya kuongozwa na propaganda zilizojaa maneno matamu ya hadaa za kisiasa. Sehemu ya HOJA ni maneno ya hotuba iliyoandikwa ya Lowassa na sehemu ya JIBU LA HOJA ni maoni yangu.
HOJA: Mimi naamini kwamba hata katika kipindi hiki ambapo Watanzania wanaonekana kutaka mabadiliko bado wanaendelea kuamini kwamba watayapata mabadiliko hayo ndani ya CCM. Lakini kama alivyotupa wasia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini, Watanzania wasipoyapata mabadiliko hayo ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Mimi naamini kwamba CCM tunao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka. Tuwape imani na imani hiyo iwe ni ya dhati na ya ukweli kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa uongozi imara wanaouhitaji kwa ajili ya kujenga taifa imara.
JIBU LA HOJA: Miaka zaidi ya hamsini ya utawala wa CCM hawajaleta mabadiliko kwanini tuamini mwana CCM mwingine ambaye amekuwa ndani ya chama hicho hicho na akishika nafasi mbalimbali za uongozi ataweza kuleta mabadiliko kupitia chama kile kile chenye mifumo ile ile ambacho bado kinatumikiwa na kutumika na watu wale wale? Kilichoshindwa kufanyika miaka hamsini na ushee kitaweza vipi kufanyika ndani ya miaka mitano ijayo?
HOJA: Vyama vya siasa vinajumuisha watu na vinaongozwa na watu. Moja ya hulka ya binadamu ni kubadilika kulingana na mahitaji ya mazingira anayoishi. Kwa maneno mengine, binadamu ni dynamic. Kwa sababu hiyo basi, hata vyama vya siasa vinapaswa kuwa dynamic. CCM haijapata kuwa na upungufu wa sifa ya dynamism. Kwa zaidi ya miongo mitano sasa, CCM (na kabla yake TANU na ASP) iliweza kubadili dira na mwelekeo wake ili kwenda sambamba na mahitaji ya Watanzania ya wakati husika. Ndiyo maana tumepita katika vipindi tofauti vya mpito kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto nyingi zilizotukabili.
JIBU LA HOJA: Kwa miongo mitano na zaidi dynamism ya CCM imekuwa na matokeo tunayoyaona. CCM haijawahi kuwa na mabadiliko makubwa yenye manufaa kwa taifa labda tangu baada ya Uhuru na mara baada ya uongozi wa Mzee Mwinyi. Kuanzia kuingia kwa Mkapa na Kikwete dynamism ya CCM imeendelea kuwa na inatishia kuendelea kuwa a catastrophic dynamism. Yaani mabadiliko yenye majanga kwa taifa. Chochote ambacho utawala huu umeahidi kukifanya na ukaanza kukifanya mwisho wa siku kimegeuka kuwa majanga!
HOJA: Kwa maoni yangu ili kuifanya kazi hiyo na kuzikabili changamoto nilizozieleza, nchi yetu inahitaji uongozi wenye sifa zifuatazo:
- Uongozi wenye uthubutu, usioogopa kufanya kufanya maamuzi magumu;
- Uongozi thabiti na usioyumba;
- Uongozi makini na mahiri;
- Uongozi wenye ubunifu na wenye upeo mkubwa;
- Uongozi utakaozikabili changamoto kifua mbele na siyo kuzikimbia;
- Uongozi unaoamini katika mfumo shirikishi katika ujenzi wa Taifa;
- Uongozi unaozingatia muda katika kutekeleza majukumu yake.
Naamini pia kwamba wananchi wanataka Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe na sifa kuu zifuatazo:
- Aweze kuwaunganisha Watanzania (kukabiliana na viashiria vya migawanyiko ya aina mbali mbali inayoinyemelea Tanzania);
- Aweze kuja na sera na mikakati ya kuinua uchumi wa Tanzania na kukuza pato la Mtanzania;ikiwemo kupunguza tofauti ya kipato kati ya aliyekuwanacho na wasiokuwanacho;
- Aweze kuja na sera na mikakati ya kuzalisha ajira kwa vijana wetu;
- Aweze kutokomeza mianya ya rushwa kwa vitendo;
- Aweze kuwa mfano wa kuchapa kazi na kuwajibika;
- Asimamie nidhamu ya matumizi ndani ya Serikali;
- Aweze kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali;
- Aweze kutumia fursa yetu ya kijiografia kibiashara
JIBU LA HOJA: Hivi Lowassa anataka kutuambia kuwa miaka hamsini na ushee ya utawala wa Serikali ya chama chake ambayo na yeye amekuwa sehemu ya uongozi huo huo imekuwa vigumu hivyo kumpata mtu mwenye sifa kama hizi? Mbona hii habari ya hizi sifa za kiongozi ambaye watu wanamtaka si ngeni sana kivile?
Ukiangalia hizi sifa si ndizo hizo hizo alizosifiwa nazo Kikwete wakati watu wanamuuza? Si ndiyo hizo hizo alizoimbiwa Mkapa kuwa ni Msafi? Au watu wamesahau Mzee Mwinyi alipoimbiwa kuwa amekuja na Fagio la Chuma? Si wana CCM lukuki ambao wamewahi kujitokeza kugombea wamedai kuwa na sifa hizi hizi? Kwanini leo ziwe mpya na za kuvutia kutoka kwa mtu ambaye naye alikuwepo kwenye uongozi uliokuwa unadai sifa hizi hizi?
HOJA: Miongoni mwa mafanikio ninayojivunia katika uongozi na utumishi wangu, na ambayo Watanzania wanayatambua na naamini wanayathamini, ni pamoja na:
- Nikiwa Waziri wa Maji chini ya uongozi mahiri wa Rais Mkapa,tulithubutu kushawishi na kuongoza hatua za kukataa kufungika na makubaliano yaliyowekwa na wakoloni ambayo yalikuwa yanazizuia nchi zilizopakana na Ziwa Victoria zisiweze kufaidika ipasavyo na maji ya Ziwa hilo. Leo hii ndugu zangu wa Kanda ya Ziwa wanafaidika na ujasiri wetu katika kukabiliana na suala hilo zito.
- Nikiwa Waziri wa Mazingira, tulipanda miti mingi zaidi kuliko wakati mwingine wowote tokea Uhuru na pia kuwakabili kikamilifu na kuwachukulia hatua waliochafua na kuharibu mazingira.
- Nikiwa Waziri Mkuu, tulisimamia agizo la Rais Kikwete na kufanikisha utekelezaji wake ndani ya miaka miwili kwa kujenga shule nyingi za sekondari kuliko wakati mwingine wowote tokea Uhuru.
- Kipindi hicho hicho, tulisimamia agizo la Rais Kikwete la kuanzisha Chuo Kikuu cha Dodoma na kuhakikisha kinakamilishwa kwa wakati. Leo hii Chuo Kikuu hicho ni fahari ya Tanzania.
Tunapomtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano ni lazima tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika nchi yetu. Na kwa Chama Cha Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia Mwenyekiti wa Chama chetu.
JIBU LA HOJA: Inaonekana Lowassa bila kuwa na madaraka makubwa hawezi kufanya lolote. Amesema kuwa amekuwa Waziri kwa muda mrefu sana tangu wakati wa serikali ya Rais Mwinyi. Hivi kama Mbunge nahata akiwa Waziri ni sheria gani ambayo imetokana na mawazo yake ambayo ilipitishwa na Bunge kukabiliana na mojawapo ya changamoto anazozitaja?
Hapa ameishia hadi miaka saba hivi tu nyuma. Hivi baada ya kuondoka Uwaziri Mkuu Lowassa amefanya nini kitaifa? Ameleta mswada gani Bungeni, ametoa hoja gani kuhusu ajira Bungeni? Ametoa suluhisho gani? Au Watanzania wanatakiwa wampime kwa mambo aliyoyafanya akiwa Waziri tu lakini wasiulize aliyoyafanya akiwa Mbunge? Si mtunga Sheria yeye ametunga sheria gani kutuonesha angalau mwelekeo wa suluhisho la matatizo ya taifa letu?
HOJA: Mimi, baada ya kutafakari kwa kina changamoto tulizo nazo na matarajio na matumaini waliyo nayo Watanzania, naamini kwamba Uongozi imara unaolenga kujenga Taifa imara unapaswa kuwa na dira yenye malengo yafuatayo:
MAJIBU YA HOJA: Tuangalie hivi anavyoita ni vipaumbele vyake:
HOJA: - Kuimarisha Muungano wetu kwa kuyashughulikia yanayotutenganisha na kuyafanyia kazi ili yasivuruge yale yanayotuunganisha ambayo ni mengi zaidi na makubwa zaidi.
JIBU LA HOJA: Kama ahadi ya hili ingekuwa ni mbegu basi ingekuwa imeota mbuyu sasa! Haya matatizo ya Muungano yamekuwa yakizungumzwa tangu 1964. Chama chake kimekuwa kikiongoza Serikali zote mbili kwa miaka zaidi ya hamsini sasa. Bado wanazungumzia kuyashughulikia? Kama hadi leo wao wameshindwa kwanini tuamini kuwa wataweza tena katika miaka mitano ijayo? Siyo kwamba hakuna tena akiba ya fikra bora za kutatua matatizo hayo isipokuwa akiba iliyojaa ahadi zisizowezekana?
Halafu kweli kabisa kuahidi hili ni la lazima hivi? Kwani kuna mwana CCM anayeweza kusema akichaguliwa ataudhoofisha Muungano? Au walioodhoofisha sasa hivi waliahidi watafanya hivyo? Lakini zaidi hajasema ni jinsi gani yeye mwenzetu atashughulikia kuimarisha muungano. Yale yanayotutenganisha ni yapi na atafanya nayo nini yeye kitu ambacho kimeshindwa kufanya hadi sasa?
HOJA: - Kushughulikia matumizi mabaya ya siasa za udini na ukabila kwa kuimarisha siasa zilizoshiba uzalendo na zenye kutuelekeza kwenye Utanzania wetu.
JIBU LA HOJA: Mbona hajasema atafanya nini hasa? Kwa mfano hadi hivi sasa hatujui anasimama wapi kwenye suala la Mahakama ya Kadhi jambo ambalo ni miongoni mwa machungu sana kwa CCM? Au yeye atafanya nini kuondokana na haya mambo; siyo kwamba ni rahisi zaidi kuahidi kwa ujumla tu lakini kukwepa kusema vitu mahsusi atakavyofanya? Hili la kuimarisha siasa zilizoshiba uzalendo unalifanya vipi? Kwa kuwapiga watu bakora? Kuwafundisha?
Au Lowassa na Watanzania wengine wameshasahau ahadi alizotoa Rais Kikwete alipofungua Bunge baada ya kuchaguliwa mara ya kwanza ile Disemba 30, 2005? Si ni kwenye hotuba ile iliyoshangiliwa Bungeni Rais Kikwete aliahidi kufanya mambo kumi ambayo yataimarisha utaifa? Yameshindikana yale? (Kusoma Hotuba ile ya Kikwete tembelea mtandao wa tafakari.com ulinganishe hawa watoa nia na ahadi za JK).
HOJA:- Kujenga uchumi imara na wa kisasa, na ambao ni shirikishi unaomnufaisha kila Mtanzania aliyeko mjini au kijijini.
JIBU LA HOJA: Hivi Lowassa na wengine kutoka chama tawala ambao wanatuahidi kuimarisha Uchumi wanawafikiria vipi Watanzania? Siyo kwamba kila miaka mitano wanatuahidi kuimarisha uchumi? Miaka hamsini baadaye bado haujaimarika au kuna kitu gani kinakosekana?
Kikwete si alituahidi uchumi unaopaa na Lowassa akaja na ndege inayopaa. Wakati ule watu walidhani nimemnanga tu; jamani hiyo ndege haipai tu miaka yote hii? Inatumia mafuta ya taa? Au watu watoke waisukume?
HOJA: - Kukuza kipato cha wananchi na kunyanyua hali za maisha ya watu wetu. Tunapaswa kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi tunaouzungumzia unamnufaisha Mtanzania aliyeko mjini au kijijini na kwamba hali za Watanzania wa matabaka yote zinanyanyuka na kwamba wanaridhika na kuuona uhalisi wa ukuaji wa maendeleo tunayoyazungumzia.
JIBU LA HOJA: Hivi ataweza vipi kukuza kipato cha wananchi wa matabaka yote wakati yeye na wabunge wenzie wameomba wapewe kifuta jasho cha kutumikia miaka mitano cha karibu milioni 200 na ushee kwa kila Mbunge? Hivi, watainua vipi kipato cha wananchi wakati wao (wabunge, mawaziri n.k) kipato chao ni karibu mara 45 zaidi ya kipato cha mwananchi wa kawaida?
Wakati wa Nyerere mshahara wa Rais ulikuwa kama mara 12 ya mshahara wa mwananchi wa kawaida leo hii mshahara wa Rais wa Tanzania ni karibu mara 80 ya kipato cha mwananchi wa kawaida. Je, Lowassa akiingia atapungusha mshahara wa Rais au ataongeza kima cha chini bila kuongeza mishahara ya juu? Au kwa vile kasema yeye bado anautaka utajiri zaidi basi tusije kushangaa akaongeza mshahara wa Rais (of course kwa kutumia taratibu zilizopo) na kuwa mara hata 100 zaidi ya kipato cha mwananchi wa kawaida?
Halafu hivi anafikiria Watanzania wamesahau ahadi ya kushughulikia "umaskini wa kipato"? yaliishia wapi?
HOJA:- Kuondokana na sifa mbaya ya kuwa Taifa ombaomba. Kwa wingi wa rasilimali tulizo nazo na neema ya ardhi, maziwa, mito na bahari Tanzania tuna kila sababu ya kuacha kuwa bakuli la ombaomba na badala yake kuwa mkoba wa neema katika Afrika.We can transform our nation from being the begging bowl to become the bread basket of Africa.
JIBU LA HOJA: Hili mbona halionekani kuwa lina ukweli ndani yake? Siyo yeye aliyeenda kuomba mafundi wa kutengeneza mawingu ya mvua toka Thailand miezi michache kabla ya yeye kujiuzulu na kabla ya aliowaomba kupinduliwa? Hivi miaka yote hii karibu sasa tangu aache Uwaziri Mkuu ameleta hoja, mswada au wazo gani Bungeni ili kulifanya taifa lisiwe la ombaomba?
HOJA: - Kujenga mfumo mpya wa elimu unaojielekeza kuwatayarisha vijana wetu waweze kuajirika, kujiajiri na kushindana katika soko la ajira. Tumepiga hatua kadhaa katika elimu lakini kiwango cha elimu bado ni hafifu. Pamoja na kuwa na shahada (degrees), bado wahitimu wetu hawawezi kushindana kwenye soko la ajira. Wakati tunazungumzia kuunganisha soko la ajira katika Afrika Mashariki,hatuna budi kujikita kubadili mfumo wetu wa elimu na kuuelekeza kwenye mafunzo ya ufundi na stadi yanayowajenga wahitimu wetu kuwa wabunifu na wenye kujiamini katika kukabiliana na changamoto za maendeleo duniani.
JIBU LA HOJA: Hili suala la elimu mbona ni kama wanazungusha pia; hivi kuna chama ambacho kimejaribu kuboresha elimu yetu kuliko CCM kwa miaka yote hii. Au amesahau tulishakuwa na mipango ya kila namna ya kuboresha elimu? Sasa kwanini haiboresheki? Kuanzia MMEP, MMEM, MKUKUTA, MKURUBITA, MTUKUTU, MFILISIKA HADI MFISADIKA; mipango yote hii imeshindikana ina maana hatimaye sasa amepata jawabu? Kwanini hajalitoa hilo wazo miaka hi inane Bungeni ili kusaidia? Au alipojiuzulu Uwaziri Mkuu na wazo la kutoa mawazo ya kuliinua taifa likafahadi Watanzania wampe Urais na wasipompa na mawazo hawapi ngo?
Kwenye ile hotuba ya Kikwete mbona nay eye aliahidi makubwa tu kwenye elimu? Mbona Kikwete aliahidi mambo kumi na moja kuyafanya na kati hayo kumi na moja anayoahidi Lowassa leo hii yamo ndani? Siyo kwamba anatuambia chama chake na serikali yake wameshindwa kuboresha elimu hii na sasa wanataka nafasi nyingine ya kujaribu tena? Si akubali kwanza sera ya CCM ya elimu imeshindwa?
HOJA: - Kuhakikisha tunakabiliana ipasavyo na kulipunguza kwa kiasi kikubwa kama si kulimaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama. Ni jambo la kusikitisha kwamba tumezungukwa na mito na maziwa lakini bado watu wetu hawana maji ya kunywa hata ndani ya Dar es Salaam.
JIBU LA HOJA: Suala la maji mbona ni kama elimu vile vile? Anachoahidi Lowassa leo mbona kilishaahidiwa na Kikwete na kabla yake Mkapa vile vile? Kikwete alisema hivi kwenye ile hotuba yake: Ni makusudio yangu kuwa tuwe na Mpango Kabambe wa Maji kwa nchi nzima. Mpango ambao utajumuisha mikakati na mbinu mpya za kutekeleza kwa kasi Sera ya Maji na kutatua tatizo la maji. Aidha, tutakamilisha miradi mikubwa ya ukarabati na upanuzi wa Majisafi na Majitaka Dar es Salaam, na ule wa kupeleka maji katika miji ya Kahama, Shinyanga na vijiji vitakavyopitiwa na bomba kutoka Ziwa Victoria.
Sasa leo Lowassa anatuahidi nini jipya? Inakuwaje watu wanashangilia lile lile kutoka hazina ile ile ya fikra? Mbona hakuna jipya hapa? Miaka tisa baadaye ile miradi mikubwa ya majisafi na majitaka ya Dar imekamilika? Na watu wa Dar bado wanamuangalia Lowassa kama sehemu ya suluhisho au ilikwama kwa sababu yey ehakuwemo tena serikalini na akagoma hata kukukumbushia Bungeni?
HOJA:- Kujenga na kusimamia mfumo imara wa kutekeleza sera na sheria tunazozitunga na kuzipitisha kwa lengo la kumtumikia Mtanzania na kumjengea uwezo wa kubadili maisha yake ili tuweze kwenda sambamba na viwango vya kimataifa. Tanzania imepata sera na sheria nzuri sana lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu. Tumekuwa wepesi wa kutunga sera na sheria lakini wazito mno wa kuzitekeleza na kuzisimamia. Uongozi imara wenye kulenga ujenzi wa Taifa imara utahakikisha tunakuwa mfano wa utekelezaji wa sera na sheria tulizo nazo na mpya zitakazotungwa kukabiliana na malengo tuliyojiwekea.
JIBU LA HOJA: Hivi kweli Lowassa na wengine wanaamini kabisa kuwa Tanzania ina sheria na sera nzuri? Kama hili lingekuwa kweli tungekuwa hapa kweli? Hivi amesahau kabisa orodha ya sheria mbalimbali 40 ambazo zilioneshwa miaka karibu ishirini nyuma kuwa hazifai lakini bado zimo vitabuni? Siyo kwamba hata majuzi tumepitisha miongoni mwa sheria mbovu kabisa kupitishwa na nchi ya kidemokrasia? Hizi sera nzuri kama zingekuwa nzuri hivyo si watu wangejitahidi kuzitekeleza? Siyo kwamba sera zenyewe ni mbaya maana kama zisingekuwa mbaya Lowassa na hawa watangaza nia iweje leo wanazungumzia mabadiliko? Wanabadilisha nini sura za watekelezaji? Mbona hili tumekuwa tukilifanya kila baada ya miaka mitano?
Hayo ndiyo mambo Lowassa na timu yake wanasema watayafanyia kazi kama watapata ridhaa. Sisi wengine tunauliza mbona hamna jipya? Mbona hii lugha ya ahadi hizi ni kama tunaifahamu na tumeizoea? Labda tutakapoangalia kile anachoita ramani ya uongozi labda tutaona mambo mapya lakini hadi hivi sasa kwa maoni yangu na nina uhakika wengine watakubaliana nami Lowassa bado hajatuambia jambo jipya la kutufanya tuamini kuwa anafaa kupewa nafasi nyingine. Inaonekana endapo atakubaliwa kuwa Rais itakuwa ni mwendelezo wa watu wale wale wenye fikra zile zile kutoka chama kile kile; na sichelei kusema itakuwa ni awamu ya tatu ya fikra za utawala wa Rais Kikwete.
Watanzania hawajachoka bado? Bado hawajakoma?
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com