Kamati yaanza kuichunguza Richmond, watu maarufu wahojiwa
Muhibu Said na Mwanaid Omary
KAMATI Teule ya Bunge ya Kuchunguza mchakato wa zabuni ya uzalishaji umeme wa Kampuni ya Richmond Development (RDC), imeanza kuwahoji watu maarufu, akiwamo Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA).
Wengine waliokwisha kuhojiwa na kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dk Harrison Mwakyembe ni Msajili wa Makampuni na Ofisa kutoka Kampuni ya Usajili katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko (BRELA).
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe, alisema walianza kazi hiyo kwa kukusanya na kupitia nyaraka muhimu zinazohusiana na Richmond.
Alisema wanatarajia kuendelea na kazi hiyo iliyoanza Novemba 15, mwaka huu kwa wiki mbili zijazo kwa kufanya uchunguzi katika taasisi mbalimbali za serikali, ikiwamo Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme nchini (Tanesco).
Dk Mwakyembe alisema mikutano ya utendaji kazi wa kamati hiyo, inafanyika kwa sura ya kimahakama kwa wanaohojiwa kuapishwa na wanaohitajiwa na kamati kupelekewa hati maalum ya wito.
Aliwataka wananchi ndani na nje ya nchi wenye taarifa au nyaraka zozote kuhusu Richmond waziwasilishe katika Ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa, ushauri utakaowasilishwa, utalindwa chini ya sheria za Bunge.
"Tupo hapa (Ofisi za Bunge) kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 12 jioni," alisema Dk Mwakyembe na kuongeza kuwa hawategemei kusafiri kwa kuwa nyaraka zote muhimu wanazo.
Hata hivyo, alionya atakayewasilisha taarifa au nyaraka za uongo, kutia chumvi au za kughushi, atakuwa amefanya kosa la jinai kwa mujibu wa sheria.
Pia aliwataka waandishi wa habari kuhakikisha taarifa zote zinazohusu kamati hiyo watakazozitangaza zinatoka katika vyanzo vya kuaminika.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stella Manyanya ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum, alisema kamati hiyo haitaficha ukweli na itakuwa tayari kuuarifu umma hata kama itabainika kuwa kigogo alihusika.