MBUNGE wa Monduli, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ametahadharisha mjadala kuhusu Katiba nchini kuwa chanzo cha kuharibu wa amani iliyoko nchini.
Lowassa alitoa tahadhari hiyo jana wakati akifungua studio ya muziki ya FLEM, jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa hivi sasa inaoneka kuwapo kwa mashindano ya kuharibu amani kutokana na mjadala huo kupamba moto.
Alisema kuwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo moyo wa kuharibika kwa amani unavyozidi kuongezeka.
Alisisitiza kuwa hata katika mijadala mbalimbali inayoendelea nchini hasa ya Katiba, wananchi wanatakiwa kupingana kwa hoja na si kwa kuhatarisha amani.
"Tunatakiwa kutunza amani yetu kama mboni ya jicho maana hata nchi jirani za wenzetu ikiwamo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi hawajawahi kuwa na amani kama tuliyonayo sisi, hivyo tunatakiwa kuhakikisha tunaitunza kwa uwezo wetu wote," alisema Lowassa. Katika kusisitizia hilo, aliwashauri waimbaji wa Injili kuamka la kutunga nyimbo zinazohamasisha na kuchochea utunzaji wa amani, ili iendelee kudumu.
"Waimbaji wa Injili wanafanya kazi nzuri sana ingawa katika maisha kuna mahali unayumba, unaanguka na kupanda, lakini yote hayo ni kwa uwezo wa Mungu.
"Hakikisheni mnatunga nyimbo za kutetea amani maana kwa sasa kila mtu ana lake analosema, vyombo vya habari vinachochea kwa njia yake, hivyo tuilinde hii amani," alisema.
Alisema kuwa bila kuwa na amani hakuna taifa linaloweza kufikia maendeleo, hivyo jamii inapaswa kupingana bila kusababisha mvurugano.
Alisema amani ni tunu pekee aliyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hivyo tunatakiwa kuitetea kwa nguvu zetu zote.
Alisema kuwa ni kipindi cha ajabu sasa, kwani kila mtu amekuwa akiamka na jambo lake linaloonekana kuhatarisha amani.
Kwa upande wake, mchungaji wa kanisa la FPCT la Mtoni Kijichi, Joseph Malundo, aliwataka wamiliki wa studio hiyo kuacha kubweteka na mafanikio hayo bali wazidi kumuomba Mungi ili azidi kuwapandisha juu zaidi.
Alisema hatua hiyo itawezesha vijana wengi kupata ajira hasa kwa kumtumikia Mungu.