SoC01 Maabara ni uti wa mgongo wa Huduma bora za Afya Tanzania

SoC01 Maabara ni uti wa mgongo wa Huduma bora za Afya Tanzania

Stories of Change - 2021 Competition

Bengarulu

Member
Joined
Apr 12, 2014
Posts
17
Reaction score
17
MAABARA NI NINI

Maabara ni jengo maalumu lilojengwa mahususi lilosheheni mashine na vifaa maalumu (machine and equipments) na vitendanishi (reagents) kwa ajili ya kufanya majaribio (trials), vipimo (tests) mbalimbali kulingana na mahitaji. zipo maabara za aina nyingi sana kama vile maabara za tiba, maabara za kemikali, maabara za tafiti za chanjo, maabara za madawa na nyingine nyingi ila leo napendelea kuongelea maabara za tiba (Clinical Laboratory). Maabara ya Tiba lengo lake mahususi ni kufanya vipimo mbalimbali kwa kutumia sampuli ya mgonjwa kama vile damu, mkojo, makohozi n.k ili kubaini uwepo au kutowepo kwa ugonjwa, kufuatilia muenendo wa matibabu ya mgonjwa na kuangalia hali ya utendaji kazi wa mwili kwa kuchunguza seli,analytes na metabolites kiwango cha virutubisho.

Maabara ya tiba imegawanyika kwenye sehemu tofauti tofaui zinazoitwa idara (unit) ambapo kila idara imetengwa kufanya kazi yake mahususi ili kutimiza malengo ya maabara nzima kwa ujumla. Idara hizo ni Kemia uhai (clinical chemistry), Mikrobiolojia (microbiology), Parasitoloji (Parasitology), Hematolojia (Hematology) kwa pamoja zinaunda Clinical Pathology Laboratory. Baadhi ya taasisi kubwa zenye Central Pathology Laboratory zina mabara ya Anatomical Pathology iliyogawanyika kwenye histopatholojia (histopathology na saitolojia (cytology).
Maabara za tiba zinaweza kuwepo kwenye hospitali au kituo cha afya (attached lab) au ikawa inajitegemea yenyewe (stand-alone lab).

KAZI YA MAABARA YA TIBA

Kwenye utoaji wa huduma bora za afya maabara imekua kiungo muhimu kwenye utabumbuzi wa magonjwa (Diagnosis), kufuatilia muenendo na maendeleo ya matibabu ya wagonjwa, (monitoring) kufuatilia ubora wa dawa n.k. Maabara ya tiba imekua kitovu cha tafiti za kiafya tafiti ambazo zinatoa takwimu za hali ya maambukizi (prevalence) ya magonjwa mbalimbali kama vile Malaria, Kifua kikuu, virusi ya Ukimwi na Covid-19. Takwimu zinazosaidia watunga sera na mamlaka kupanga mikakati ya kiutendaji kwa ushahihi.

Kutokana na utafiti uliofanywa na professor Tony Badrik wa chuo kikuu cha patholojia nchini Australaria (Australaria college of Pathology) ilibainika ya kuwa, asilimia 70 (70%) ya maamuzi ya kitabibu (clinical decisions) yanategemea uchunguzi wa maabara. Kwa mfano kuamua mgonjwa huyu apatiwe dawa fulani kwa muda fulani inategemeana na majibu ya vipimo vyake vyilivyopelekwa maabara. Baadhi ya Medical procedures zinategemea kwa kiasi kikubwa majibu ya vipimo vya maabara kabla havijafanyika, kwa mfano ili mgonjwa apelekwe kufanya baadhi ya vipimo ya mionzi (radioimaging tests) kama vile MRI na CT- scan ni lazma apimwe utendaji kazi wa figo lake kwanza (renal function test). Ili wataalamu wa mionzi wajue ni kiasi gani cha dozi ya radiopharmaceuticals anachotakiwa kupewa mgonjwa wakati wa procedure.

Pia maabara inafanya uthibitisho wa uwepo au kutokuwepo kwa ugonjwa fulani baada ya uchunguzi mfano aliyekua Waziri wa Afya 2020 Mh. Ummy Mwalimu alitangaza uwepo wa ugonjwa wa covid-19 nchini kufuatilia vipimo vya maabara

Kwenye sekta ya afya kote duniani kwa sasa iko vitani kupambana na usugu wa madawa (drug resistance) hususani dawa dhidi ya bakteria (antibiotics). Maabara imekua mstari wa mbele kupambana na janga hili ambalo linatabiriwa kuwa tishio zaidi siku za usoni. Ili kuhakikisha jamii inakua salama dhidi ya usugu wa madawa, maabara inafanya kipimo cha kuotesha bakteria (Culture) na kuwachunguza dawa zinazowafaa (sensitivity). Culture inahusisha kuotesha bakteria kutoka kwenye sampuli ya mgonjwa inaweza kuwa damu, mkojo, kinyesi n.k (kutokana na ugonjwa unaohisiwa), maabara wataotesha bacteria aliyopo kwenye sampuli ya mgonjwa ambae ndiye anayemsumbua mgonjwa, baada ya bakteria kuoteshwa atafanyiwa Sensitivity test kujua ni aina gani za dawa na kiwango cha dozi kinachomfaa mgonjwa kutibu ugonjwa huo.

Culture na Sensitivity imekua msaada mkubwa wa kuhakikisha mgonjwa anapatiwa matibabu sahihi dhidi ya bakteria, hivyo kupunguza uhatari (risk) wa kupata usugu wa madawa (drug resistance).

HISTORIA YA HUDUMA ZA MAABARA YA TIBA NCHINI TANZANIA

Huduma za maabara ya tiba nchini zilianza rasmi mwishoni mwa karne ya 19 wakati wa utawala wa Kijerumani. Mnamo mwaka 1987 maabara ya kwanza ya serikali ilijengwa Ocean road Dar es salaam, maabara hiyo ya Ocean road iliwahi kutembelewa na mwanasayansi na mtafiti nguli duniani Dk. Robert Koch aliyefika kwenye maabara hiyo na kufanya kazi zake wakati alipokua anafanya tafiti zake za malaria na homa ya malale ukanda huu wa Afrika mashariki.

Maabara ya Ocean road Dar es salaam iliendelea kukua hadi kufikia kuwa Central Pathology Laboratory baada ya uhuru chini ya Wizara ya Afya. Kuanzia kipindi hicho hadi leo hii huduma za maabara zimienea nchi nzima kwenye ngazi tofauti tofauti za hospitali, vituo vya afya na zahanati. (attached laboratories) na zile maabara zinazojitegemea (stand-alone laboratory)

HALI YA HUDUMA ZA MAABARA ILIVYO SASA NCHINI

Kwa takribani ndani ya miaka 20 iliyopitaa hadi sasa kumekua na mageuzi makubwa sana kwenye taaluma ya maabara nchini. Mageuzi haya yamesababibwa na ongezeko la wataalamu wa maabara kwenye madaraja tofauti tofauti ya kielimu, Utandawazi, Uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa huduma za Maabara, Kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za maabara (demands) na kuongezeka kwa sera na kampeni juu ya uboreshaji wa huduma za Afya nchini. Kutokana na baadhi ya sababu tajwa hapo nyuma Huduma za maabara zimeendelea kukua na kuimarika kila kukicha na kuweza kufanya kazi zake kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa. Maabara imekua mstari wa mbele kwenye mchakato wa kuzuia (prevention) kuvumbua (diagnosis) na kufuatilia muenendo (monitoring) wa magonjwa mbalimbali yanayowakabili watanzania. Kuongezeka kwa Maabara zilizoidhinishwa (Accredited) na taasisi mbalimbali za kimatifa zinazosimamia Ubora wa Maabara ulimwenguni kote ni kiashiria cha kukua kwa kada ya maabara nchini.

CHANGAMOTO

Licha ya hatua tulizopiga kwenye huduma za Maabara nchini zipo changamoto kadha wa kadha zinazofubaza upatiakanaji wa huduma bora za maabraa. Kama tuliangalia huko juu Maabara ni uti wa mgongo wa huduma bora za afya, dosari yeyote inayotokea kwenye huduma za maabara haibaki maabara pekee bali itaendelea kwenye mfumo mzima wa utoleaji wa huduma za afya.

Zipo changamoto nyingi kwenye huduma za maabara ambazo baadhi yake ni kama ifuatavyo;

  1. Upungufu wa watalalamu wa Maabara, hii ni changamoto kubwa inayopunguza ufanisi wa shughuli za kila siku za maabara. Rasilimali watu kwenye kada ya maabara bado ni kizungumkuti. Licha ya vyuo vya kati na vikuu nchini na nje ya nchi kuzalisha wataalamu bado upungufu ni mkubwa ambao kwa namna moja ama nyingine unasababisha upatikanaji wa huduma za maabara usiwe rafiki ikiwemo uwepo wa muda mrefu wa kusubiri majibu ya vipimo jambo ambalo baadhi ya watu wanakua na mtazamo hasi juu ya huduma za maabara wakiamini ni sehemu ya kwenda kusota na kupoteza muda.
  2. Uelewa finyu juu ya huduma za Maabara na kada nzima ya Maabara kwa ujumla, Kada ya Maabara ni uti wa mgongo wa huduma bora za afya ulimwenguni kote lakini changamoto kubwa kwenye kada ya Maabara jamii haina uelewa wa kutosha au naweza kusema wengi hawaijui na wachache wanaoifahamu hawajui thamani yake. Hii sio Tanzania pekee bali ni ulimwenguni kote. January 30 mwaka 2015 mwaadada Lisa Esposito, Mwandishi wa habari za Afya nchini Marekani aliandika Makala aliyoipa kichwa kilichosomeka “Unseen Proffesionals detect crucial health Information from your medical tests”, kwenye moja ya Digital media kubwa nchini Marekani inayoitwa World reports Us news. Lisa ameendika Unseen professionals (Wataalamu wasioonekana) akimaanisha ni watu ambao wanafanya kazi zao kwenye majengo maalum ambayo hayafikiwi na watu wa kawaida hivyo hawaonekani na watu wanapokua wanafanya kazi zao ila licha ya kutoonekana kwao ni watu ambao wanapata taarifa nyingi na muhimu za kiafya kupitia tu kwenye vipimo wanavyowafanyia wagonjwa wao. Licha ya kutotambulika ila pia wanakosa hata recognition na appreciation kitu kinachopunguza ari na morali ya kazi, mfano kila mwaka ifikapo mwezi Aprili linatengwa juma nzima kwa ajili ya maadhimisho ya wiki ya Maabara ulimwenguni kote ambayo kwa mwaka huu wiki ya maabara iliadhimishwa juma liloanzia tarehe 20, ya mwezi Aprili na maadhimisho hayo Tanzania kitaifa yalifanyika mkoa wa Simiyu lakini sio ajabu hata wakazi wa Simiyu hawakufahamu, hakuna hata tweet au post ya kiongozi yeyote aliepost tu kuwapogeza watalamu wa maabara kama wafanyavyo kwenye siku za wauguzi, matabibu n.k
  3. Vifaa tiba na vitendanishi, hivi ni vitendea kazi vya wataalamu wa maabara kwenye shughuli zao za kila siku, hivyo kukosekana au kuchelewesha kupatikana kunaleta athari za moja kwa moja kwenye utoaji wa huduma za maabara ikiwemo kutoweza kutoa kwa wakati majibu ya wagonjwa hivyo kushindwa kuchangia maamuzi ya kitabibu jambo ambalo linadidimiza ufanisi wa huduma kwa wagonjwa. Changamoto hii inasababishwa na gharama kubwa za vifaa tiba na vitendanishi na kucheleweshwa kwa mchakato wa manunuzi kwa baadhi ya taasisi au kutoweka kipaumbele kwenye manunuzi. Pia baadhi ya taasisi zinakosa mzabuni wa uhakika anaweza kuwasambazia vitendanishi kwa wakati.
MAPENDEKEZO
Maabara ni nyenzo muhimu sana kwenye sekta ya Afya. Kukua na kuendelea kwa huduma za maabara ni mafanikio na ukuaji wa kada nyingine za afya na sekta nzima ya afya kwa ujumla. Uchunguzi sahihi wa magonjwa ndio nguzo ya kupata tiba sahihi, hivyo basi serikali,wahisanin wadau na jamii nzima kwa ujumla hatuna budi kuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zinazoikabili kada ya maabara, ili kuleta ufanisi wa huduma za maabara napendekeza yafuatayo;
  1. Kuajiri wataalamu wa maabara wa kutosha na wenye uwezo, kuongezeka kwa nguvu kazi kutasaidia kupunguza work load iliyopo ili kuongeza ufanisi wa huduma za maabara na kwa wakati.
  2. Kuthamini na kutambua kwa usawa michango ya kada zote za kiafya kwenye mchakato nzima wa utoaji wa huduma za afya, italeta usawa na motisha kwa wafanyakazi wa kada zote afya hivyo watafanya kazi kwa moyo.
  3. Ili zoezi la manunuzi la vifaa tiba na vitendanishi likamilike kwa wakati na kwa usahihi ni vyema kila kada iwe na wataalamu wa manunuzi (procurement officer) ili iwe rahisi na haraka kukamilisha mchakato kwani kila kada wanafahamu vipaumbele vyao hivyo ni rahisi kufanya maamuzi yenye tija unaponunua kitu unachooenda kutumia mwenyewe kuliko unachoagizwa
  4. Wawekezaji na wafanya biashara kwenye sekta ya afya na nyinginezo waingie kuwekeza kwenya Maabara pia, licha ya faida watayoipata watakua wamesaidia jamii kupata matibabu sahihi
  5. Kuboresha maslahi ya wataalamu wa maabara kwani itakua chachu ya kufanya kazi kwa bidii na weledi uliotukuka na pia hata vizazi vijavyo vione kuna haja ya kusoma kada ya maabara.
  6. Kusambaza huduma bora za maabara kwa ngazi za chini za maabara kama vituo vya afya na zahanati ambako kwa sasa huduma nyingi zinazopatikana ni zile tu za msingi.
Mwisho Naomba kura yako, Maoni yako, Ushauri kwenye comments pia kama hutojali naomba share kwa wengine. Ahsante sana.
 
Upvote 18
Hakika maabara ni muhimu sana katika sekta ya afya ingawa imekuwa haionekani kuwa muhimu kwasababu haitambuliki rasmi kama uti wa mgongo katika afya
 
Back
Top Bottom