Maamuzi magumu ya wazazi/walezi chanzo cha kuharibikiwa kwa watoto.

Maamuzi magumu ya wazazi/walezi chanzo cha kuharibikiwa kwa watoto.

emaJenerali

Member
Joined
Mar 7, 2014
Posts
11
Reaction score
1
KILA mzazi anapenda kuona maendeleo ya mwanae yanafanikiwa kwenye maisha. Lakini Jitihada za mzazi/Mlezi zinafikia kikomo pale mtoto anapoonesha ukaidi wa kutosikia maoni, ushauri, na hata mafundisho ya Mzazi/mlezi na kujikuta akiangukia mikononi mwa wananchi wabaya na kukumbwa na madhila.

Lakini pamoja na ukaidi huo wa mtoto, wazazi huwa wa mwisho kuchukua maamuzi ya kumtelekeza mtoto pindi anapoonekana hafundishiki wala haambiliki. Wahenga wanasema uchungu wa mtoto aujuaye ni mzazi. Pamoja na ukaidi wa mtoto, mzazi hujitahidi kwa hali na mali kumrudisha mwanae kwenye njia ya malezi ili asikutane na madhila ya walimwengu.

Aidha, uchungu wa mzazi kwa mtoto wake huwa na kikomo hasa pale mtoto anapo hisi yuko juu ya wazazi/walezi wake.

Ikifikia hatua hiyo, wazazi/walezi wengi hujiweka pembeni kwa maana kwamba anamwacha afanye analotaka kufanya bila kumpa ushauri wala mafundisho ya kumrudisha kwenye misingi ya malezi. Kwa wale watoto ambao wamebahatika kupata elimu, basi anamwona baba au mama yake hawawezi tena kumwongoza kutokana na kwamba wanao mlea labda hawakufikia elimu aliyo fikia yeye.

Wakati mwingine maamuzi ya familia pamoja na majukumu mengine ya kifamilia anayaendesha yeye kwasababu tu eti amesoma kuliko wazazi wake.

Ikifikia hatua hiyo , kama mtoto amefikisha umri wa kuweza kujitegemea (miaka 18), mzazi/mlezi hujikuta pamoja na kwamba si kwa mapenzi yake ila kwa utukutu wa mtoto anakusudia kumfukuza mwaanae nyumbani.

Mara nyingi sababu kubwa inayomtenganisha Mzazi na mwanae ni kutomithilika kwa tabia ya Mtoto. Kuna methali inayosema asiyefundishwa na wazazi hufundishwa na ulimwengu, hapo ndipo mzazi anaponyoosha mikono na kumkabidhi mtoto wake kwa Walimwengu ili wamfundishe.

Kuna mfano mzuri, watoto wa mitaani walio wengi wamekimbizwa nyumbani kutokana na tabia zao, kuna wale wachache ambao wamekimbia nyumbani kutokana na hali ngumu ya maisha ya wazazi, pamoja na wazazi kuwatelekeza lakini wengi wanao kimbia nyumbani hutokana na kutomidhilika kwa tabia zao.

Kuna tabia ambazo wazazi wanashindwa kuzivumilia kwa mfano, tabia kama udokozi, umalaya, uzembe uliokithiri, kiburi, ujambazi, pamoja na nyingine kama hizo ambazo zinamfanya mzazi achukue maamuzi magumu kwa mwanae.

Nilifanya mahojiano na Marium Saimoni ambaye kwa namna moja au nyingine amejiingiza kwenye biashara ya kujiuza (Umalaya) sababu ambazo zilimfanya mama yake ashindwe kuvumilia tabia ya mwanae na kuamua kumkabidhi kwa walimwengu ili wamfundishe.

Kabla dada huyu hajaanza kujihusisha na biashara ya kujiuza, anaeleza historia yake kwamba walikuwa wakiishi Mwanza na wazazi wake wote wawili, kwa bahati mbaya baba alifariki akiwa bado mdogo kwa hiyo malezi aliyapata kwa mama zaidi .


Dada huyu, anaeleza aliacha shule akiwa darasa la tatu kitendo ambacho kilimlazimu kukaa nyumbani na kusaidia kazi za nyumbani pamoja na mama yake.


Sababu za Marium kuacha shule zinasikitisha, anasema alibakwa na vijana ambao hakuwajua wakati akienda shuleni, kitendo ambacho kilimpa wasiwasi wa kuendelea na shule.


Dada huyu anasema kabla hajaacha shule mama yake alikuwa anamjali kwa kumtimizia mahitaji yote ya shule japo kuwa walikuwa kwenye familia yenye dhiki.


Dhiki anayoieleza Marium ni ile ya kuishi chini ya dola moja kwa siku.Kula mlo mmoja kwa siku ilikuwa ni kitu cha kawaida kwao.


Baba yake alikuwa ni mfugaji, Mama yake alikuwa ni mama wa nyumbani kwa hiyo fedha zilizokuwa zinapatikana kwa ajili ya mauzo ya mifugo zilitumika kuendeshea familia kwa chakula pamoja na kuwasomesha kaka zake pamoja na shughuli nyingine za kifamilia.


Anaeleza, baada ya baba yake kufariki, maisha ya familia yakawa magumu kutokana na baba alikuwa muhimili wa familia katika kuendesha majukumu ya kifamilia, hapo ndipo alipoanza kuona madhila ya dunia kutokana na wakati mwingine walikuwa wanashinda na mlo mmoja kwa siku. Anaeleza Marium


Kwa sababu mama yake alikuwa ni mama wa nyumbani na hakuwa na kazi yoyote itakayo mwingizia kipato, alimshawishi Marium kwenda kufanya kazi kama mfanyakazi wa ndani (house girl) kwa jirani yao ili wapate fedha ambazo zingesaidia kuendesha maisha ya pale nyumbani.


Hata hivyo, Mariam alikubali na alifanya kazi ile kwa mwezi mmoja, mwezi uliofuata alifukuzwa na baba mwenye nyumba kwa madai kwamba alikuwa hana nidhamu.

Maisha yaliendelea, anaeleza yalikuwa ni maisha ya kubangaiza ilifika wakati mifugo iliyoachwa na baba yake ilikwisha kutokana na usimamizi mbovu wa mali za baba yake ambapo wazo la kuhamia mjini lilimjia mama yake. Marium anasema hakumbuki ni mwaka gani hasa walikuja Dar es Salaamu lakini anahisi ni mwaka wa 2002.

Ni Baada ya mama yake kuuza mali zote zilizoachwa na baba yake ikiwemo nyumba aliyokuwa ameijenga baba yake kipindi akiwa hai.

Anaendelea kueleza, Walihamia Tabata ambapo ni karibu na ndugu zao wa ukoo mmoja walio kuwa wanaishi Tabata. Walipata kiwanja huko Tabata wakajenga chumba kimoja na banda la uwani ambapo nyumba hiyo iliwawezesha kujisitiri ili waweze kutafuta maisha mengine.

Wahenga wanasema, ng'ombe wa maskini hazai na hata akizaa huzaa dume, baada ya kuishi takribani miaka kumi kwenye nyumba hiyo maeneo ya Tabata kando ya Mto Msimbazi mafuriko yaliyotokea mwaka jana yalisababisha nyumba yao kujaa maji na kubomoka. Hapo ndipo serikali ilipowaonea huruma na kuwapeleka Mji mpya (Magupande).

Hii ndio historia fupi ya Maisha ya Marium ya kilicho wafanya watoke Mwanza na kuja Mjini (Dar es Salaam) na sasa wako Mji Mpya (Magupande).

Kitu gani kilichomfanya mpaka akajiingiza kwenye Umalaya.
Pamoja na kazi yake ya kujiuza, Marium ni Mama mwenye watoto wawili, anasema ameingia kwenye biashara ya Ukahaba kutokana na hali mbaya ya maisha aliyotokea, pia kwasababu ya kukosa elimu ambayo itamwezesha yeye kuajiriwa kwa maana kwamba elimu yake ni ya kuishia darasa la tatu.

Watoto wote wawili amewapata wakati akifanya biashara ya kujiuza na kila mmoja amemzaa na wanaume tofauti.

Anasema mara ya kwanza alipoanza kujihusisha kwenye ukahaba, alikutana na dada mmoja ambaye jina lake tunalo, ambaye alikuwa ni mzoefu kwenye biashara ya ukahaba.

Dada huyu alikuwa anaishi jirani na Marium ambapo alitazama maisha anayoishi Marium ndipo alipopata mwanya wa kumshawishi ili wajiunge naye kwenye biashara hiyo.


Kutokana na maisha ya shida ambayo Marium alikuwa anaishi pamoja na mama yake, aliamua kujiingiza kwenye biashara hiyo ya kujiuza ambapo dada huyo alimshawishi kwa malezo kwamba kazi ya kujiuza ina hela jambo ambalo Marium anasema aliona kama ukombozi kwake.

Marium anaendelea kueleza kwamba siku ya kwanza walitoka na dada huyo ili amfundishe jinsi atakavyo wavutia wanaume ili wamchukue (kwa nia ya kujiuza) na ndipo siku hiyo ya kwanza alipopata mwanaume (mteja) ambaye waliondoka nae kwa makubaliano kwamba angempatia kiasi cha fedha lakini anasema hakumtajia kiasi gani cha fedha.


Anaeleza, walipofika njiani wakielekea nyumbani kwa huyo mwanaume, walikuja wanaume wengine watatu bila makubaliano yoyote wakamshika kwa nguvu na kumbaka.

Tukio hili la kubakwa lilimfanya akae nyumbani kwa muda wa wiki mbili akiwa anauguliwa maumivu, anasema kutokana na uhaba wa fedha hakwenda hospitali kupima afya yake kujua kama ameambukizwa magonjwa ya zinaa au la, alitumia njia za asili kujitibu mfano kujikanda na maji ya moto, pia alitumia dawa za asili alizokuwa analetewa na mama yake.


Katika maelezo yake tukio kama hili la kubakwa sio mara ya kwanza kumtokea, lilishamtokea tena akiwa darasa la tatu ambapo pia alitumia njia hizi za asili kujitibu.


Baada ya kupona sasa, Marium anasema aliendelea na kazi yake ya ukahaba kwani haikuwa na jinsi yoyote ya kuiacha kutokana na kukosa elimu ambayo itamwezesha kupata ajira kitu ambacho aliona ukombozi wa maisha yake ni kujiuza tu (ukahaba).

Marium amejikuta akipata Matatizo ya kutosikia.
Kwa maelezo ya Marium amepata tatizo la kutosikia akiwa kwenye biashara ya kujiuza (Ukahaba). Sio rahisi kuamini lakini ndivyo ilivyo.

Anasema, Mama yake alikuwa hapendi (yeye Marium) ajihusishe kwenye vitendo vya ukahaba jambo ambalo alilipinga kwa kumpiga ili aachane na tabia hiyo.

“Mara nyingi mama alikuwa anawatuma watu wananishika halafu yeye (mama) ananipiga vibao vya masikioni na kwenye mashavu” Anaeleza Marium.

Kwa maelezo ya Marium anasema mama yake alikuwa anapendelea kumpiga sehemu hizo za masikioni na kwenye mashavu kutokana na sehemu hizo zinauma sana kuliko sehemu nyingine. Anasema mara nyingi akifanya makosa mama yake humtishia kwamba atampiga makofi ya masikio akijua makofi ya masikio yanauma.


Anaeleeza amepata mimba akiwa na miaka 13, anasema ilikuwa ni bahati mbaya kwake, alikuwa hapendi kuwa na mtoto katika umri huo kutokana na hakuwa na uwezo wa kuitunza mimba hiyo.
Pia, alihofia mama yake angemfukuza nyumbaani kutokana na hakupenda mwanae apate mimba akiwa bado na umri mdogo.

Baada ya kupata mimba ya kwanza, anasema mama yake alimchukia kiasi cha kumpiga na kumwambia akamtafute mwanaume aliyempa mimba jambo ambalo Marium anasema haikuwa rahisi kwenda kuishi na mwanaume huyo kutokana na mwanaume kumkana kwamba hakumpa mimba.


Kwa hiyo, kipigo kutoka kwa mama yake kiliendelea, ikafikia hatua akawa halali nyumbani kwa kuhofia kupigwa jambo ambalo anasema lilimfanya afanye ngono na wanaume tofauti tofauti ili apate sehemu ya kujisitiri.


Pia anaeleza kwamba, wanaume aliokuwa anatembea nao walikuwa wanampiga kwa madai ya kuwagonganisha na wanaume wengine (kutembea na wanaume zaidi ya mmoja). Anaeleza walikuwa wanampiga vibao vya masikio kitendo ambacho kilimwongezea kilema cha kutosikia.


Anaeleza, Kila mwanaume aliyekutana naye alikuwa akiwaeleza kwamba hana mwanaume jambo ambalo liliwafanya wanaume kuvutiwa naye kiasi cha kumweka ndani kama mke jambo ambalo Marium anasema haikuwa raisi kiasi hicho kwani hakuweza kuishi na mwanaume.


Anaelezea utofauti alionao na wanawake wengine wanaojiuza

Anakiri yuko tofauti na wanawake wengine wanaofanya biashaara ya ukahaba kutokana na kuwa na matatizo ya kutosikia. Lakini anasema hilo halimpi shida kutokana na kwamba umbo lake pamoja na uzuri alio nao unawavutia wanaume wengi wanaokuja kupata starehe hiyo ya ngono.

Anasema, kutokanaa na kuwavutia wanaaume anaweza kukusanya sh. 100,000 mpaka 150,000 kwa siku kama biasharaa imekuwa nzuri.


Aidha, anasema wanaume hawamshangai kwa kutosikia kwake, huwa anawaeleza wanaume anao kutana nao tatizo lake mapema kabla hawajaanza makubaliano ya hela pamoja na starehe nyingine.

Anaeleza kwamba tofauti hii ya kutosikia inamfanya afanye kazi ya ziada ambayo itamwezesha kuwavutia wanaume wengi.

Kazi ya ziada anayoisemea anatumia pesa nyingi katika kununua mavazi pamoja na vifaa vingine vya urembo kama pochi, simu nzuri za mkononi, hereni, cheni, pete, bangili, kubadili staili za nywele pamoja na matumizi mengine ambayo yatamfanya awavutie wanaume.


Anasema wanaume wengi wanavutiwa na urembo pamoja na mavazi, kwake yeye anaona mwanamke akivaa vizuri na kujiweka katika mwonekano mzuri basi mwanaume lazima avutiwe naye.


Uhusiano na mama yake mpaka sasa

Uhusiano wa Marium na mama yake si mzuri kutokana na kwamba kazi anayoifanya sio rasmi, kwa maana kwamba haikubaliki katika Jamii.

Kwa upande wa Marium anasema bado anampenda mama yake kutokana na kwamba ndiye aliye mlea mpaka walipokosana kwa sababu mama yake alishindwa kuvumilia tabia yake ya ukahaba.


Uhusiano na mama yake ulivunjika kabisa pale Marium alipopata mtoto wa pili ambapo ni mwaka mmoja baada ya kujifungua mtoto wa kwanza.


Anasema, pamoja na kutoelewana na mama yake, huwa anamtumia mama yake hela kila mwisho wa mwezi kwa njia ya huduma ya M- pesa kwa ajili ya matumizi.


“Nampenda sana mama yangu sitaki apate shida, japokuwa hataki nifanye kazi ya kujiuza lakini ndiyo inayoniweka mjini, hela ninazopata kidogo namtumia na yeye”


Matumaini ya Marium anasema ipo siku ataachana na kazi ya kujiuza. Anasemsa huwa anafikiria na kujiuliza kazi anayoifanya ya ujana lakini akifika uzeeni hajui atafanya nini kwa maana kazi hiyo haitaji mzee, mwisho ni miaka 35.


Aidha anasema anajuta kwanini amejiingiza kwenye ukahaba, anasema mama yake anatambua kazi ya kujiuza sio ya kudumu ndio maana alikuwa anampiga ili aachane na tabia hiyo. Anaeleza sio tu amaekosana na mama yake pia na ndugu zake wote wamtenga kutokana na tabia yake hiyo.


Anatoa wosia kwa wasichana ambao wana umri kama wa kwake kwamba waepuke makundi ambayo yatawasababishia kujiingiza kwenye biashara ya kujiuza, pia wapime ushauri wanaopewa kabla ya kuufanyia kazi. Kuna msemo unaosema akili za kupewa changanya na zako.
 
Back
Top Bottom