SoC02 Maana na viunga vya Utawala Bora

SoC02 Maana na viunga vya Utawala Bora

Stories of Change - 2022 Competition

lameckM

New Member
Joined
Oct 7, 2019
Posts
2
Reaction score
4
Maandiko na filosofia mbalimbali kutoka kwa wasomi na wanazuoni mbali mbali ni chachu kubwa ya elimu juu ya Utawala bora. Wasomi na wanazuoni wengi wameweza kuongelea na kutoa maana halisi ya Utawala bora na vitu vinavyopelekea kuwepo kwa utawala ulio bora na wenye kusadifu mahitaji ya watawaliwa kwa kuzingatia uwiano na uhusiano kati ya watawala na watawaliwa. Waandishi wengi na wanazuoni wameweza kutoa maana halisi ya Utawala bora, huku wengi wakieleza kuwa ni Utawala ambao unazingatia ukuu wa katiba, Utii wa Sheria na utekelezaji wa matakwa ya wananchi yenye tija kwa taifa zima. Nimekuchanganya?, Usijari utanielewa.

Utawala bora ni hali ya nchi au tawala zingine kuwa na uongozi au serikali ambayo inafanya kazi kwa kuzingatia matakwa na mamlaka yake kisheria, Uhuru wa mihimili ya nchi kwa maana ya Bunge, Serikali na Mahakama pamoja na kuzingatia kuwa Serikali inafanya kazi kwa kuzingatia na kuendeleza mamlaka ya Umma na si matakwa ya mtu au Kiongozi binafsi. Kwa maana nyingine Utawala bora ni hali ya kuwepo kwa utawala unaozingatia matakwa na matarajio ya watawaliwa kwa uwianisha na matakwa ya kisheria juu ya wajibu na mamlaka ya serikali ama uongozi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa ujumla ndani ya tawala husika. Sasa ni vitu gani vinathibitisha uwepo wa Utawala bora?

Waandishi wengi wa makala lukuki zihusuzo maswala ya utawala na sheria kwa kiasi kikubwa wameweza kupanua mawanda ya uelewa juu ya Utawala bora kwani kupitia maandiko yao mengi wameweza kujenga hoja juu ya viunga vya utawala bora ili kujibu swali ambalo pengine hata wewe msomaji unalo kichwani kwamba ni vitu gani huthibitisha uwepo wa Utawala Bora? . ukweli ni kwamba kutokana na maendeleo ya utawala wa sheria na sera kwa ujumla tumekuwa na miongozo mbalimbali ambayo ndiyo kipimo cha uwepo wa utawala bora katika nchi au tawala husika, miongozo hiyo ndiyo viunga halisi vya kuthibitisha uwepo wa utawala bora. Ili kuthibitisha uwepo wa utawala bora lazima tuthibitishe uwepo wa viunga hivi:

Uhuru katika utendaji kazi wa Mihimili mitatu ya nchi, ni miongoni mwa viunga ambavyo huthibitika kuonyesha uwepo wa Utawala bora. Mihimili mitatu ya nchi kwa maana ya Serikali, Bunge na Mahakama ni mihimili iliyowekwa kisheria na yenye kazi na wajibu tofauti katika nchi husika. Bunge likiwa kama mhimili mkuu wa nchi lina wajibu wa kutunga sera na sheria zenye manufaa kwa wananchi na serikali kwa ujumla, sheria hizi zitalenga kutoa muongozo wa mambo yote yahusuyo wananchi,serikali na maswala mengine yote yahusuyo nchi husika. Mahakama kama mhimili wa pili kazi yake kuu ni kutafasiri sheria na kufanya maamuzi huku serikali ikiwa na wajibu wa kuhakikisha sheria zinafatwa na pia kuratibu shughuli zote za maendeleo kwa nchi.

Ni dhahiri kwamba ili kuthibitisha uwepo wa Utawala bora ni lazima mihimili hii mitatu iweze kufanya majukumu yake kwa uhuru na weledi bila ya kuingiliwa na mamlaka yeyote kutoka nje au ndani ya mhimili husika. Uhuru wa Mihimili ya nchi iko katika namna mbili kwa maana ya Uhuru dhidi ya kuingiliwa na mamlaka za nje ya mhimili na Uhuru dhidi ya kuingiliwa na mamlaka za ndani ya mhimili. Aina ya kwanza ya Uhuru huu inamaanisha kwamba kusiwe na Kuingiliana katikamajukumu kati ya mihimili hii mitatu mfano, Bunge kuingilia majukumu ya mahakama au serikali kuingilia majukumu ya Bunge au mtu kutoka mhimili mmoja asifanye kazi katika mhimili mwingine mfano: Mbunge kuwa waziri, lakini ya pili maana yake ni kwamba ndani ya mhimili husika kusiwe na muingiliano wa mamlaka na utekelezaji wa majukumu. Tuendelee kidogo!

Utawala wa Sheria
, ni miongoni mwa viunga vinavyoweza kuthibitisha uwepo wa utawala bora katika nchi ama tawala husika. Utawala wa Sheria ni filosofia yenye kumaanisha kwamba hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria bila ya kujali cheo ama nafasi wala wasifu alionao. Filosofia hii inamaanisha katika shughuli za kiutawala au utekelezaji wa maswala ya kiuongozi basi kila mtu atatekeleza majukumu kutokana na matakwa ya kisheria bila kuvuka mipaka na uwezo aliopewa kisheria. Pia filsofia hii imelenga kudhibiti shughuli za kiutawala ziweze kufanywa kwa namna inayotakiwa kisheria lengo likiwa ni kuratibu mamlaka na kuwajibisha watawala wanaoishi juu ya sheria kwa kuvunja sheria na kufanya kazi nje ya mamlaka yao. Kiunga hiki ni chachu ya utawala bora kwani kimelenga kuratibu shughuli za utendaji kwa watawala ili kuzingatia matumizi bora ya mamlaka kama yalivyotolewa kisheria.

Mamlaka na nguvu ya Umma,ni kiunga kingine cha Utawala Bora, Katika filosofia ya utawala bora nguvu ya umma ni jambo la msingi sana kuzingatia ili kutambua kama kuna uwepo wa utawala bora katika nchi ama tawala husika. Mamlaka au nguvu ya umma ni hali ya serikali ambayo kimsingi inapokea mamlaka kutoka kwa wananchi kufanya wajibu wake ili kutimiza malengo na matakwa yenye manufaa kwa wananchi na nchi kwa ujumla. Kutokana na uelewa huu ili tuweze kuthibitisha kwamba kuna utawala bora ni lazima tuweze kuthibitisha kwamba serikali inatekeleza majukumu kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa na Umma lakini pia inawajibika kwa manufaa makubwa ya umma na sii vinginevyo.

Haki na Usawa, ni viunga muhimu vinavyoashiria utawala bora katika tawala au nchi husika. Haki kwa ujumla ama lugha rahisi ni stahiki ya mtu aliyonayo ama iliyo chini ya umiliki wake, lakini usawa ni hali ya uwepo wa uwiano mmoja bila ya kujali tofauti zilizopo zenye kuwatofautisha watu mfano jinsi au dini. Haki na Usawa ni vielelezo na viunga vya utawala unao hakisi maendeleo kwa wananchi na tawala husika kwa ujumla. Uongozi unao zingatia Haki na usawa katika uwajibikaji ni chachu ya kudumisha uhusiano kati ya serikali na wananchi jambo linalopelekea uwepo wa utawala bora, Utawala wa Umma.

Uwazi na Uwajibikaji pia ni miongoni mwa viunga ambavyo hutumika kuthibitisha uwepo wa utawala bora. Uwazi katika maswala ya utawala ni hali ya serikali kufanya kazi katika uhalali na uwazi kama itarajiwavyo na Umma wa nchi ama tawala husika bila ya kuficha taarifa muhimu zenye manufaa kwa umma. Uwajibikaji ni hali ya serikali au watawala kufanya kazi au utendaji wa majukumo yao kwa kiwango kinachokidhi matakwa ya jamii kama yalivyojengwa na sera ama sheria. Ni wazi kwamba uwajibikaji na uwazi ni chachu ya utawala bora na makini kwani huvutia imani ya umma kwa serikali.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom