SoC03 Mabadiliko ya katiba hayaepukiki

SoC03 Mabadiliko ya katiba hayaepukiki

Stories of Change - 2023 Competition

Missandei

Member
Joined
Apr 21, 2023
Posts
58
Reaction score
87


Habari zenu

Andiko hili linalenga kuwamasisha wananchi wenzangu juu ya umuhimu wa katiba mpya. Wale wote wenye mapenzi mema na nchi hii bila kujali itikadi zao za kisiasa, kidini au kikabila watakubaliana na mimi kuwa katiba mpya ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.

Kwa ufupi kabisa katiba ni sheria mama zinazoainisha namna nchi itakavyoongozwa. Katiba tunayotumia hapa nchini hivi sasa ni ile ya mwaka 1977.
Zifuatazo ni sababu kubwa zinazopelekea uhitaji wa katiba mpya ndani ya nchi yetu;

Haki ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka imenyang’anywa.

Uchaguzi wa mwaka 2020 ni kielelezo tosha juu ya hili ambapo matokeo ya uchaguzi ule yalishangaza wapiga kura na kuwafanya wajione kupoteza muda kwenda kupiga kura.
Hayo ni matokeo ya upungufu wa katiba yetu ambao umepelekea tume ya uchaguzi kushindwa kusimamia uchaguzi huru na wa haki. Wote tu mashahidi wa jambo hili kuwa tume yetu ya uchaguzi haipo huru na inaundwa na Raisi wa nchi hivyo tunahitaji katiba mpya itakayoweza kutupatia tume huru ya uchaguzi isiyopelekwa pelekwa na viongozi watakaokuwa madarakani lakini pia kumpunguzia Rais madaraka.

Sambamba na hilo tunaona kuwa katiba yetu ya sasa hairuhusu matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa na tume kupingwa mahakamani.
Katiba yetu ya sasa inasema hakuna mahakama yoyote yenye mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na tume ya uchaguzi. Yani wananchi tumenyang’anywa haki ya kuchagua viongozi wanaotufaa na pia hatuna pa kushtaki? Huzuni iliyoje.

Sisi wananchi tunahitaji katiba mpya ili tuweze kuihoji mahakamani tume ya uchaguzi kwa kushindwa kusimamia uchaguzi huru na wa haki.

Athari za uchaguzi usio wa haki ndiyo hizi tunaziona, matumizi mabaya ya kodi za wananchi, viongozi kutokuwajibika na kuwakilisha ajenda zao binafsi kwakuwa wanajua sio wananchi tuliowaweka kwenye nafasi hizo na pia hatuna uwezo wa kuwaondoa.

Tunahitaji katiba mpya ili sisi wananchi tuweze kuwashtaki viongozi tuliowapa dhamana kutuongoza kwa kukiuka misingi ya uongozi pamoja na kujihusisha na ufisadi. Tunahitaji kuweza kuwashtaki wabunge, mawaziri, na hata raisi kwa kutumia vibaya nafasi zao hili litaongeza uwajibikaji na kupunguza ufisadi katika nchi yetu.

Pia ingelikuwa afadhali kama vyama vinavyoshiriki chaguzi vingebanwa na katiba kubadili wagombea wao baada ya mgombea kushinda kwa vipindi viwili mfano kwa wagombea wa kiti cha ubunge, mbunge astaafu baada ya miaka 10 ya kutumikia nafasi ya ubunge na asiweze kuwa na vigezo vya kusimamishwa tena na chama chake kugombea nafasi hiyo bali awapishe wengine hususani vijana.
Tunaona vyama vikisimamisha mtu huyohuyo kugombea ubunge ilihali ameishakuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 10, je ni kuwa hakuna wengine wanaoweza kuongoza? Si kweli. Tunahitaji viongozi wenye maono mapya kuendana na mabadiliko ya jamii na siyo kuongozwa kwa mazoea na mtu mmoja kwa zaidi ya miongo miwili.

Hivyo Watanzania wenzangu ningependa jambo hili la mabadiliko ya kikatiba tulichukulie kwa uzito kama jambo la kitaifa na sio kama hivi sasa linavyochukuliwa miongoni mwa watanzania wengi kuwa ni jambo la kisiasa. Yoyote mwenye uzalendo na nchi hii bila kujali itikadi ya chama chake ataunga mkono harakati hizi na sisi wananchi ndiyo tunatakiwa tuwe vinara katika kufanikisha jambo hili kwa kupaza sauti zetu kwani viongozi waliopo madarakani hawawezi kulipigania kwakuwa katiba iliyopo inawafaidisha wao.
Ndugu watanzania amkeni usingizini, katiba tuliyonayo hapa nchini hivi sasa ni kama kichaka cha kuwalinda viongozi walio madarakani kuliko kuhakikisha viongozi hao wanasimamia maslahi ya wananchi wao na taifa pamoja na kafuata misingi ya uwajibikaji na utawala bora.

Hali kadhalika, ukiona mwenzako anapinga mabadiliko ya katiba basi jua kwa namna moja au nyingine katiba iliyopo inampa faida anazozijua, hivyo nawasihi watanzania tusiwe watu wa kufuata mkumbo bila kuchanganua mambo.

Vilevile tusiishie tu kuhimiza kutungwa kwa sheria na taratibu mpya ilihali katiba tuliyonayo inavunjwa bila hatua zozote kuchukuliwa. Katiba isiishie kuandikwa tu na kubaki vitabuni bali nchi iongozwe kupitia kwayo na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa katiba vinapotokea visifumbiwe macho hata kidogo. Mfano katiba yetu ya hivi sasa inataka mbunge kuvuliwa ubunge mara moja iwapo mbunge huyo ataacha kuwa mwanachama wa chama chake. Je wabunge 19 wasiotambuliwa na chama chao kule bungeni wanafanya nini?
Kama katiba iliyopo inavunjwa na hakuna anayewajibishwa ni wazi kuwa hata mchakato wa katiba mpya utakuwa hauna tija kama wananchi wengi wanavyodhani.
Kwenu viongozi husika tunahitaji hatua stahiki zichukuliwe kufuatia matendo ya uvunjifu sheria za nchi ili wananchi tusipoteze imani na serikali, na pia tuweze kushiriki kikamilifu kutimiza wajibu wetu na haki zetu za msingi kama vile kulipa kodi, kutoa maoni ya katiba mpya, kupiga kura nk.

 
Upvote 4
Back
Top Bottom