SoC02 Mabadiliko yaliyopo, yajayo; na kile tunachoweza kufanya

Stories of Change - 2022 Competition

the brain activator

New Member
Joined
Sep 2, 2022
Posts
2
Reaction score
1
Ukipitia taarifa mbalimbali za vyombo vya habari kama redio, runinga, magazeti na mitandao ya kijamii utakutana na maneno 'mabadiliko' au 'kawaida mpya', yawe yamesemwa moja kwa moja au kwa meneno mengine yenye maana karibu sawa nayo, ndio! Dunia inabadilika na itaendelea kubadilika; sisi Watanzania hatupaswi kujaribu kupuuza ukweli huu muhimu unaotukodolea macho au kuigiza kana kwamba hautuhusu kwa sababu kwa hakika unatuhusu kwa sababu nasi ni sehemu ya wakazi wa ulimwengu.

Mabadiliko si kitu kigeni, tangu mwanzo wa ulimwengu kumekuwepo na mabadiliko kadhaa yaliyochagizwa na sababu mbalimbali. Ya hivi karibuni ni mabadiliko kwenye mifumo ya ufanyaji kazi ya ulimwengu yaliyosababishwa na vita ya kwanza na ya pili ya dunia pamoja na Anguko Kuu la Kiuchumi.

Migogoro hii mitatu iliyotokea kati ya mwaka 1919 mpaka 1945 kwa pamoja ilibadilisha mifumo ya dunia ambayo ipo mpaka leo kuanzia kuundwa kwa taasisi za fedha, kijamii na hata kisiasa za kimataifa ili kujibu matokeo ya migogoro hiyo. Kwa maneno mengine migogoro hiyo iliisha zamani lakini matokeo yake yangalipo mpaka leo.

Sasa hivi tunashuhudia kipindi cha mageuzi kuelekea enzi mpya itakayomaanisha kukoma kwa kawaida za zamani na kuanza kwa kawaida mpya; mageuzi hayo kwa mara nyingine tena yanaletwa na migogoro! Pamoja na mingine ni mgogoro wa ugonjwa wa UVIKO 19, vita mbalimbali na mapinduzi ya kiteknolojia yanayochochea mgogoro wa ajira kati ya watu na vifaa vya kiteknolojia. Jambo moja ni hakika: migogoro hiyo itaisha lakini matokeo yake yatabaki nasi kwa muda mrefu ujao, ni matokeo hayo yanayopaswa kushugulisha zaidi akili zetu.

Katika chapisho hili tutaangazia mifano kadhaa juu ya namna migogoro ya ulimwengu inavyochochea mabadiliko na kile tunachoweza kufanya kuhusu mabadiliko hayo:

Mabadiliko ya kiuchumi: Wakati ugonjwa wa uviko19 ulipoingia ulimwenguni mwishoni mwa mwaka 2019, hatua kadhaa za kupambana nao zilichukuliwa kama vile kuzuia mikusanyiko ya watu, lakini pia raslimali fedha nyingi zilielekezwa kwenye mapambano dhidi ya Corona.

Matokeo ya hatua hizo ni mdororo wa kiuchumi uliosababisha mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa za msingi, kufilisika kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja hasa ambao shughuli zao za kiuchumi zinategemea mikusanyiko ya watu mfano biashara. Ikiwa jeraha hilo kwenye uchumi bado halijapona Vita nchini Ukraine imetokea na kuharibu zaidi uchumi.

Kwa sasa kuna kilio kote duniani juu ya mgogoro wa kiuchumi hasa tukijua kwamba huenda uchumi hautarejea hali yake ya kawaida, huku raia wakizilaumu serikali zao kuhusu hali ngumu za maisha, serikali zinabebesha mzigo wa lawama migogoro tajwa. Lakini malalamiko na lawama haziwezi kuwa suluhu, suluhu ni kuelewa ujumbe ambao mgogoro huu unatuletea: ujumbe kwamba uchumi huu tulionao itafika wakati utashindwa kuhimili athari za migogoro hivyo utabadilika kutoka huu wa analojia kwenda wa kidijitali, mathalani tuliona namna biashara za mitandaoni zilivyokua kwa kasi wakati wa janga la Corona huku sarafu za kidijitali zikikua na kupata umaarufu mkubwa; ndiko uchumi unahamia.

Watu wetu lazima wafundishwe namna ya kushiriki kwenye uchumi wa kidijitali ili wasije wakaachwa nyuma. Ni muhimu kukumbuka kwamba mwishoni mwa migogoro hii ya kiuchumi kutakuwa na makundi mawili: washindi na washindwa, hatupaswi kuchagua kuwa washindwa.

Mabadiliko ya kielimu: mnamo wakati ambapo miito inazidi kuongezeka ikitaka mifumo ya utoaji elimu ibadilishwe kwa kutokidhi mahitaji ya wakati huu na ule ujao, madhara ya mifumo ya elimu hii iliyopitwa na wakati yanazidi kuonekana waziwazi. Watanzania tumeachwa nyuma kwa karibu kila jambo hii ni kwa sababu ni ngumu sana kuishi maisha ya kileo kwa kutumia mifumo ya kizamani. Tumekuwa tukishindwa kwenye usaili na wenzetu wa nchi nyingine, ni kwa sababu wao wanaenda na wakati huku sisi tuking'ang'ania mifumo chakavu ambayo haina majawabu kwa maswali ya kizazi hiki.

Tunatumia kigezo cha kukariri kupima akili za watoto wetu mashuleni ili kutengeneza kizazi cha wakaririshaji wa baadae huku tukifubaza uwezo wao wa kufikiri na kupuuzilia mbali stadi muhimu za maisha ambazo zingeweza kuwasaidia kujiajiri. Matokeo ya mifumo hii mibovu ni kutengeneza wasomi feki wanaotafuta majawabu kwa matatizo yao binafsi badala ya wao kuwa majawabu kwa matatizo ya jamii na taifa.

Vijana wetu wengi wamejiajiri kwenye biashara za mitandaoni siku hizi lakini kukosa elimu sahihi juu ya uchumi wa kidijitali kumewafanya wawe wahanga wa matapeli na uwekezaji usio na tija, wakati huohuo janga la ukosefu wa ajira linazidi kuelekea kiwango cha hatari; janga hili ni bomu linalosubiri kulipuka! Hatuwezi na hatupaswi kusubiri lilipuke, ni wakati wa kubadilisha mifumo ya elimu ili kutengeneza kizazi cha watu wenye fikra chanya zenye kutoa majibu kwa maswali ya jamii ambayo haikupata fursa ya kwenda shule na kufikia kiwango cha maendeleo tunachotaka.

Mabadiliko ya kiteknolojia: vitu vitatu; cha kwanza, mabadiliko kwenye sekta ya teknolojia yanapokuja yanatupa machaguo mawili, ama tuwe sehemu ya teknolojia au tuwe watumwa wa teknolojia. Katika dunia ambapo teknolojia inaendesha karibu kila nyanja ya maisha ni muhimu sana tuandae kizazi cha Watanzania watakaokuwa sehemu ya teknolojia.

Cha pili, mabadiliko ya teknolojia yanakuja na pande mbili, kuua/kupunguza ajira za zamani na kutengeneza ajira mpya. Kwamba watanzania watapoteza ajira zao za zamani au watapata ajira mpya itategemea na maandalizi wanayofanya sasa hivi, mfano inakadiriwa teknolojia itapunguza kwa asilimia 50 ajira zilizopo kufikia mwaka 2025, kufikia mwaka huohuo pia maelfu ya ajira yatakuwa yamezalishwa kufuatia mapinduzi kwenye teknolojia kama zile za maroboti na akili bandia(artificial intelligence) na masoko mtandao (online marketing).

Ni wakati wa watanzania kuchagua upande wanaotaka kuwa ili wasije kuachwa nyuma. Cha tatu, kukua au kufa kwa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kutategemea ni kwa kiasi gani teknolojia imekaribishwa kwenye sekta hizo.

Mfano mdogo ni sekta ya kilimo, dunia inapambana na majanga mawili: njaa na mabadiliko ya hali ya hewa, kupitia matumizi ya teknolojia za hali ya juu (advanced technologies) wakulima wa kitanzania wanaweza kuboresha kiwango na ubora wa mazao yao(katikati ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi) ili yaweze kumudu ushindani kwenye soko la kimataifa wakati huohuo majukwaa ya teknolojia yatawawezesha wakulima wetu kukutana na wanunuzi wa mazao bila kuhitaji watu wengine katikati (middle men) ambao wamekuwa wakiwaibia wakulima na kuwasababishia hasara.

Wakifanya hivyo wakulima watapata faida inayoendana na uwekezaji waliofanya hivyo moja kwa moja sekta ya kilimo itakua. Vitu hivi vitatu vitusukume Watanzania kama mtu mmoja mmoja na kama taifa tuwekeze zaidi kwenye teknolojia ili kuendana na mabadiliko yaliyopo na yajayo.

Nipende kuhitimisha kwa kusema: dawa ya mashaka ni maarifa; katikati ya misukosuko inayotokea kwenye kipindi hiki cha mageuzi yatakayotupeleka kwenye mifumo mipya ulimwenguni, mashaka yamekuwa mengi sana miongoni mwa watu.

Ukiwasikiliza watanzania utaona wengi wana mashaka kuhusu kesho yao, kesho ya biashara/kampuni zao,kesho ya elimu za watoto wao na kadhalika. Ni kwa sababu maisha katika kipindi hiki cha mpito (transition period) ni kama vile maisha hayatabiriki, lakini mashaka HAYAWEZI kusuluhisha misukosuko tuliyonayo bali maarifa yanaweza!

Mashaka yetu yatusukume kuchukua hatua ya kutafuta maarifa juu ya ujumbe ambao misukosuko hii imetuletea, ni ujumbe wa mabadiliko! Kadri tutakavyo tafuta maarifa ndivyo tutazidi kugundua kwamba hakuna kitu cha kutia mashaka, kuna kitu cha kukielewa; kuelewa kwamba tumepewa fursa ya kuchagua tuwe sehemu ya kesho au la.

Uchaguzi huo utatokana na maamuzi na maandalizi tunayofanya leo, huwezi kuwa sehemu ya kesho ambayo hujajiandaa kwayo! Mtu mmoja alisema haikuwa ikinyesha wakati Nuhu alipojenga Safina, na mimi niseme bado haijaanza kunyesha, bado wakati tunao wa kufanya maandalizi na maamuzi yenye lengo la kuhakikisha tunafika tunakotaka na kesho ya taifa letu iwe bora kuliko jana. Naomba kuwasilisha.

Email: doctordanny71@gmail.com
WhatsApp:+255 784 998 625
 
Upvote 1
Mimi naitwa Lumola Nimekupigia Kura Naomba na Mimi unipigie Kura kupitia SoC 2022 - Tufuge nyuki kwa maendeleo endelevu na tuwalinde kwa wivu mkubwa
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…