Wastaafu wa EAC wavamia Ikulu - Tanzania daima
na Nasra Abdallah
WASTAAFU wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameapa kulala katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam, hadi watakapopewa majibu sahihi ya lini watapewa fedha zao.
Wazee hao zaidi ya 30 walifikia uamuzi huo jana baada ya kusubiri zaidi ya saa nane majibu ya uhakika ya lini watalipwa fedha hizo nje ya geti la Ikulu bila mafanikio.
Msemaji wa wazee hao, Nathanel Mlaki, aliyeruhusiwa kuingia ndani ya ofisi za Ikulu kwa niaba ya wenzake na kukaa huko zaidi ya saa nane, aliwaambia wazee hao kuwa Ikulu imewaomba wapewe nafasi ya kuzungumza na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ili awape majibu ya uhakika ya lini wanaweza kupata fedha zao.
Suala la sisi eti kwenda halafu turudi kuja kusikia atakachosema Luhanjo haliingii akilini
tunachoona ni bora tulale hapa kama ni kutukuta, atukute kwenye viwanja hivi ili aone tunavyoteseka. Na hata asipotokea kesho (leo), bado tutaendelea kulala hapa, alisema Mohamed Matumbwa, mmoja wa wastaafu hao.
Hata hivyo, wazee hao waliliomba Jeshi la Polisi kuwapa ulinzi kwa kipindi chote watakachokuwa hapo. Walidai kuwa nia yao si kufanya fujo, bali kufuatilia haki zao.
Mmoja wa wastaafu hao, Nelson Bilali, alisema wako tayari kufia kwenye ardhi hiyo ya Ikulu wakidai kuwa wamechoka kudhalilishwa kwa kufuatilia mafao kwa zaidi ya miaka 30 bila ya mafanikio.
Mei, mwaka huu, wazee hao waliandamana hadi viwanja hivyo, lakini walipozwa na mmoja wa wasaidizi wa Ikulu kwa walipoambiwa kuwa msaidizi huyo atafanya jitihada ndani ya wiki moja, kuhakikisha anawakutanisha na Lihanjo pamoja na kundi la wataalamu ili kupitia upya madai yao ya sh. bilioni 450.
Hata hivyo, walisisitiza kwamba hawana mpango wa kurudi mahakamani, kwani walishashinda kesi hiyo nje na ndiyo maana walianza kulipwa fedha zao kipindi cha uongozi wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa. Waliambiwa kuwa mafao hayo yanalipwa kwa awamu.
Habari zilizopatikana baadaye jana usiku, zilisema kuwa wazee hao walitawanyika baada ya polisi kuwataka wafanye hivyo.
Maoni ya Wasomaji
Maoni yanayotolewa na wasomaji wa safu hii ni ya kwao na sio maoni ya kampuni ya Freemedia Ltd. Aidha sio maoni ya mtunzi au mwandishi wa habari au makala husika hapo juu. Maoni haya hayajahakikiwa wala kuafikiwa na kampuni ya Freemedia Ltd.
Maoni 4 yameshatolewa. (Nawe toa maoni yako!)
Lipeni hawa Wazee wacheni mambo ya ubabaishaji. Kama hamuwezi kuwalipa watu mishahara yao hizi jumuiya mnazianzisha za kazi gani?. Mimi nafikiri umefika wakati sasa Serekali ifungashe virago iende likizo. Kama mnaanza kutapekli watu hata mishahara yao kodi mnakusanya za nini ndugu zangu. Kwanza hiyo ni pesa kidogo sana ukilinganisha na fedha ambazo wawekezaji wanazihamisha kila kukicha. Chonde chonde walipeni Wazee wa watu fedha zao wakajipumzishe.Kama Serekali haina fedha chukueni kwa MAFISADI.
na OLE LETIPIPI, TANZANIA, - 15.07.08 @ 08:12 | #21675
MIMI NI MMOJA WA WADAI NA HALI HALISI KWA KIFUPI NI KAMA IFUATAVYO:-
BAADA YA KUVUNJIKA KWA EAC, MWAKA 1977, CROWN AGENCY,ALIYEKUWA LIQUIDATOR, ALIGAWA MAFAO KWA WALIYOKUWA WAFANYAKAZI WA NCHI YA KENYA, UGANDA NA TANZANIA. FEDHA HIZO ZILIKUWA ZA KIGENI NA ZILIAMBATANA NA MASHARITI KUWA SEREKALI HUSIKA ITAWALIPA WAFANYAKAZI HAO KWA THAMANI HALISI NA COMPOUND INTEREST YA 7%. KENYA NA UGANDA WAKALIPWA KAMA ILIVYO AGIZWA. SERIKALI YA TANZANIA IKAZIWEKA HELA HIZO ZA KIGENI BOT NA IKAJISAHAU MPAKA 2004 WAKATI RAIS MSTAAFU MHE. MKAPA ALIPOKIRI KUWA HELA HIZO ATAZILIPA HATA KAMA NI KWA AWAMU. WAZIRI WA FEDHA WAKATI HUO,MHE. MRAMBA ALIOMBA BUNGENI BL.50 ILI ANZE KULIPA NA BUNGE LIKAIDHINISHA. ALIVYOMALIZA VIKAO VYA BUNGE TU, WAZIRI AKAJIONGEZEA BL.67 NA KUFANYA JUMLA YA BL117. ILI KUTUSHAWISHI NA TUSAHAU ILE JUMLA YA BL.450 ZILIZOAHIDIWA NA MHE.RAIS. TATIZO LETU LEO NI THAMANI YA FEDHA NA FAIDA YA 7% KATIKA MIAKA 30. ALICHOTAKIWA MHE.MRAMBA AFANYE NI KUGEUZA HELA ZILIZOTAKIWA KULIPWA 1977 KWA EXCHANGE RATE YA $ WAKATI HUO,NA KUKOTOA MAHESABU KUTUMIA DOLLAR HIZO KUANZIA 1977 HADI 2008. BAADA YA HAPO NDIYO ABADILISHE KWA TZS
na rR.B. BWANGA, MOSHI/TANZANIA, - 15.07.08 @ 08:39 | #21683
Kwa usanii wa serikali ya Tanzania, wazee wetu hawa wataanza tena kulipwa pesa zao mwaka 2009-10 wakati uchaguzi unakaribia kama walivyozugwa 2004-05 ili waipigie tena kura CCM!
Serikali inazo pesa nyingi sana ndio maana wanaingia mikataba mibovu ili waweze kuzihamisha kupitia hayo makampuni ya kifisadi. Kutokuwalipa hawa wazee ni unyanyasaji tu wa serikali kwa hao wazee hakuna issue nyingine.
na Msugu Pe-igwite, Iringa, Tanzania, - 15.07.08 @ 10:52 | #21723
Kitendo cha kuwaletea wastaafu hao polisi ni cha udhalilishaji kwani wasingekaa hapo kama serikali ingekuwa imewalipa pesa yao.Kwanini serikali ya Tanzania imekaa kisanii kiasi hicho jamani?Wastaafu hao wanadai haki yao na siyo msaada!Kwa kweli kwa hali hiyo sioni kama itakuwa fair kwa watanzania kuipa kura tena ccm ktk uchaguzi kunaokuja kwani serikali yake inafanya kazi zake kwa kubahatisha na kiujanja ujanja tu.Wote walioko kwenye system wanaishi vizuri wakati idadi kubwa ya wananchi wenye kipato cha chini wanaishi kwa taabu.Mfano mkubwa ni hawa wazee wanahangaishwa kwa pesa ambazo ni halali yao kabisa!Mmm,Tanzania kweli ni kiboko.
Ninaipenda sana nchi yangu but kila nikifikiria maudhi na manyanyaso ya huko naona ni bora niendelee kuishi huku ugenini.Inaniuma kuona ninachangia pato la nchi ambayo si yangu lakini ni heri nifanye hivyo kwani ninafaidika na kodi ninayolipa hapa kwani nina uhakika wa huduma zote muhimu kuliko nilivyokuwa ninachangia hapo nyumbani kila kitu shida kuanzia matibabu,miundo mbinu n.k.
Wito wangu kwa serikali tafadhali,tafadhali sana walipeni hao wazee wote.Walio hai muwalipe wenyewe na waliotangulia mbele ya haki nina uhakika kuwa wameacha warithi wao hivyo wana haki ya kulipwa.Bila hivyo sidhani kama kutakuwa na Tanzania yenye neema kama inavyosemwa na kiongozi wetu wa nchi bali ni Tanzania ya shida na machungu tele.
na seven abraham, Copenhagen,Denmark, - 15.07.08 @ 14:05 | #21810
Yeyote anaeipa serikali yetu ya CCM sifa yoyote ile amefunikwa na wingu la giza lisilo mfano wake. Ni serikali ya ghilba, uwongo na uzandiki ukiongozwa na viongozi wezi na wanafiki. Damu ya Wahanga hawa siku zote itakuwa juu ya wale wote waliokuwa serikalini toka awamu ya Mwinyi, Mkapa na Kikwete.