SoC04 Maboresho kwenye Sekta ya Utalii ili kuendana na Ongezeko la Watalii nchini

SoC04 Maboresho kwenye Sekta ya Utalii ili kuendana na Ongezeko la Watalii nchini

Tanzania Tuitakayo competition threads

Frajoo

Member
Joined
May 28, 2024
Posts
12
Reaction score
3
Dibaji.

Sekta ya utalii ni sekta inayoongoza kwa kuingiza mapato nchini kwa miaka mingi sasa,na ni moja ya Sekta zinazokua kwa kasi.Kutokana na utajiri wa vivutio vya utalii tulivyonavyo nchini inakadiriwa takribani watalii Milioni 1.4 kwa mwaka huja Tanzania,kwa mujibu wa tafiti.

Aidha Rais wetu Samia Suluhu Hassan ,amekuwa akiitazama Sekta hii kwa jicho yakinifu ndio maana leo sote tunamsifu kwa juhudi za makusudi alizozionesha kwa kuvitangaza vivutio vyetu na kuunyanyua utalii kupitia filamu ya Royal tour pia kwa kuboresha uongozi ili kusimamia vyema hifadhi na kuratibu kazi za utalii kwa weledi ili kukidhi matakwa ya watalii pasi na kuleta madhara kwa taifa,bali faida kizazi hadi kizazi.

Utangulizi.

Matunda ya hamasa zinazofanywa na Serikali yetu sikivu hakika yanaonekana hasa tukizingatia Sekta ilidorora kutokana na athari za Ugonjwa wa Covid-19 ulioisumbua dunia.Sasa sote tunakubaliana nchi imefunguka ,utalii umefunguka!Ni matarajio ya wengi kwamba msimu wa kupokea watalii wengi (High season) kwa mwaka huu idadi ya watalii itavuka Milioni 1.4 .

Na nina imani miaka 25 ijayo Tanzania itakuwa moja ya nchi zenye mafanikio makubwa kwenye kiwanda cha utalii .Na vivutio vyetu maarufu zaidi kama Ngorongoro Crater,Serengeti na Mlima Kilimanjaro zinaweza zikawekwa kwenye ngazi za juu za Vivutio pendwa zaidi duniani,lakini kama tukijipanga vizuri.

Yapo maeneo ambayo kimsingi nadhani yanahitaji kuboreshwa ili kuiimarisha Sekta hii ,izidi kututangaza vyema na kutuingizia fedha za kigeni na kuongeza Pato la taifa maradufu. Napenda niorodheshe eneo moja baada ya lingine na maoni yangu ambayo natamani kuona yanachukuliwa hatua.

1. Kuliongezea thamani zao la Utalii wa kitamaduni.(Cultural Tourism.)

Utalii wa kitamaduni ulianzishwa rasmi mwaka 1996 chini ya usimamizi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ikiwa na lengo la kuruhusu Watalii kuchangamana na Wazawa kwenye Vijiji vya Tanzania ,ili wajifunze maisha halisi ya Watanzania,yaani kusikiliza hadithi zetu zenye historia za mashujaa na makabila mbalimbali yenye tamaduni tofauti,hasa tukizingatia Tanzania tuna zaidi ya makabila 120 na kila kabila lina lugha yake na utamaduni wake.Utalii huu ulipata muitikio mkubwa kwa Watalii kwakuwa iliwafurahisha wanaporudi nchini kwao wakibeba zawadi walizonunua kwa wajasiriamali wakitamaduni (Souvenirs)

Ukanda wa kaskazini mwa Tanzania walikuwa wakwanza kuchangamkia fursa ya kuanzisha Makampuni madogo ya utalii wa kitamaduni, baadae wakaunda umoja wao yaani TACTO (Tanzania Association of Cultural Tourism Organizers) lengo ni kuimarisha zao hili na kujadili mustakabari wa sekta ya utalii kwa ujumla ili Utalii wa kitamaduni uimarike zaidi.

Maoni mengi ya Wadau yametolewa kwenye vikao vya wadau pamoja na wenye dhamana Wizarani.Serikali iliona manufaa ya zao hili, na mwaka 2017 ilianza rasmi mpango wa kupeleka Utalii huu Nyanda za juu kusini ili wananchi wa huko nao wawekeze kwenye zao hili.Kigezo ni kwamba kunafikika,kwa maana zipo hifadhi nyingi ukanda ule,hivyo ni rahisi kupata wateja ambao watakwenda kutalii.

Kwa upeo wa kawaida tu unaweza kugundua Utalii huu unategemea hifadhi au utalii wa Wanyama pori,misitu,maziwa na Milima.Hii inamaana bado Sekta haijafaulu kushawishi watalii wakaja mahususi kwaajili ya Utalii wa kitamaduni.

Tunahitaji matangazo zaidi kama ilivyo kwa kila biashara.(Promotions) na hili ni jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii.Ili kuwasaidia hawa TACTO mwishowe hizo Cultural enterprises zipate wageni wa moja kwa moja pasi na kutegemea Makampuni yanayopeleka wageni porini,kuwapelekea wageni kama wakiwa na muda wa ziada.

Kivipi? …Nadhani Bodi ya utalii Tanzania ifungue matawi kwenye Mataifa potential zaidi ,kwa ushirikiano na Balozi husika.Hivyo vituo viwe kama kijiji cha Makumbusho pale Dar na kila baada ya muda fulani kunakua na matukio (Events) ambapo kunakuwa na Maonesho ya ngoma za asili,documentaries zakitamaduni,picha zilizochorwa na wasanii wetu zinazosadifu mazingira na maisha halisi ya Watanzania na vyakula vya asili.

Hii italeta hamasa kwa watalii kutamani kuja kushuhudia mubashara kuhusu maisha halisi ya Watanzania.

Aidha, kuna nyongeza ya mawazo kwenye Utalii wa kitamaduni, kama;

(a) Kuongeza baadhi ya Vivutio: kama ziara za kwenda Mirerani kupata uzoefu wa uchimbaji madini na utayarishaji mzima.
(b.) Kujenga Museum kubwa kwenye jiji la utalii (Arusha)

Mkoani Arusha Museum ipo lakini hii nayotaka kuona inajengwa ni kubwa zaidi ambayo haitakuwa tu ikiwekwa vinyago ,vitabuna picha pekee,bali yenye eneo kubwa ambalo kutakuwa na migahawa ya vyakula vya asili, Ngoma za asili zikitumbiza,pamoja na kuhusika katika Maonesho yote ya utalii kama Karibu-Kilifair,Site na mengineyo.

(c.) Kuongeza maudhui ya Utamaduni kwenye muendelezo wa Filamu za utalii.

Kwenye filamu ya Royal tour nimeona Maudhui ya Utamaduni hayajasisitizwa kama ilivyo kwa hifadhi zetu,hivyo nadhani kuna haja ya kukoleza wino kwenye eneo hili,ili kutangaza zaidi aina hii ya utalii.Ikibidi kuwe na filamu ya Utalii wa kitamaduni kabisa ili kuleta msisitizo.

2. Wadau wa utalii wateuliwe TANAPA na kwenye Bodi ya Utalii Tanzania.

Natambua Bodi ya Utalii ina wakereketwa wa masuala ya utalii lakini huchukua muda mrefu hadi kuielewa vizuri sekta ilivyo kwa Mapana yake.Wakati huo wapo wadau wa utalii wengi wao wakiwa ni wamiliki wa makampuni na mahoteli yakitalii.Watu hawa wana uzoefu sana ,wana mashauri mengi jengefu kwenye Sekta.

Watu kama Willbard Changulo(Mwenyekiti wa TATO.), Zainabu (Mkurugenzi wa Zara tours.) na wengine wengi sana.Japo ni wamiliki wa makampuni lakini zipo faida nyingi za kuwa na watu kama hawa kwenye Serikali hakika kuna maboresho mengi yatafanyika kuliko faida binafsi.

3. Uwekezaji kwenye utalii uzingatie Uhifadhi wa mazingira,utamaduni wa wazawa wa maeneo husika, na elimu kuhusu utalii kwa wenyeji.

Kwenye Sekta ya utalii swala la uwekezaji ni endelevu na lenye tija kwenye maendeleo katika sekta.Moja ya uwekezaji unaofanyika mara kwa mara ni ujenzi wa mahoteli yakitalii na Campsites kwenye maeneo yaliyo mbali na miji,ambako kiuhalisia ni jamii za wafugaji na wawindaji.

Sababu ni ya msingi kwakuwa ni mazingira yenye uoto wa asili ambayo ni moja ya vivutio vya utalii,pia ni jirani na hifadhi za Taifa.

Changamoto; Katika ujenzi kuna ufyekaji wa mapori ili kupata maeneo ya kujenga hoteli,lakini pia Wazawa hulazimika kuwekewa mipaka au kuhamishwa kabisa kwenye mazingira yao ,ambako ndio chimbuko lao.

Athari ; Kupotea kwa historia na Utamaduni wa Wazawa.Kila jamii ina historia yake ambayo hutunzwa kupitia mazingira,mitindo ya maisha ambayo ndio hukamilisha Utamaduni wa jamii.Mfano Utamaduni kuandaa dawa na tiba asili uhusisha mazingira asili na aina ya maisha ,hasa kwa jamii zilizo mbali na miji.Hivyo wanapohamishwa na kupelekwa mazingira mapya ,moja kwa moja wanapoteza taratibu zao.

Hata kama watahamia mazingira yenye huduma bora za kijamii lakini asili jadi zao ni muhimu kuzienzi.Mathalani mitishamba ambayo ni ya asili kiuhalisia ni vigumu kuiotesha kwenye ardhi tofauti.Na Utamaduni tumeona ni zao la thamani la utalii .

Cha kufanya; Watunga Sera waainishe kwamba Utamaduni wa jamii husika ni moja ya vivutio vya utalii.Wapo watalii wanatamani kujua jamii hizo zinaishi vipi maeneo hayo ambayo kimtazamo ni maeneo hatari yaliyo mbali na huduma nyingi zakijamii.

Pia kuwahusisha Wazawa hao katika uwekezaji ili watoe maelekezo ni mazingira yapi hasa wanapaswa kuwekeza ili kuepuka kuingilia mila na desturi za jamii hizo.

Aidha ,inaleta maana kama miradi ikawanufaisha wanajamii waliokutwa kwenye maeneo hayo ya uwekezaji.Kwa maana ya kuwaajiri ,kiwapa fursa za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kuwajengea iwezo na kutoa fursa za masoko ya uhakika kupitia mradi husika.Na sio kuwaondoa kama kikwazo .

Kuhusu huduma za kijamii ,zipo ambazo Serikali kupitia Sekta ya utalii inauwezo wa kuwahudumia, kwa maana ya kuwasogezea.Lakini tu ,itaposisitizwa kwamba maisha yao ni kivutio cha utalii na wao ndio dira ya uwekezaji kama mtazamo wa ushirikishwaji utazingatiwa.

4. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ikodishe Maeneo yenye Maziwa,Misitu na Maporomoko ya maji ili kuboresha uwekezaji.

Kiuhalisia Wizara na hifadhi haziwezi kuwekeza kila eneo kwa viwango vya kimataifa ili kuvutia Watalii.Hio ndio sababu kubwa nadhani ni bora kukaribisha Wawekezaji waweze kuwekeza kwa ubora unaoendana na zama hizi.Kwa mfano kuna maziwa kama Ziwa Duluti lililopo Arusha ,wamejitahidi kujenga ofisi nzuri za hifadhi na wamekaribisha muwekezaji anatoa huduma ya mgahawa ni kitu kizuri lakini isingeishia hapo.

Kuna maeneo mengi yalipaswa kuboreshwa hata ile Mitumbwi ambayo Mamlaka wanakodisha zilipaswa kuwa zenye kuvutia zaidi mfano kuletwa kwa boti za kisasa zenye nafasi ya kuweka vyakula na vinywaji ili kuvutia hata utalii wa ndani.

Kuweka BBQ za nyama pori kila mwisho wa wiki.Hayo yote yanaweza kufanyika na wawekezaji kama watatangaziwa kuna nafasi ya kuwekeza mwenye wazo bora anakodishwa afanye maboresho.Kuna rafiki yangu aliniambia ingekua kwa nchi zilizoendelea hata Nguva wawili wangekuepo ili hata kiingilio chake kingekuwa bei yenye maslahi.

Hivyohivyo kwenye maporomoko ya maji kama ya misitu ya Mlima Meru kulipaswa kuwekezwa vizuri ili kuvutia watalii zaidi.Huduma za Zipline Adventure na mambo kadha wa kadha yenye kuleta ladha kwenye utalii.

5. Usafi uzingatiwe sana kwenye Miji yakitalii.

Kuna kipindi Moshi iliongoza kupata watalii wa ndani bila wadau wa utalii kustuka,kwasababu ya habari njema zilizoenea nchini kwamba Moshi ni mji msafi sana.Kwa tafsiri hio usafi ni kivutio cha kwanza ambacho watu huzungumzia kabla ya yote wanapotembelea sehemu fulani.

Hivyo kwa miji yote yakitalii inapaswa kuwa na usafi kuzidi maeneo mengine kwavile ndio hutoa taswira ya nchi,husema kilakitu kuhusu Watanzania.Licha ya hivyo huvutia biashara zingine kama za vyakula na malazi .

Kilichonisukuma ni hali halisi ya jiji la Arusha hasa maeneo ya katikati ya jiji, ukipita kwenye masoko ya vyakula kama Kilombero na Mjini kati hakika ni aibu kwenda na Mtalii kufanya utalii wa jiji.Mazingira ni machafu,yaani matunda na vyakula vilivyooza hutupwa hovyo,hakuna utaratibu mzuri wa kufanya usafi.

Huduma za maji hakuna na uchafu ukikusanywa bado gari la taka huchelewa kuchukua.Zaidi mpangilio wa wafanyabiashara ni mbaya kuna msongamqno na upangaji holela wa vyakula /bidhaa.Nadhani haipaswi kuwa vile kama mji wa kitalii.

6. Maduka ya kubadilisha fedha yarudishwe kama zamani.(Bureau exchange.)

Sina uhakika sana na sababu za kufunga maduka ya kubadilishia fedha ,ambayo yalikuwa kila mahali kwenye miji ya kitalii.Hakika yalirahisisha maisha ya watalii na waongoza utalii ,kwakuwa huduma zilitolewa wakati wote ,hata kama Watalii wamefika usiku aidha kutoka nchini kwao au porini hawakuwa na hofu juu ya kubadili fedha .

Lakini sasa imekuwa changamoto hadi kwa wamiliki wa makampuni ,inawapasa wawahi muda wa mabenki ,baada ya hapo kuna maeneo machache sana yakutoa huduma hio baada ya muda wa kazi wa kiserikali.Hili litazamwe kwa jicho pevu kama tunatazamia kupokea watalii wengi siku za mbeleni.

7. Wabeba mizigo na Waongoza watalii wa Kilimanjaro waongezewe mapato na kupewa Bima za afya.

Kiukweli hawa vijana wanafanya kazi ngumu,fikiria kupanda mlima mrefu zaidi Afrika jumlisha kubeba mzigo mzito mgongoni.Lakini ujira wao ni mdogo na hawana Bima ya afya.Miaka ya nyuma makampuni yaliyomilikiwa na Wazungu angalau walikuwa wanawajali watu hawa,lakini baada ya kuwapiga vita waliacha kuwekeza.

Hali ni mbaya sasa ni aibu kwa wawekezaji wazawa wasiojali Watanzania wenzao wanaofanya kazi ngumu.Kuna wakati Watalii hupenda kujua malipo yao na wao ni binadamu hawawezi kudanganya ilhali wanaumia,hivyo ni aibu kwa sekta na ni ishara ya kudumaa katika huduma.

Hitimisho.

Haya ni baadhi ya maboresho ambayo natamani kuona yanafanyika kwa miaka hii ya karibuni ili mpaka kufikia miaka 25 Tanzania tuwe mbali katika sekta ya utalii ambayo huchochea sekta nyingine kukua pia.Sekta moja huitegemea nyingine katika safari ya maendeleo.Mfano kwenye huduma za kijamii tumekuwa tukipokea wageni wanaojitolea (Volunteers) kutoka nchi zilizoendelea.Watu hawa hawapaswi kutozwa pesa kwaajili ya kujitolea kama hali ilivyo sasa,kwanza wanaisaidia jamii na serikali pia.

Lakini pia baada ya muda wao kuisha maranyingi hutembelea kwenye vivutio vyetu vya utalii.Wengi huhairisha kuja kwakuwa wanajumlisha na gharama za kuishi maisha ya kujitolea hasa kulipa kama ni hospitali hivyo kwa namna nyingine tunaikosesha sekta ya utalii.Watu hawa pengine hata malazi wangepata kwa gharama nafuu zaidi ili mwishoni watalii kwa uhuru kwakuwa wengi wao bado ni wanachuo.

Asante kwa muda wako;

Nawasilisha.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom