Mabwepande: Raia wacharuka baada ya nyumba zao kubomolewa

Mabwepande: Raia wacharuka baada ya nyumba zao kubomolewa

Suley2019

JF-Expert Member
Joined
Oct 7, 2019
Posts
2,203
Reaction score
5,610
NYUMBA zaidi 11 katika mitaa ya Mabwepande na Mjimpya Kata ya Mabwepande Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam zimebomolewa na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha, huku wamiliki na familia zao wakilalala nje kwa siku mbili.

Ijumaa saa 10:00 jioni, waliotekeleza ubomoaji huo baada ya kupata maelekezo kutoka kwa viongozi wa Idara ya Mipango Miji Halmashauri Manispaa ya Kinondoni, walikuwa wamevaa kininja (maski) kuficha nyuso zao.

Diwani wa Mabwepande, Mhajilina Kassim maarufu kama ‘Obama’, alisema ubomoani huo umefanyika bila yeye kuhusishwa wala viongozi wa serikali za mitaa hiyo.

"Baada ya wananchi kunipa taarifa za tukio hilo, niliwasiliana na Ofisa Mtendaji Kata nikamuuliza kwanini wanaendesha operesheni hiyo bila kumjulisha akasema yeye amepewa maelekezo kutoka Manispaa kusimamia zoezi hilo," alisema.

Obama alisema kitendo cha kuwabomolea wananchi nyumba hizo ambao hawana hatia hakikubaliki, kwani iwapo hawataridhika na wakaamua kwenda mahakamani kushtaki watasababisha halmashauri iingie gharama katika kusimamia kesi hiyo.

Alisema inashangaza kutekelezwa kwa obomoaji huo, kwa sababu wananchi wa maeneo hayo walishafungua kesi mahakamani na kuweka zuio la kutobomoa nyumba zao ambapo kesi ya msingi ambayo ipo Mahakama Kuu haijamalizika.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabwepande, Mwalimu Muda Magwala, alisema zoezi hilo limewashtua, kwa sabahu serikali ya mtaa haikushirikishwa chochote, badala yake wabomoaji walifika eneo la tukio na kuanza kuzibomoa nyumba za wananchi.

"Juzi nilikuwa kwenye kikao ilipofika saa 10:00 jioni nilipigiwa simu na mjumbe wa shina kwamba nyumba za wananchi zinabomolewa na diwani alipojulishwa aliagiza wabomoaji wasitishe kwanza zoezi hilo, lakini hawakufanya hivyo na wananchi waliobomolewa wakalazimika kulala nje, " alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Mjimpya, Mohammed Basta, alisema ubomoaji ulipoanza aliwasiliana na Ofisa Mtendaji kata akamweleza kuwa amepewa maelekezo na mabosi wake kusimamia.

Nao waathirika wa tukio hilo, walisema wanashangaa nyumba zao kubomolewa wakati maeneo hayo waliyanunua kihalali na wana nyaraka zote za ununuzi ambazo nyingine zimetoka Manispaa.

Jesca Wilson ambaye alijitambulisha kuwa pia ni Ofisa Mtendaji wilayani Handeni Mkoani Tanga, alisema yeye ni kiongozi anafahamu hawezi kununua eneo bila kufuata taratibu, na kwamba anazo nyaraka halali za ununuzi wa eneo hilo.

"Shilingi milioni 30 kwa usawa huu iteketezwe bila kupewa notisi, kiukweli jana/(juzi) nilikuwa nipate ‘shok’ nianguke kwa presha nife baada ya kusikia nyumba yangu imebomolewa," alisema.

Jesca alimuomba Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gongwe, kufuatilia suala hilo ili haki iweze kutendeka kwani kitendo kilichofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ni cha uonevu na hakiwezi kukubalika.

Naye Jafari Lucas Magoto alisema anashangaa nyumba yake kubomolewa bure kwa kuwa kama eneo hilo lilikuwa na tatizo angemuuliza na serikali wangekaa pamoja wakajadiliana kupata mwafaka.

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, alipopigiwa simu kuhusu malalamiko ya wananchi hao alisema taarifa za kufanyika kwa operesheni ya kubomoa nyumba maeneo hayo alikuwa nazo.

" Zoezi hilo lilikuwa na baraka zote za Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Mkoa, tatizo asilimia kubwa Mabwepande kuna uvamizi sana wa viwanja, na sheria inataka ili ujenge lazima uwe na kibali cha ujenzi, " alisema.

Mnyonge alisema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alishatoa maelekezo kuwa serikali ya mtaa haihusiki na kuuza viwanja, lakini watu hawasikii.

IPP Media
 
Back
Top Bottom