Kabila la Wamwera kutoka wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi limefanya ibada maalum ya kuombea taifa amani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba mwaka huu
Akizungumza wakati wa ibada hiyo ya maombi, Kiongozi wa jadi wa Wamwela, Chief Nakyoto Ismail Hassan Malibiche, alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi, akiwataka Watanzania kuchagua viongozi kwa njia ya amani bila kushawishika kuingia kwenye vurugu au machafuko.
“Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakichochea fujo katika kipindi hiki muhimu kwa taifa. Hili halikubaliki kabisa. Amani ni tunu ambayo hatupaswi kuichezea,” alisema Chief Malibiche.
Soma > Chief Nakyoto atoa wito wa Amani na Utulivu kipindi cha Uchaguzi
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, aliwataka wananchi kuwa waangalifu dhidi ya wanasiasa na wanaharakati wanaotumia uchaguzi kama fursa ya kuleta vurugu na kuvuruga amani ya nchi
“Serikali haitavumilia mtu yeyote atakayejihusisha na uchochezi wa aina yoyote ile. Tunataka uchaguzi uwe wa amani na utulivu kama ilivyo desturi ya taifa letu,” alisema Moyo.
Ibada hiyo ya maombi imeonyesha mshikamano wa kijamii na kuthibitisha dhamira ya wananchi wa Nachingwea kushiriki uchaguzi kwa njia ya kidemokrasia, salama na yenye tija kwa taifa zima.