Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Maoni ya katuni
Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wameeleza kilio chao kwa serikali cha kufanya kazi katika mazingira magumu na kutaka yaboreshwe.
Madaktari hao pamoja na wafanyakazi wengine wa hospitali hiyo, walitoa kilio hicho juzi kwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, huku wakihoji sababu za kuwaongezea wabunge posho ya vikao kutoka
Shilingi 70,000 hadi shilingi 200,000 kwa siku, na kusema kwamba wao kama Madaktari Bingwa wanaona vitendo hivyo ni udhalilishaji mkubwa wanaofanyiwa na serikali.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Dk. Prim Saidia, alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa wafanyakazi wa hospitali hiyo hasa Madaktari Bingwa hawakubaliani na hatua ya kuwarundikia posho wabunge huku wao wakiendelea kutaabika. Alisema kitu cha kusikitisha ni kwamba daktari ambaye amesoma na kupata shahada
zaidi ya mbili anaendelea kupata posho ya Sh. 10,000 wakati katika ustawi wa nchi ndiye mtu muhimu na anayepaswa kuangaliwa kwa makini. Aliongeza kuwa kitendo cha kuwapa wabunge Sh. 200,000 huku madaktari na wafanyakazi wa hospitali wanalipwa kiasi kidogo na wengine hawalipwi kitu, ni kitendo cha kuwadharau.
Alieleza kwa ujumla madaktari wanaofanya kazi kwenye hospitali hiyo wanafanya kazi kwa ukwasi mkubwa kutokana na wengi wao kushindwa hata kufika hospitalini kutokana na kukosa fedha za nauli.
Malalamiko ya wataalamu wengi katika sekta ya umma wakiwemo madaktari kuhusu maslahi duni sio ya leo
bali ni ya miaka mingi. Mara kadhaa serikali imekuwa ikiyapokea na kuahidi kuyashughulikia kadri ya uwezo wa bajeti unavyoruhusu. Wengi tunafahamu jinsi serikali yetu ilivyo na uwezo mdogo wa kifedha kuweza kuongeza maslahi kwa watumishi. Hata hivyo, pamoja na uwezoo mdogo wa serikali kimapato, bado serikali haijaonyesha nia ya dhati ya kushughulikia malalamiko ya wataalamu hao yakiwemo ya madaktari.
Taaluma ya udaktari ni nyeti kwa maana kwamba wanataaluma hao wanahudumia watu wengi wenye matatizo mbalimbali ya kiafya wakati mwingine nje ya muda wa kawaida wa kazi.
Kutokana na hali hiyo, madaktari wanatakiwa kulipwa mshahara mzuri pamoja na marupurupu mengine ili waweze kufanya kazi zao kwa tija na ufanisi. Kwa kufanya hivyo, kungewasaidia kutekeleza majukumu yao bila kuwa na manunguniko wala tamaa ya kuiba mudawa kazi ili kwenda kufanya kazi nje ya mwajiri kwa ajili ya kuongeza kipato cha ziada.
Hatusemi kwamba madai ya madaktari yashughulikiwe kwa kuwaongezea maslahi kwa asilimia mia moja, bali serikali iyaongeze hatua kwa hatua badala ya kutoa ahadi zisizotekelezeka. Tena ahadi hizo kutolewa wakati unapoibuka mgogoro na madaktari kulazimika kugoma. Uzoefu wetu unaonyesha kwamba migomo ya
madaktari hususan katika Hospitali ya Muhimbili imekuwa ikiathiri wagonjwa ambao hawana hatia kutokana na kukosa huduma na wengine kupoteza maisha.
Kwa bahati mbaya sana, hatua ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni ya kutaka kujipandishia posho ya vikao kutoka Shilingi 70,000 hadi Shilingi 200,000 kwa siku imeibua chuki miongoni mwa watumishi wa serikali na jamii kwa ujumla. Hatua hiyo inatafsriwa kuwa serikali inawajali
wabunge kuliko watu wengine na ndiyo maana inawapandishia posho wanapozidai bila kujali hali ya uchumi.
Hii ndiyo sababu madaktari wa Muhimbili juzi walipomweleza Dk. Nkya malalamiko yao kuhusu maslahi, walikuwa wakilaani kupandishwa kwa posho ya vikao kwa wabunge bila wao na watumishi wengine wa umma
kuboreshewa maslahi. Ushauri wetu ni kwamba sasa umefika wakati kwa serikali kuangalia upya namna ya kushughulikia malalamiko ya watumishi wake wote badala ya kutoa ahadi wakati inapozuka migogoro ya kikazi hususan migomo na maandamano na baadaye kushindwa kuzitekeleza.
Ili kuepusha mgogoro wa kikazi na madaktari, itakuwa vyema ikiwa madai ya maslahi ya madaktari wetu yatashughulikiwa kwa wakati na serikali. Vile vile tunawaomba madaktari nao watumie utaratibu mzuri wa mazungumzo katika kudai maslahi yao na wakumbuke kuwa suo wao pekee wanaostahili kuboreshewa mafao bali watumishi wote wa umma.
CHANZO: NIPASHE