Analogia Malenga
JF-Expert Member
- Feb 24, 2012
- 5,108
- 10,191
Waenda kwa miguu jijini Dar es Salaam hudiriki kuvuka njia zenye msongamano wa magari barabarani licha ya kuwepo kwa madaraja yanayopita juu, huku wengi wao wakisema madaraja hayo ni marefu mno kuvuka, utafiti umebaini. Utafiti huo umefanywa na wanasayansi kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Taasisi ya Karolinska na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Haya yanajiri wakati serikali ikiwa imejenga na bado inapanga kujenga madaraja zaidi ya juu katika barabara zenye shughuli nyingi jijini ili kuwalinda waenda kwa miguu dhidi ya ajali za barabarani zinazoweza kuzuilika, pamoja na vifo. Takriban asilimia 30 ya vifo vyote vya barabarani nchini Tanzania vinahusisha waenda kwa miguu, huku majeraha mengi ya barabarani miongoni mwao yakitokana na vivuko, hii ni kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Kimataifa ya Usalama Barabarani.
Watafiti walifanya mahojiano na waenda kwa miguu 19 katika madaraja sita ya juu yaliyopo katika vitongoji vya Kawe, Buguruni, Manzese, Morocco, Kimara na Ubungo na kubaini kuwa kuna ushiriki mdogo wa jamii katika mipango na maamuzi ya ujenzi wa madaraja hayo.
Matokeo ya utafiti yanaonyesha kwamba watu wengi wanaelewa umuhimu wa madaraja lakini “Maoni ya wengi, kutokana na mahojiano yalikuwa ni kwamba walishangawa na kuona ujio wa miradi ya madaraja ya juu ya waenda kwa miguu…” Wakati wa utafiti huo, baadhi ya waenda kwa miguu walisema walikwepa kuvuka madaraja ya juu kwa sababu ya masuala ya usalama hasa nyakati za usiku, wizi na utimamu wao wa mwili.
Watafiti wanasema ushiriki wa jamii katika kupanga na kubuni madaraja haya, ungeongeza uelewa wa wazi na wa pamoja kuhusu jinsi, lini, wapi, na kwa nini daraja linapaswa kujengwa. “Faida nyingine yakuhusisha jamii katika mipango ingekuwa na katika kuhakikisha kwamba wanatunza miundombinu ya ndani na karibu na daraja,” wanasema watafiti, ambao wameshapisha matokeo yao katika Jarida la Kimataifa la Utafiti wa Mazingira na Afya ya Umma.
Idadi kubwa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam husafiri kila siku kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa sababu mbalimbali, huku wengi wa wasafiri hao wakiwa na umri wa kati ya miaka 15 hadi 45 ambalo ndilo kundi lenye tija kiuchumi. Kwa mujibu wa kituo cha Usalama Barabarani cha mwaka 2016, asilimia 54 ya vifo na majeruhi barabarani nchini Tanzania ni kati ya miaka 15 hadi 64 hivyo kuhitajika kuwepo kwa usimamizi thabiti wa usalama barabarani katika nyanja zote za usalama barabarani.
“Matokeo yetu pia yanaonyesha kuwa madaraja marefu ya waenda kwa miguu yanaweza kusababisha matumizi yasiyofaa sio tu na wazee, wagonjwa, na watu wenye shida ya mwili bali pia na vijana na wenye nguvu,” wanasema. Mtafiti mkuu, Daudi Katopola, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji cha Dar es Salaam anatoa wito wa kuwepo kwa ufumbuzi wa kiubunifu na wa gharama nafuu kwa wasafiri wanapovuka barabara.
“Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wamadaraja ya juu ilhali hayatumiki ipasavyo na watu waliokusudiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa,’’ anasema Katopola, ambaye anasomea Shahada ya Uzamivu ya Global Public Health katika Taasisi ya Karolinska nchini Sweden.
Chanzo: MwanaSayansi