SoC02 Madarasa ya TEHAMA muhimu Shuleni

SoC02 Madarasa ya TEHAMA muhimu Shuleni

Stories of Change - 2022 Competition

Abeida

Member
Joined
Jul 14, 2022
Posts
13
Reaction score
7
Abeid Abubakar

Namuuliza mtoto wangu anayesoma darasa la sita katika shule binafsi moja ya mchepuo wa Kiingereza kama wanafundishwa kompyuta.

Jibu lake la hapana linaninyong’onyesha.

Pengine ningeliamini kama angekuwa anasoma shule katika moja ya shule za umma, ambazo weng tunajua hali zake; shule ambazo hata huduma ya umeme ni jambo geni.

Nalazimika kumpa ‘ABC’ za namna ya kutumia kifaa hicho kupitia kompyuta mpakato yangu na anaonekana kuwa na juhudi kweli ya kujifunza.

Najiuliza huyu anaakisi mamilioni mangapi ya watoto wa Kitanzania ambao kama wangeanza kufinyangwa tangu wadogo kutumia vifaa hivi na vinginevyo vya kiteknolojia kama vishkwambi, tabiti projekta nk, Taifa litakuaje miaka ijayo?

Bila shaka tutakuwa na Taifa lenye watu wengi wenye weledi wa Tehama na teknoloji za kisasa kwa jumla.
Kwa nini leo vifaa vya Tehama na teknolojia kwa jumla havina nafasi katika shule zetu? Kwa nini kwa mfano hatuna maktaba za Tehama?

Hatuwezi kufikiria maendeleo ikiwa hatuanzi kufundisha stadi za kuwa wagunduzi wa teknolojia tangu wakiwa wadogo shule za msingi wakakua na stadi hizo hadi wanapokuwa wakubwa.

Tunaweza tusiwe na vifaa hivi kwa maelfu lakini vichache vinawezekana na vikawa chachu kwa wanafunzi kujifunza.

Lakini ili tufike huko lazima tuhakikishe kuwa shule zinakuwa na umeme hata kama wa nishati ya jua na pia kuunganishwa na mkongo wa taifa kwa ajili ya upatikanaji wa intaneti.

Ikiwa wakati ule wa janga la Uviko-19, tuliweza kuona jitihada za kusimamia elimu kidijitali, tukaona kwa mfano Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), wakifungua maktaba mtandao, shule zikawa na programu za ufundishaji kisasa, kwa nini hilo halifanyiki sasa?

Tuanze wapi?
Nashauri kuwa na darasa mfano la Tehama na teknolojia kwa ujumla kwa kila shule au hata baadhi ya shule za msingi.

Darasa hili liwe ama maabara ya kivitendo lililosheheni vifaa vya kisasa. Inawezekana wanafunzi wote wasinufaike, lakini kukawa na wachache maalumu kupitia program maalumu. Naamini miongoni mwa hao wachache hatutokosa mabingwa wa Tehama miaka ijayo.

Kukiwa na jengo, vifaa na msimamizi wa mafunzo hata kwa kumtumia mwalimu mmoja shuleni hapo mwenye mafunzo maalumu, darasa hilo linaweza kuja kutoa matunda makubwa. Madarasa hayo yanaweza kujengwa na Serikali, mashirika au taasisi binafsi.

Ikiwa leo tunaona namna taasisi mbalimbali zinavyohimu kutoa ufadhili wa kununua madawati, ujenzi wa vyumba vya madarasa, kwa nini hamasa pia isiwe katika ujenzi wa madarasa haya maalumu ya Tehama?
Chombo kama Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF), kinaweza kikatumika kwa kiwango kikubwa kuratibu madarasa haya, ikiwa kitawezeshwa na uzuri chombo hicho kimekuwa kikifanya hivyo.

Kwa mfano, taarifa ya mfuko huo ya Septemba 14 2021 iliyomo kwenye tovuti yake ya ya www.ucsaf.go.tz, tayari mfuko umetoa mafunzo ya Tehama kwa wanafunzi wa kike 744 wa shule za umma Tanzania nzima, imetoa vifaa vya Tehama kwa shule takribani 700 pamoja na kuunganisha shule 400 za umma na mtandao wa intaneti.

Hapa ndipo pa kuanzia. Moto huu wa UCSAF unaweza kusambaa zaidi shuleni kwa kuwa na madarasa haya maalumu,

Tunaweza kuwa na madarasa ya Tehama katika shule nyingi japo kwa kuanzia yakawa na vifaa kama kompyuta, vishkwambi, simu za kisasa na vinginevyo vinavyoweza kuwajengea watoto uwezo wa kuja kuwa wabunifu wa Tehama.

Ikiwa tutashindwa kuwa na madarasa hayo kwa kila shule, tunaweza kuwa na darasa angalau moja kwa ngazi ya kata, tarafa, wilaya au hata mkoa. Darasa hilo likatumika kuwakusanya watoto ambao tumewabaini kuwa na utundu wa kisayansi na kisha kuwawekea miundombinu ya kutosha.

Kwa wafadhili mfano wafanyabiashara, mashirika binafsi na asasi za kiraia, ujenzi wa madarasa ya aina hii sidhani kama unaweza kuwa kibarua kizito kwao. Muhimu ni mamlaka za kiserikali na wadau wa elimu kwa jumla kuchagiza uanzishwaji wa madarasa haya.

Kama kwa sasa baadhi ya shule zina madarasa ya kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, kwa mtindo huu huu tunaweza kuchagua shule kadhaa tukaziwekea nazo madarasa ya Tehama, lengo ni kunoa watoto na kuwaandaa kuwa wabunifu katika teknolojia za kisasa ambazo ndizo zinazoendesha ulimwengu.

Tusipokuwa na mikakati mfano wa huu, sioni namna ambayo Watanzania tunaweza kushiriki katika mapinduzi ya kiteknolojia yanayoibuka kila siku ambayo yamejikita katika matumizi makubwa ya vifaa vya kiteknolojia vinavyotumia Tehama na mashine.

Tukiipa Tehama kisogo, hata ndoto ya kuwa na nchi ya uchumi wa kati wa juu unaotegemea viwanda ifiapo 2025, inaweza kuyeyuka tukaendelea kubaki nyuma kimaendeleo.

Nina ndoto kuona watoto katika madarasa haya wakipatiwa stadi za msingi za Tehama, ili hatimaye kuwajengea ujuzi wa masuala mbalimbali ya kiteknolojia kupitia sayansi ya kompyuta na fani kadhaa za kisasa kama ‘Artificial Intelligence’ ambayo inachagiza mashine na kompyuta kufanya kazi zenye kuhitaji akili za kibinadamu.

Nina ndoto ya kuona madarasa haya yanakuwa chachu ya kuwajengea watoto msingi wa kuja kuwa wataalamu wa ufundi wa vifaa vya kiteknolojia kama simu za kisasa. Waje kuwa wagunduzi wa programu tumishi zenye manufaa kwa Taifa katika kila sekta, wabunifu wa mitandao ya kijamii na programu nyingine mbalimbali za kompyuta na teknolojia kwa jumla.

Tukijipanga japo kwa kuwa na shule kadhaa za mfano, naona kabisa Tanzania ijayo ya wagunduzi kama Bill gates (Microsoft), Mark Zuckerberg (Facebook/ Meta), Steve Jobs (Apple) na wengineo wengi.

Kama hatutofika ngazi ya magwiji hawa, bado naiona Tanzania itakayokuwa imesheheni gunduzi na bunifu kama za Max malipo (kampuni ya miamala kwa njia za kielektroniki), VSOMO (elimu ya ufundi stadi kupitia simu za mkononi chini ya Godfrey Magila, majukwaa ya kimitandao kama Jamii forum na Club House na bunifu nyinginezo nyingi ambazo wabunifu wake sio tu wananufaika kiuchumi, lakini wanatoa mchango kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mwandishi ni mkazi wa Dar es Salaam. Anapatikana kwa barua pepe: abeidothman@gmail.com
 
Upvote 2
wadau uzi huo leteni mawazo yenu. Nawashukuru
 
Back
Top Bottom