SoC04 Madini ya kimkakati Tanzania, lulu inayotazamwa na dunia. Je, tumejiandaa?

SoC04 Madini ya kimkakati Tanzania, lulu inayotazamwa na dunia. Je, tumejiandaa?

Tanzania Tuitakayo competition threads

ngamshe

Member
Joined
Feb 22, 2015
Posts
6
Reaction score
1
Tanzania tuiitakayo ni nchi yenye maendeleo makubwa zaidi ya watu katika ukanda wa Afrika mashariki. Itakayoweza kuondoa kabisa umasikini na kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo. Hii ni kutokana na ukweli kuwa Tanzania ipo eneo zuri kiuchumi (Good economic geographical position), kwa kuwa na Bahari ya Hindi. Imepakana na nchi nane, ardhi yenye rutuba, Madini , vivutio vya utalii, Watu, maji safi na madini mengi, kama: metali (dhahabu, chuma na nikeli), vito (ruby, spinel na Tanzanite), ujenzi (soda ash, jasi), madini ya nishati (makaa ya mawe, kinywe, urani) pia gesi asilia na mafuta.

Zipo njia nyingi za kupita kufikia Tanzania tutakayo, kwasasa tutazame kuhusu madini ya kimkakati kama turufu yetu nikiwa na Imani kuwa madini haya yatatutoa!

Mchango Sekta ya Madini Kiuchumi

Takwimu za Serikali zinaonesha kwamba mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa la Mwaka 2023 ni 9.0% sekta ya madini imekua kwa 11.3% tu, Aidha, Sekta ya Madini imekuwa kinara kwa kuingiza fedha za kigeni nchini 56.2% ya thamani ya mauzo ya bidhaa zisizo za asili zilizouzwa nje ya nchi, mchango huo ni mdogo sana. Tanzania inastahili zaidi ya hili, tunaweza kufika mchango kwenye pato la taifa 30% mwaka 2050 tukijiandaa kimkakati.

Madini ya Kimkakati Yanayopatikana Tanzania.

Madini haya kiingereza wanayaita “Strategic/transitional/green/critical Minerals” kutokana na umuhimu wake katika uchumi wa Dunia ya sasa, madini haya ni lulu inayotafutwa na kutazamwa na Dunia.

Kwa mujibu wa Taarifa za Tume ya Madini, Wizara ya Madini na Taaisis ya Jiolojia na Utafiti Tanzania (GST) , Tanzania kuna mengi ya kimkakati miongoni mwayo ni Lithium – Dodoma, Rare earh Element (REE) - wigu hill mbeya na Nguala Songwe , Cobalt - Kabanga Ngara, Lithium- Hombolo Dodoma , Kinywe - Ruangwa mlima Chiliogali- Lindi na Epanko-Mahenge Morogoro, Nikeli-Kabanga Ngara, kapalungulu Kigoma, Dutwa Briadi, Urani - Dodoma na Namtumbo (mkuju na madaba na luwegu) Ruvuma, Phosphate - Malizi na Minjingu Arusha, Tantalum –Niobium- Panda hill Mbeya, Helium – ziwa Rukwa.
1000079723.jpg

Picha kutoka wizara ya madini.

Kwa nini Madini ya Kimkakati ni Muhimu Leo?

Kwanza, masuala ya mazingira, Miongoni mwa jitihada iliyochukuliwa na Jumuiya za Kimataifa ni Itifaki ya Kyoto (Kyoto Protocol) ya 1997 na Mapatano ya Paris (Paris Climate Agreement) ya 2015. Kupunguza Hewa Ukaa (Net-Zero-Emission) ifikapo 2050 kwa sehemu kubwa madini haya yanazalisha nishati mbadala. Pili, maendeleo ya Sayansi na Teknolojia. Tatu, masuala ya ulinzi na usalama. Nne, uchumi, hizi ni malighafi viwandani ambazo hutengeneza ajira nyingi na bidhaa zinazoweza kuuzwa nje ya nchi kwa thamani kubwa.

Mikakati ya Mataifa Makubwa.

Kuna msuguano mkubwa wa Utawala wa Dunia (Global-Hegemony), kuanzishwa kwa BRICS, Vita eneo la mashariki ya kati, vita ya Ukraine na Urusi vinasukuma Dunia kujitafakari katika kutetea ushawishi wake kwenye Siasa-uchumi. Mbinu kubwa wanayotumia Afrika ni ushawishi wa misaada, mikopo na uwekezaji (FDI) kimikataba.

Machi 2024, Baraza la Umoja wa Ulaya lilipitisha Sheria ya Madini Ghafi ya Kimakakati (Critical-Raw-Material-Mineral, CRM-Act) https://europa.eu/!wwncnT

Idara ya Nishati ya Marekani (Department-of-Energy) imefanya uchambuzi wa kina kuhusu mahitaji ya madini ya kimkakati DOE Critical Materials Report - 2023 (energy.gov)

Nchi za asia wapo mbioni kuwekeza nje ili kupunguza utegemezi kwa mafuta, na kuwekeza kwenye viwanda na teknolojia.

Kasi ya Utafutaji, Uzuiaji Maeneo na Uchimbaji wa Madini ya Kimakakati.

Taarifa ya Tume ya madini inaonesha kuna ongezeko la maombi na leseni za madini ya kimkakati zinazokuja kwa sura ya Utafiti (PLs) ambapo kwa mwaka 2018 leseni za utafiti zilizoombwa zilikua 120 lakini mwaka 2023 leseni ziliombwa 333 na Leseni maalum za uchimbaji (SMLs) zimetolewa nne (4) ndani ya miaka miwili kutoka 2021/2023, hata hivyo yapo malalamiko ya kuwa wenye hizi leseni wanahodhi maeneo.
1000094997.png

Picha kutoka Tume ya madini.

Tanzania na Uwekezaji wa Madini ya Kimkakati.

Tayari imeingia kwenye makubaliano na majadiliano kuhusu sekta hii.

  • Januari 2021, Tanzania iliingia mkataba na Kampuni ya Uingereza, LZ Nickel, itawekeza kwenye Mradi wa Uchimmbaji wa Nikeli(Miaka-33).
  • April 2023, Tanzania iliingia mkataba wa madini wenye thamani ya Dola Milioni 667 na kampuni tatu za Australia yatakayochimbwa Lindi, Morogoro na Songwe.
  • Mei 2024, Tanzania ilisaini makubaliano na nchi ya Korea Kusini kuhusu kuwekeza katika madini ya kimkakati (Nikel, Lithium na Kinywe.)
  • Juni 12, 2024 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko alifanya mazungumzo na Naibu Katibu wa Idara ya Nishati ya Marekani (Deputy Secretary of Energy), Mr. David Turk Kuhusu nishati safi na madini ya kimkakati hasa Kinywe na Nikel.
Je, Tumejiandaa Kimkakati?

Hapana. Kujiandaa kimkakati ni kuwa na mpango wa kufaidika na rasilimali hizi na kuchukua tahadhari za kiusalama ili kuunufaisha umma kupitia Sekta za Uchumi. Haya si madini ya kawaida, nayo huisha. Bado hatujatunga mifumo ya kisheria (Legal-Framework) ya namna ya kushughulikia na kunufaika na madini haya ya kimkakati, iliyopo ni ya jumla inayotumika kwenye madini mengine. Ulaya wanatunga sheria seuze sisi tuliyonayo?

Nini Kifanyike?

  1. Tume ya Mipango iratibu Mjadala wa Kitaifa Kuhusu Rasilimali za Madini ya Kimakati (SMR) wa Wananchi na Wataalamu, maazimio yake yatengenezewe mkakati wa miaka 50 katika uchumi wa nchi (50 years Strategic Mineral Plan) kutatua tatizo la ajira na huduma za jamii (afya, elimu na nishati).
  2. Serikali isiingie zaidi mikataba ya uchimbaji, ipeleke mswada Bungeni wa Mfumo wa Kisheria (Legal-Framework) wa Madini ya Kimkakati, kuanzia sera maalum ya madini ya kimkakati na mfumo wa kikodi kuiwezesha Tanzania kumiliki zaidi miradi yote kwa Ubia, uwe si chini ya 51% kwa Tanzania, sio kigMawio kiduchu.
  3. Bunge litumie mamlaka yake kutazama makubaliano ya Serikali yanayohusu madini ya kimkakati na kuyachambua kuona ni kwa namna gani Taifa litanufaika, kwa kutumia Sheria ya Mikataba ya Utajiri wa Maliasili na Rasilimali (Upitiaji na Uboreshaji wa Masharti Yenye Shaka) ya Mwaka 2017. litunge sheria maalum itakayohusu madini haya.
Hitimisho

Serikali kama isipofanya maamuzi haraka ipo hatari kama Taifa lisinufaike ipasavyo kama ilivyo kwenye dhahabu, Tanzanite na Almasi. Hata hivyo maandalizi hayo yatazame usalama wa Taifa tukiwa na mafunzo kutoka DRC, Msumbiji na Sudan Kusini kwani kwa sehemu fulani yanatokana na sehemu na utajiri wao. Chaguo ni letu, yanyonywe, yatutoe au yatupofoe!
 

Attachments

  • 1000094997.png
    1000094997.png
    187.3 KB · Views: 4
  • 1000094997.png
    1000094997.png
    187.3 KB · Views: 9
Upvote 5
Back
Top Bottom