Maelezo ya Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) ACT, Ismail Jussa alipozungumza na Wanahabari Makao Makuu ya Chama, Vuga, Zanzibar, Februari 27, 2025

Maelezo ya Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) ACT, Ismail Jussa alipozungumza na Wanahabari Makao Makuu ya Chama, Vuga, Zanzibar, Februari 27, 2025

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
WhatsApp Image 2025-02-27 at 17.26.05_2c38aed2.jpg

UTANGULIZI:
Nimewaita hapa leo kuzungumzia kashfa kubwa (major scandal) inayozunguka kile kilichopewa jina la uwekezaji wa kimataifa katika Bandari ya Zanzibar ambacho sasa kinawatafuna wananchi masikini wa Zanzibar walioangushiwa zigo kubwa la kubeba gharama za mradi huo wa kashfa. Zigo hilo linawatafuna zaidi masikini za Mungu kipindi hichi tukiwa tunaingia mwezi mtukufu wa Ramadhan, hali ya kuwa tayari wananchi hao wamefukarishwa na utawala uliopo wa Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar chini ya Rais Hussein Mwinyi, katika kiwango cha umasikini na ufukara ambacho hakijawahi kuonekana katika miaka ya karibuni.

Hatua yangu hii ya leo ni kutimiza ahadi niliyoitoa tarehe 16 Februari, 2025 nilipokuwa nikizungumza na wananchi wa Zanzibar kupitia mkutano wa hadhara wa Chama chetu cha ACT Wazalendo uliofanyika huko Tomondo Mshelishelini, Wilaya ya Magharibi B Unguja. Siku hiyo nilizungumzia kashfa kadhaa zinazoigubika Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Hussein Mwinyi lakini kutokana na ufinyu wa muda nikasema nitafanya mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia kashfa kubwa inayozunguka hicho kinachoitwa kuwa eti ni uwekezaji wa kimataifa katika Bandari ya Zanzibar.

Binadamu ni wepesi wa kujisahaulisha wakeshatimiza yao. Lakini sisi wengine hatusahau. Tuwakumbushe basi. Ilikuwa ni katika kipindi kile cha mikutano ya kila mwezi kati ya Rais Hussein Mwinyi na waandishi wa habari (ambayo baada ya majigambo mengi, sasa imeota mbawa) kwamba hichi kinachoitwa uwekelezaji wa kimataifa katika bandari kilipigiwa upatu kwa hoja kwamba menejimenti ya Shirika la Bandari la Zanzibar (Zanzibar Ports Corporation) iliyokuwepo ilikuwa imeshindwa kazi, kwamba hakuna ufanisi kwenye bandari hiyo na kwamba hali hiyo imepelekea usumbufu mkubwa kwa watumiaji, imezorotesha biashara na kuongeza gharama za maisha kwa wananchi wa Zanzibar kunakotokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa.

Tuliahidiwa kwamba mwekezaji anayepigiwa upatu atatatua matatizo yaliyokuwepo na atafanikisha mambo yafuatayo:
1. Atapunguza muda wa meli kukaa bandarini na kupakua makontena na kwamba meli haitokaa zaidi ya siku mbili kwa kazi hiyo;
2. Atapunguza muda wa wenye makontena kupata makontena yao;
3. Ataondosha urasimu na kuleta ufanisi wa kiwango cha kimataifa katika upakuaji wa makontena katika hatua zote kuanzia kwenye utayarishaji wa nyaraka hadi utoaji wa makontena;
4. Ataongeza eneo la kuwekea makontena ili kuondosha msongamano wa makontena uliokuwepo;
5. Atapunguza viwango vya gharama (charges) kwa watumiaji wa bandari.

Tulitangaziwa kwa mbwembwe zote kwamba mwekezaji wa kimataifa anayekuja ni kampuni ya Ballore ya Ufaransa ambayo tuliambiwa ina uwezo mkubwa na imejijengea sifa za kimataifa.

YALIYOJIRI:
Jambo la mwanzo ambalo wananchi wa Zanzibar walilishuhudia lilikuwa ni vituko katika utiaji saini wa hicho kilichoitwa uwekezaji wa kimataifa. Mtu angetegemea kwa jinsi uwekezaji huo ulivyopambwa na Rais Hussein Mwinyi wakati anaupigia debe basi utiaji saini ungefanyiwa mbwembwe zote kama ilivyo kawaida ya mambo ya Serikali hii. Lakini tulichokishuhudia ni utiaji saini huo kufanyika kienyeji enyeji, tena wakati wa usiku.

Tukashuhudia badala ya kutia saini na kampuni ya Ballore ya Ufaransa, utiaji saini ukifanywa na kampuni iliyoitwa African Global Logistics (AGL). Lakini wakati wa utekelezaji ulipofika, hata hiyo kampuni ya African Global Logistics (AGL) hatukuiona na badala yake tukasukumiwa kitu kinachoitwa Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT).

Hivi watu hawa wanatufanya watu wa Zanzibar ni wajinga kiasi gani hata tushindwe kuona maigizo haya?
Tukumbushe pia kuwa hatua hii ya bandari kukabidhiwa huyo anayeitwa mwekezaji ilifanywa baada ya ukiukwaji mkubwa wa sheria za Zanzibar, na hasa Sheria ya Manunuzi ya Umma kwenye eneo la taratibu za zabuni (tendering process and procedures) na Sheria ya Ushindani wa Haki (fair competition).
Ubabaishaji ulionekanwa tokea mapema.

Hakukutangazwa zabuni na wala hakukufanyika uchunguzi (due diligence) wa kujiridhisha kuhusu ni nani hasa huyu mwekezaji anayepigiwa upatu ambaye anataka kukabidhiwa lango kuu la kuingilia na kutoka Zanzibar, kwa maana ya bandari kuu ya nchi yetu.

Duniani kote, bandari ni sehemu muhimu kwa usalama wa nchi na huwa haipaswi kutolewa kiholela tu kama ilivyofanyika hapa kwetu.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed alipoulizwa katika Baraza la Wawakilishi kuhusu uzoefu wa kampuni iliyopewa bandari yetu na iwapo Serikali iliwahi kuifanyia tathmini kabla, alijibu kuwa kampuni ni nzuri na inajulikana kimataifa, na hivyo Serikali haikuona haja ya kuifanyia uchunguzi kwa sababu ilikuwa imejiridhisha kuhusu uwezo wake. Binafsi, siamini kwamba Dk. Khalid mwenyewe alikuwa anayaamini yale aliyokuwa akiyasema.

Tunasema hayo kwa sababu wakati wa majadiliano kuhusiana na mkataba huu, hata Timu ya Majadiliano ya Serikali (Government Negotiating Team - GNT) ilikuwa inasukumwa tu mpaka kufikia sehemu ya watu muhimu kutoka Serikalini katika timu hiyo kujitoa kwa kutokubaliana na yaliyokuwa yanaendelea.

UWEKEZAJI ULIOFANYIKA UKO WAPI?
Sasa ni miaka miwili tokea mwekezaji ambaye mwanzoni tuliambiwa ni kampuni ya Ballore, kisha akageuka kuwa ni Africa Global Logistics (AGL) na hatimaye akageuka kuwa ni Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT), akabidhiwe Bandari. Wananchi wa Zanzibar wanajiuliza mwekezaji huyu amewekeza nini hadi sasa?
Kinyume chake, kama ilivyo kawaida ya miradi ya kijanja janja kama hii, ni Serikali kupitia fedha za wananchi maskini wa Zanzibar ambao wanakamuliwa kodi za komesha kila uchao, ndiyo iliyowekeza tena kwa gharama zinazoonesha ufisadi mkubwa katika bandari hiyo na kumjengea mwekezaji huyu mazingira ya kuja kuchuma kwa migongo ya wananchi maskini wa Zanzibar.
WhatsApp Image 2025-02-27 at 17.26.05_8c585802.jpg
Hapa niwakumbushe tena jambo ambalo nililisema kwenye mikutano ya hadhara kwamba miezi michache tu kabla ya huyu anayeitwa mwekezaji kupewa bandari hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Shirika la Bandari la Zanzibar ilitumia fedha za walipa kodi wa Zanzibar kiasi cha shilingi bilioni 17 kununua vifaa vya bandari na kuweka mfumo wa e-Port. Gharama za kuweka mfumo wa e-Port peke yake zilikuwa ni dola za Kimarekani milioni 6.8 (yaani US $6.8 Million). Hii ilikuwa ni tofauti kubwa sana na kiwango cha dola za Kimarekani 645,000 (yaani US $665,000) tu zilizotumika kufunga mfumo wa e-Port katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni kubwa sana ukilinganisha na Bandari ya Malindi, Zanzibar.

Fedha hizi za walipa kodi masikini wa Zanzibar zilitumiwa kumtengenezea mazingira mwekezaji aliyekuwa anaandaliwa wakati huo, ili yeye asitumie chochote kuweka vifaa na badala yake akabidhiwe bandari ikiwa tayari ina vifaa hivyo na kujichumia faida aliyokuwa hakuitolea jasho. Tunajiuliza baada ya miaka miwili, mwekezaji kawekeza nini? Walioko bandarini wanasema mwekezaji huyu hakuleta hata kalamu na karatasi na badala yake anatumia kalamu na karatasi alizozikuta bandarini.

Haya yanafanyika huku mwekezaji huyo aliyekuwa hakuwekeza chochote akiramba asilimia 70 ya faida na Serikali kupitia Shirika la Bandari la Zanzibar iliyofanya uwekezaji wote ikiambulia asilimia 30 tu ya faida.

Tulinganishe hili na mwekezaji mzalendo, Sheikh Said Salim Bakhresa kupitia kampuni ya AZAM MARINE, ambaye yeye biashara yake ni ya usafiri wa baharini lakini bado wakati wa Serikali ya Awamu ya Saba alijitolea gharama zake binafsi kutengeneza eneo la kuhudumia abiria (passenger terminal) na kulifanya kuwa la kisasa bila ya kuchangiwa chochote na Serikali.

Hadi leo, Serikali na wananchi wa Zanzibar wanafaidika na msaada ule.

HALI ILIVYO SASA:
Hali ilivyo sasa ni kwamba watumiaji wa bandari ile na wananchi wa Zanzibar wanasaga meno huku mwekezaji anakula faida raha mustarehe. Hakuna hata moja katika yale mambo matano yaliyoahidiwa wakati mradi huu unapigiwa upatu yaliyotimizwa. Tujiulize:
1. Je, kweli muda wa meli kukaa bandarini na kupakua makontena umepungua? Na je, kweli meli hazikai zaidi ya siku mbili kama tulivyoahidiwa?
6. Je, kweli muda wa wenye mizigo kupata mizigo yao umepungua au umeongezeka?

7. Je, kweli urasimu katika upakuaji wa makontena katika hatua zote kuanzia kwenye utayarishaji wa nyaraka hadi utoaji wa mizigo umepungua au umeongezeka?

8. Je, kweli eneo la kuwekea makontena limeongezwa? Na je, kweli msongamano wa makontena uliokuwepo umeondoka au umeongezeka?

9. Je, kweli gharama (charges) kwa watumiaji wa bandari zimepungua au zimeongezeka?

Majibu ya maswali hayo wala sina haja ya kuwapa mimi. Kikao cha juzi, tarehe 25/02/2025 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jengo la ZAWA kati ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohammed na uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) kwa upande mmoja, na watumiaji wa Bandari wakiwemo wafanyabiashara na wanaotoa huduma za kutoa mizigo bandarini kwa upande wa pili, kimeanika uoza ulioletwa na mwekezaji huyu kutokana na huduma zote kuzorota na kuwasababishia usumbufu mkubwa watumiaji, kuongeza gharama kwa wafanyabiashara na watoaji mizigo bandarini na kupelekea kupandisha bei za bidhaa kwa wananchi wa Zanzibar. Kwa ufupi, ni kielelezo kikubwa cha ufisadi na kufeli kwa Serikali iliyopo madarakani.

Hivi tunavyozungumza, tena katika kipindi muhimu cha kukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo mahitaji ya wananchi huongezeka na ukali wa maisha yao ndiyo hudhihirika zaidi kutokana na umasikini walioingizwa na Serikali ya CCM isiyowajali, tumeshuhudia msongamano mkubwa wa meli za mizigo ambapo meli zinakaa zaidi ya wiki mbili kusubiri kupakua mizigo.

Miongoni mwa meli zilizopo bandarini zinazosubiri kushusha mizigo ni hizi zifuatazo:

1. MV LAURA
2. MV LORD H
3. MV LIMA
4. MV ZANZIBAR EXPRESS
5. MV NAHA
6. MV KAIZER
7. MV TRITEX GLORY
8. MV MIREMBE JUNITH
9. MV BRO QUAN
10. MV AMU JAMEEL
11. MV ST. JOHN
12. MV BAODA
13. MV AL AMAL
14. MV CMA CGM
15. MV CONT SHIP VIE
16. MV SISLEEN

Kama inavyoeleweka, wafanyabiashara wengi hapa Zanzibar huongeza uagizaji wa bidhaa katika kipindi kinachokaribia mwezi mtukufu wa Ramadhan, ili kukidhi mahitaji ya wananchi na pia kusaidia kushusha bei ya bidhaa kwa sababu bidhaa zinapokuwa nyingi kwenye maghala na maduka ndipo bei hushuka. Hii ni kanuni ya msingi kwenye biashara inayojulikana na kila mtu, kwa maana ya ‘supply and demand’.

Malalamiko makubwa kwa mwaka wa pili sasa tokea mwekezaji anayetajwa akabidhiwe bandari ni kwamba kukosekana kwa ufanisi na kushindwa kwake kazi kunaonekana zaidi katika kipindi kama hichi cha kuelekea Ramadhan ambapo mahitaji ndiyo huwa makubwa zaidi.

Wafanyabiashara wanalalamika kwamba makontena yao yanachelewa kutolewa huku yakiwa yameshafika Zanzibar na huyapata baada ya kupita mwezi wa Ramadhan na kuwasababishia hasara kubwa.

Huduma za ushushaji wa makontena zimezidi kuzorota kwani tofauti na zamani, kwa sasa mtu hawezi kupata makontena yake hadi yapelekwe kunakoitwa ICD yaani Inland Container Yard ya Maruhubi ambako huchukua zaidi ya siku saba hadi siku kumi, wakati tuliambiwa kuwa shughuli zote za ushushaji makontena hazitozidi siku mbili.

Uzembe mwengine au pengine ni mpango wa makusudi wa kuendelea kuwakamua watu fedha, ni kwamba mtu anaweza akawa tayari ameshalipa fedha zote lakini kuipata kontena yake ikawa kazi kubwa sana.

Na siku akiipata anatakiwa kulipia gharama za ‘storage’ kwa siku ilizokaa wakati ucheleweshaji ulisababishwa na mwekezaji.

Watumiaji wa Bandari na hasa wanaofanya kazi ya utoaji wa mizigo wanathibitisha kwamba kabla ya kukabidhiwa mwekezaji, mtu aliweza kutoa kati ya makontena 10 hadi 15 kwa siku lakini tokea kuja mwekezaji asiyefanya uwekezaji mtu anatoa kontena moja tu kwa siku.

Kwa sasa, meli nyingi za mizigo zinakataa kuja Zanzibar kutokana na usumbufu huo huku kukiwa na mamia ya makontena ya Zanzibar yaliyorundikana kwenye bandari ya Mombasa, nchini Kenya kwa zaidi ya mwezi mmoja yakisubiri meli ndogo kuyaleta Zanzibar.

Meli hizo ndogo zinapochelewa kupata nafasi ya kupakua haraka mizigo kwenye bandari ya Malindi zinashindwa kurudi kwa wakati Mombasa kupakia na kuleta makontena mengine.

Athari za hali hii iliyosababishwa na mwekezaji huyu aliyekuwa hakufanya uwekezaji wowote na sasa kazi imemshinda ni kuyavuruga maisha ya Wazanzibari kwa kiasi kikubwa sana. Sote tunajua kwamba wananchi wengi wa Zanzibar vipato vyao vinatokana na biashara na mzunguko wa fedha unaotokana na biashara. Kundi hili linajumuisha wafanyabiashara wakubwa wanaoleta bidhaa kutoka nje ya nchi, watoa huduma (agents) wa kutoa mizigo bandarini, wachukuzi, wanaofanya kazi za magari ya usafirishaji, wanaofunga mizigo, wafanyabishara wa rejareja, hadi watumiaji majumbani.

Yote haya yanazifanya hali za maisha ya wananchi ambazo ni ngumu kuzidi kuwa ngumu zaidi. Huduma zinakosekana na bidhaa zinazidi kupanda bei.

Ifikirie hali hiyo sasa kwa wananchi walioko Pemba ambao hawana bandari ya kushushia mizigo (ukiweka upande ule usanii na maigizo yaliyofanywa ya kuchukua kimeli kimoja kikenda kuteremsha mzigo bandari ya Mkoani Pemba). Wananchi wa Pemba tangu hapo wanadhilika na bei za bidhaa kwao huwa kubwa zaidi kutokana na kulipia gharama za ziada za usafirishaji kutoka Unguja kwenda Pemba.

Sasa unapozorotesha huduma kwenye bandari ya Malindi, Unguja na kuongeza gharama maana yake umewaongezea gharama za maisha maradufu wananchi wa kisiwa cha Pemba.

Hata wananchi maskini wanaotegemea sadaka za mahitaji yao mbali mbali kutoka kwa wanaojiweza wanaathirika maana sehemu kubwa ya sadaka hizo zimo kwenye makontena yaliyokwamishwa na mwekezaji kutokana na kushindwa kwake kazi.

GHARAMA ZA KUTOA MIZIGO BANDARINI:
Gharama za kutoa mizigo bandarini (port charges) ambazo ziliahidiwa kwamba zingepungua chini ya mwekezaji zimeongezeka kwa viwango na kasi ya kutisha. Kabla ya kuja mwekezaji asiyefanya uwekezaji wowote, gharama za bandari (port charges) zilikuwa TSHS. 450,000 kwa kontena. Alipoingia mwekezaji tu, gharama zikapandishwa hadi TSHS. 600,000 kwa kontena. Haukupita muda, gharama zikaongezwa tena hadi TSHS. 870,000 kwa kontena.

Mtakumbuka, kipindi hichi ndipo pale wafanyabiashara na watoa huduma za mizigo walipogoma. Pamoja na ahadi zilizotolewa kushughulikia suala hilo ambalo lilifikisha mpaka kuwa na vikao Ikulu, hakuna kilichofanywa.

Matokeo yake, sasa mwekezaji asiyefanya uwekezaji kapandisha gharama hizo hadi kufikia TSHS. 1,370,000 kwa kontena, huku akidai kwamba ongezeko hilo linahusisha gharama za kutoa kontena kutoka bandarini Malindi kupeleka ICD ya Maruhubi.

Gharama hizo zimetokana na watoaji mizigo kutakiwa kulipa dola za Kimarekani 65 (yaani US $65) za usafiri kutoka Malindi hadi Maruhubi, na baada ya hapo gharama za ziada za dola za Kimarekani 105 (yaani US $105) za mzigo kutolewa Maruhubi ikiwa ni jumla ya dola za Kimarekani 170 (yaani US $75).

Ifahamike kwamba mtu haruhusiwi kutafuta usafiri wake mwenyewe wa kusafirisha kontena lake kutoka bandari ya Malindi kuja Maruhubi.

Wote wanalazimika kutumia magari yaliyowekwa na mwekezaji asiyefanya uwekezaji, tena kwa gharama ambazo ni ‘fixed’ zilizoamuliwa na mwekezaji. Ukitaka kuona vituko zaidi na kujua nani yuko nyuma ya mradi huo, tazama magari hayo yameandikwa maneno gani ya kampeni za kisiasa na kampeni hizo zinamlenga nani.

Wahenga walisema kuwa ukistaajabu ya Mussa, utaona ya Firauni. Wakati watu wanalia na ongezeko la gharama za kutoa makontena kutoka bandari ya Malindi kwenda kile kinachoitwa bandari kavu (ICD) ya Maruhubi, sasa Serikali inasema ili kupunguza msongamano, makontena yapelekwe bandari kavu (ICD) ya Fumba.

Si siri tena sasa ni nani anayeendesha bandari ya Fumba ambao ndiyo watakuwa wanufaika wa mpango huu. Lakini pia swali linaloulizwa ni gharama zipi zitaongezeka kulipia usafirishaji wa makontena kuyapeleka Fumba na baada ya hapo mwenye kontena kulisafirisha kontena lake hadi kwenye ghala? Na mzigo wote huu, mwisho si unamshukia mwananchi mlaji anayenunua bidhaa?

MASLAHI YA WAFANYAKAZI:
Kwa upande wa maslahi ya wafanyakazi, hali takriban imebaki vile vile ilivyokuwa, kinyume na ahadi iliyotolewa kwamba maslahi yao yangeongezeka.

Wafanyakazi hawa wamegeuzwa kuwa watumishi wa kufanikisha maslahi ya mwekezaji asiyefanya uwekezaji huku wafanyakazi wakiachwa katika hali ngumu za maisha.

Kabla ya bandari kupewa mwekezaji, wafanyakazi walikuwa wanalipwa TSHS. 480,000 kwa mwezi, na sasa chini ya mwekezaji wanalipwa TSHS. 520,000 yaani ongezeko la TSHS. 40,000 tu huku wakiwa wanafanyishwa kazi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla.

Hali hii ni tofauti kabisa, kwa mfano, na uwekezaji wa kampuni ya DP WORLD kwenye Bandari ya Dar es Salaam ambapo umeongeza ufanisi kwa kipindi kifupi. Mizigo inayoletwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imekuwa inatoka kwa haraka na imeongeza maslahi ya wafanyakazi kwa zaidi ya asilimia 100 kutoka TSHS. 700,000 kwa mwezi hadi TSHS. 1,800,000 kwa mwezi.

ACT WAZALENDO TUNASEMAJE?
Kutokana na ukweli huu tulioueleza, ni dhahiri kwamba kile kilichoitwa uwekezaji wa kimkakati (strategic investment) kwenye Bandari ya Malindi, Zanzibar si chochote zaidi ya kashfa kubwa (major scandal) inayoonesha ni kiasi gani watu wanatumia ofisi za umma kujinufaisha.

Haya yanatendeka huku mamlaka zenye jukumu la kulinda maslahi ya Taifa na kupambana na ufisadi zikiwa kimya na badala yake kuwanyanyasa watumishi wa Serikali kwa mambo ya kipuuzi ili zionekane zinafanya kazi.

Inasikitisha zaidi tunapomuona Rais Hussein Mwinyi anatembelea masoko na eti kutoa wito kwa wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan huku akijua mwekezaji aliyempigia upatu na akamkabidhi bandari kwa kiasi kikubwa ndiye anayesababisha bei za bidhaa kupanda.

Sisi ACT Wazalendo tunataka hatua zifuatazo zichukuliwe:
1. Serikali ivunje mkataba na mwekezaji huyu aliyeshindwa kazi na aliyeshindwa kutimiza yote yaliyoahidiwa na kurudisha shughuli za uendeshaji wa bandari kwa Shirika la Bandari la Zanzibar (ZPC) wakati zikifanyika juhudi mpya, za wazi na zitakazofuata sheria zote za Zanzibar, kupata mwekezaji wa kweli na wa maana siyo tu wa kuendesha Bandari ya Malindi, Zanzibar bali atakayeweza kufanya uwekezaji wa kweli katika Bandari hiyo na huduma zinazoambatana nazo.

2. Serikali ichukue hatua za dharura na za haraka za kuhakikisha meli zote zilizopo bandarini zinapata nafasi ya kupakua mizigo na wafanyabiashara wanapata mizigo yao kwa wakati na kwa gharama nafuu ili kuwarahisishia wananchi wa Zanzibar upatikanaji wa mahitaji yao yote muhimu kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhan unaotukabili.

Mwisho kabisa, nitumie fursa hii kuwapa pole wananchi wa Zanzibar wanaopitia katika matatizo makubwa na hali ngumu za maisha zinazosababishwa na maamuzi mabaya ya walioko madarakani.

Niwaambie wavute subira ya miezi michache iliyobakia kufikia Oktoba 2025 ambapo watakuwa na Serikali mpya chini ya Rais mpya kutoka ACT Wazalendo atakayewajali na kubadilisha maisha yao kufikia kwenye ile Dira yetu ya kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika.

Imetolewa na Makamo Mwenyekiti Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar.
Ismail Jussa Ladhu
 
Back
Top Bottom