Analogia Malenga
JF-Expert Member
- Feb 24, 2012
- 5,108
- 10,191
Waokoaji nchini Kenya wameuopoa mwili wa kijana mmoja aliyekufa maji alipokuwa akijaribu kumuokoa mwananume ambaye alikuwa akiomba usaidizi alipokuwa akivuka mto uliokuwa umefurika .
Anna Nduku mwenye umri wa miaka 19 alianguka katika mto Kandisi karibu na eneo la Ongata Rongai , viungani vya mji mkuu wa Nairobi siku ya Jumanne.
Ni miongoni mwa zaidi ya watu 130 ambao wamefariki kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha tangu siku ya Jumanne.
Anna alikuwa akijibu kilio cha mwanaume aliyekuwa akining'inia katika eneo moja la daraja ambalo liikuwa likijengwa.
Mwanaume huyo aliokolewa lakini yeye akaanguka katika mto huo alipojaribu kumuokoa.
Mamake Nduku, Elizabeth Mutuku, alikuwa karibu wakati ajali hiyo ilipotokea.
''Nilimuona akijaribu kujitoa katika maji nikajaribu kumuokoa. Nilimwita Anna Anna! Nilitaka kumrushia kijiti ili kujaribu kumvuta lakini mto huo ulikuwa umejaa maji hivyo basi alikuwa akirushwa kutoka eneo moja hadi jingine kabla ya kusombwa na maji hayo''.
Mto huo ulikuwa umefurika kutokana na mvua kubwa inayonyesha ambayo ilianza siku ya Jumatatu.