Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Christina Mnzava, amepongeza Jeshi la Magereza kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya Jeshi hilo katika ujenzi wa Hospitali Kuu ya Jeshi la Magereza Ukonga pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za afya katika zahanati za Magereza za Ukonga na Segerea.
Dkt. Mnzava alitoa pongezi hizo tarehe 16 Februari 2025 alipokuwa akiiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, ikiwa imeambatana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, kutembelea na kukagua huduma za afya zinazotolewa katika hospitali na zahanati za Jeshi la Magereza jijini Dar es Salaam.
"Tumetembelea Hospitali Kuu ya Jeshi la Magereza Ukonga, ambapo asilimia 90 ya majengo na huduma zinazotolewa zinatokana na vyanzo vya mapato vya ndani vya Jeshi la Magereza. Mnasaidia serikali kupunguza gharama za matibabu kwa watumishi, askari, na raia wanaozunguka maeneo haya na kupata huduma hapa," alisema Dkt. Mnzava.
Aidha, kamati hiyo ilitembelea Kliniki ya Waraibu wa Dawa za Kulevya katika Zahanati ya Gereza la Segerea, ambapo Dkt. Mnzava alitoa wito kwa Jeshi hilo kuendeleza programu maalum ya kuwawezesha waraibu hao kupata ujuzi baada ya kumaliza dozi ili kuwanusuru wasirudi tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, alisema hospitali na zahanati za Jeshi la Magereza, pamoja na kuhudumia watumishi, wafungwa, na mahabusu, zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanaoishi maeneo jirani kwa kutoa huduma za afya.
Bashungwa aliongeza kuwa kutokana na wananchi wengi kuhudumiwa katika hospitali na zahanati hizo, Wizara ya Mambo ya Ndani itashirikiana na Wizara ya Afya ili kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Vilevile, Bashungwa alisema Jeshi la Magereza, kwa kushirikiana na VETA, litaangalia uwezekano wa kuwapatia ujuzi na mafunzo ya ufundi stadi waraibu wa dawa za kulevya kwa kuwaunganisha katika mpango maalum unaoendelea wa kuwapatia wafungwa ujuzi wakiwa gerezani.
Awali, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Katungu, alisema Jeshi la Magereza linaendelea kuboresha huduma za afya na tiba kwa wafungwa, mahabusu, watumishi na familia zao, pamoja na wananchi wa maeneo ya karibu na vituo hivyo kwa kutoa huduma bora za afya.