Magwiji wa Tiba Radiolojia wakutana Muhimbili kujadili kuongeza wigo wa huduma hiyo nchini

Magwiji wa Tiba Radiolojia wakutana Muhimbili kujadili kuongeza wigo wa huduma hiyo nchini

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Magwiji wa tiba radiolojia duniani ambao hutumia vifaa kama vile CT-Scan, MRI, Xray, Angiography system, Utrasound n.k kufanya uchunguzi na kutibu magonjwa mbalimbali kupitia matundu madogo, mapema wiki hii wamekutana Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutathmini hali ya utoaji huduma hiyo nchini na kujadili mbinu za kuongeza wigo wa huduma hiyo kuanzia ngazi ya hospitali zote za rufaa za kanda, kwani kwa sasa inatolewa tu kupitia hospitali ya taifa, maalum na hospitali chache za kanda.
WhatsApp Image 2024-08-18 at 13.07.33_1604b3af.jpg

WhatsApp Image 2024-08-18 at 13.07.36_f59ad6bc.jpg


Tiba radiolojia ni aina ya taaluma ya matibabu ambapo daktari bingwa mbobezi wa tiba radiolojia hutumia teknolojia ya picha (CT, Xray, Ultrasound) kumuongoza kufanya uchunguzi au tiba kupitia matundu madogo mwilini bila kufanya upasuaji mkubwa ili kuzibua mishiba ya damu iliyoziba au kusinyaa, kupunguza ukubwa wa uvimbe au vivimbe, kutibu kuvuja kwa damu (kunakosababishwa na kupasuka kwa mishipa midogo ya kwenye tumbo na utumbo), kuingiza dawa ya kutibu uvimbe wa saratani moja kwa moja kupitia mishipa ya damu inayolisha uvimbe, kuchepusha damu kwenye ini lililonyafuka na matibabu mengine mengi.

Mratibu wa Tiba Radiolojia na Tiba Mtandao kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Grace Bash amesema lengo la Serikali ni kupunguza gharama za huduma hizo kutokana na uwekezaji ilioufanya kupitia vifaa tiba na kwa kutambua umuhimu huo, wizara ina kitengo maalum kinachoratibu upatikanaji wa huduma hizo nchini ambacho kwa sasa kipo katika hatua kadhaa za utengenezaji miongozo ya huduma hiyo.
WhatsApp Image 2024-08-18 at 13.07.34_6ff5e6fd.jpg

Amesema, katika jitihada za kuongeza idadi ya wataalamu wa tiba radiolojia nchini, Serikali kupitia Mpango wa Ufadhili wa Dkt. Samia wa Huduma za Kibobezi kwa mwaka wa masomo 2024/2025 imetangaza kufadhili wataalamu waliochaguliwa katika vyuo vilivyopo ndani au nje ya nchi kwa ajili ya ubobezi wa tiba radiolojia.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema kuanzia Julai 2023 hadi Juni 2024, wagonjwa zaidi ya

2,700 wamepata huduma mbalimbali, ikiwemo kuziba mishipa inayolisha vivimbe vya kwenye kizazi kwa kutumia dawa ili kuufanya uvimbe huo kusinyaa na kuyeyuka badala ya upasuaji, kuziba mishipa ya damu iliyolika kutokana na vidonda sugu vya tumbo ambavyo humfanya mgonjwa kutapika damu, kuzibua mishipa ya damu ya miguu iliyoziba kwa wagonjwa wenye kisukari na kuwaepusha kukatwa miguu na huduma nyingine nyingi.

Ameongeza kuwa tiba radiolojia imeleta mageuzi makubwa kwa wagonjwa mbalimbali wakiwemo wa saratani kwani kupitia njia kifaa cha maalum hupelekwa moja kwa moja kupitia mishipa ya damu hadi kwenye uvimbe mahususi na kufanya matibabu hivyo kuongeza ufanisi wa hali ya juu wa tiba ukilinganisha na kuchoma sindano ambapo dawa kwanza lazima isambae mwili mzima ndipo ifike kwenye tatizo husika.

Mkutano huo wa kitaalam uliwajumuisha rais wa International Solutions kutoka Siemens Healthineers, Bw. Frank Faccini, Bw. Sebastian Ferrari, Mkuu wa Mikakati, Siemens Healthineers, ujumbe kutoka muungano wa watalaam wa tiba radiolojia (IR) ukiongozwa na Prof. Janice Newsome, Prof. Frank Minja, Dkt. Fabian Laage-Gaupp pamoja na Mkuu wa Huduma za Radiolojia Tanzania Bw. Gerald Merama, na Mratibu wa Tiba Radiolojia na Tiba Mtandao kutoka Wizara ya Afya Dkt. Grace Bash ambao kwa kauli moja wamekubaliana kuja na mpango kabambe wa mafunzo kwa watalaam kulingana na mahitaji, kuandaa miongozo husika ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hizo katika Hospitali za Rufaa za Kanda zote na badaye Hospitali za Rufaa za Mikoa.
 
Back
Top Bottom