Mitandao ya kijamii ni moja kati ya vitu vinavyoshika nafasi katika sehemu kubwa ya maisha yetu ambapo ina michango asi na chanya.Katika karne hii ya 21 tunaona ulimwengu umetekwa sana na mabadiliko mazuri ya teknolojia. Ila kwangu mimi sidhani kama mitandao ya kijamii iliyoboreshwa na teknolojia ilinisaidia.
Nakumbuka nilipokuwa sekondari mama yangu alinizawadia simu na hapo ndipo ilikua mwanzo wa mimi kuweza kunasua mitandao ya kijamii kama " instagram na facebook".Nilifurahi sana kuweza kuona mambo yanayofanyika nchi na sehemu nyingine za dunia na hapo ndipo niliweza kupata uhamasishaji wa kuiga maisha ya watu ambapo nilirubuniwa sana na mwanamitindo aitwaye" Kim Kardashian", aliteka sana moyo wangu na nikaamua kuiga yale yote aliyokuwa akiyafanya na kuyatenda.
Licha ya mimi kusoma shule za wamissionari lakini bado sikuwahi kuacha kufuatilia maovu niliyoyaona kwenye kurasa za " facebook na instagram" .Mama yangu alilalamika juu ya mabadiliko ya tabia na mwenendo wangu wa kuvaa , kuongea na hata kuishi lakini kilichomfanya asiniseme sana ni kwamba licha ya mambo yangu ya hovyo nilikuwa nafaulu na kufanya vizuri kwenye masomo na pia nilikua mtoto wa mwisho na wa kike pekee kwenye familia yetu.
Wafuasi na marafiki mitandaoni nilikua nao wengi sana na walinisifia sana kwa kuwa nilikuwa mzuri na mwenye mvuto na hii ilinipa sana kiburi kwani nilijiona mzuri kuliko wasichana wote duniani au kwa misemo ya kiswahili unaweza ukasema nilijiona kama "tausi".
Miaka ilienda kwa kasi na niliweza kuhitimu elimu yangu ya juu kwa ufaulu mkubwa na kubahatika kwenda chuo kikuu cha IFM na hapo ndipo sakata langu la maisha lilipoanzia. Hapo chuoni mimi ndiye nilijiona mrembo wa chuo, mwenye simu kali ya I phone pamoja na kuwa maarufu sana kwenye instagram hivyo basi, hamna mtu wa kuongea au kunieleza chochote kwenye maisha yangu.Niliishi ninavyotaka na kuanika mambo yangu kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa maisha yangu na mitandao ya kijamii ikaweza kunikutanisha na wanaume wengi wenye pesa na niliweza wote kutoka nao bila ya kuwa na haya wala aibu maana kwenye kamusi ya kichwa changu sijawahi kuwa na maneno" kujutia wala aibu"
Nakumbuka siku moja nilienda chuoni na kukuta watu wakinisema na kuninyooshea vidole ila sikujali wala kuona aibu maana nilikua sio muoga lakini moyo wangu ulipigwa na butwaa pale nilipoona video na picha zangu za utupu zimesambazwa kwenye kurasa yangu ya instagram. Sikujali hata niliendelea na maisha yangu kama vile sio mimi kwani nilikua na roho ya ajabu mno na wasichana wenzangu wengi walinikanya na kunionya ila niliwaangalia tu na kuendelea na mambo yangu.
Kutokana na umaarufu wa video na picha zangu za utupu kwenye mitandao ya kijamii niliweza kufahamika mpaka kwa wasanii hivyo, nikaanza kujikita na kuwa na wasanii mbalimbali . Nilishirikishwa kwenye video za miziki ya wasanii mbalimbali ambapo watu huita wasichana walioshirikishwa kwa majina ya kingereza kama " video queen au vixen" na nilipata sana ela kutokana na uzuri wangu.
Baada ya miezi kadhaa nilisimamishwa chuo kutokana na ukosefu wa nidhamu niliokuwa nao ndipo nikaamua kuanza kurandaranda mitaani maana nilidanganya familia yangu kwamba ninasoma kwa bidii na mama hakuacha kunitumia ela ya matumizi akijua nipo chuoni. Maisha yangu yalijawa na mikasa ya kujianika hovyo mitandaoni kwa kujiuza ili kupata ela . Siku zilipita na mara mwili ulianza kudhoofika na kujihisi vibaya, basi nikakata shauri ya kwenda hospitali kumuona daktari.
Hospitali nilipewa taarifa ya kuwa nina ujauzito wa miezi mitatu na pia nimeweza kupata kisonono na kaswende." Eh! mungu wanguu" nililia sana kwa majonzi na kwikwi maana niliyaharibu maisha yangu na hata mimba niliyobeba sikujua ni ya nani maana nilitoka sana na wanaume wengi zaidi ya 200, ama kweli " Majuto ni mjukuu."
Siku nikajipanga kwenda nyumbani na kuwaelezea ukweli ila niliyoyakuta huko ni simanzi isiyoweza kufutika maishani mwangu. Nilikutana na msiba na aliyefariki si mwingine bali ni mama yangu na mzazi pekee niliyebaki naye maana baba alifariki nikiwa bado mdogo sana. Nililia kwa uchungu na moyo wangu ulididimia pale ndugu waliponieleza kuwa sababu ya kifo cha mama yangu ni mimi.
Chanzo chake cha kifo ni presha na hii ni baada ya kuona video na picha zangu za utupu na kupata taarifa ya kufukuzwa chuo. Niliumia sana lakini sikuwa na chochote cha kufanya.Mara baada ya mazishi ya mama, ndugu zangu walinifukuza kwani waliniona sina maana na waliniita muuaji ikiwa mimi ndo sababu ya mama kufa. Ama kweli " Asiyesikia la mkuu huvunjika guu".
Na hapo juu ni chati inayoonyesha uongezekaji wa watu kuangalia video na picha za utupu mitandaoni, na kwa hali hii inaonyesha dhahili mmonyoko wa maadili wa watu kutokana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii hivyo basi, ili tuimarishe na kuheshimisha vizuri mitandao ya kijamii tunapaswa kutumia vizuri ili kujenga maadili mazuri na matumizi mema ya mitandao ya kijamii ili kuepuka athari kama zilizomtokea binti wa hii simulizi hapo juu.
Kutokana na simulizi fupi hapo juu napenda sana kuwashauri na kuwakanya watu hususani vijana nikiwalenga sana wasichana na mabinti wadogo kujua matumizi mazuri na mema ya mitandao ya kijamii ili waweze kutunza na kulinda utu wao na kuepuka athari zinazotokana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwani mitandao ya kijamii imeweza kusaidia watu mbalimbali na kuonyesha manufaa mengi kwenye nyanja na sekta mbalimbali kama biashara, kilimo, afya, elimu, usafiri na hata pia sanaa hivyo basi, tunapaswa kutumia mitandao ya kijamii vizuri ili kuendeleza maendeleo ya nchi yetu na uchumi wetu.
Upvote
18