SoC02 Maisha Mapya

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Jul 26, 2022
Posts
14
Reaction score
10
Hii ni novela inayohusu suala la afya hususan uzingatiaji wa maambukizi ya UKIMWI kijamii. Ni wazi kuwa wadau wanaelewa jinsi ugonjwa huu ulivyoathiri taifa hasa tangu utangazwe kwa mara ya kwanza na hayati Rais Benjamini W. Mkapa, mwaka 2000.

Inaonekana kama jamii hususan vijana hawazingatii na kuona kawaida kuhusu ugonjwa huu. Si mbaya ila ni hatari. Takwimu kuhusu maambukizi ya VVU bado si nzuri hivyo tunaona hamasa ya kuelimisha kuhusu VVU iongezwe kwa kuwa bila hivyo jamii itaona kama hakuna kitu kama VVU jambo ambalo litaendeleza wimbi la maambukizi ya VVU. Ni wazi kiwa iwapo taifa litaweza kuundoa ugonjwa huu kwa ushirikiano wa serikali na wadau basi taifa litaokoa fedha nyingi sana ambazo zitaelekezwa kwenye maendeleo ya nyanja anuwai.
Tujali afya zetu.

"Maisha ni afya.

Kwa kawaida, kijana jamali kama mimi, urefu wa futi sita na inchi nne, huwa kivutio machoni mwa wasichana wengi. Hivyo, nilikuwa nikiabiri katika makundi ya wasichana maeneo mbalimbali ya starehe. Wasichana walinichangamkia na kuniita majina mbalimbali ya furahisha na kunisifu huku kila mmoja akiniparamia ama kuwa na ashiki ya kushika kifua changu kilichotuna, na kuhiyari kuondoka nami. Mara moja moja, niliwadengulia na kuvimba kichwa. Lakini, wakati mwingine nilijihini kuondoka na mmoja ama wawili. Aliyefanikiwa kuondoka nami, alijiona mwenye bahati na pengine kujihisi mrembo zaidi mbele ya mashoga zake na kwingineko. Pamoja na hayo tashwishwi ilinikabili.

Kipindi hiki nilikuwa na umri wa miaka ishirini na moja, nikiwa na ndoto nyingi za kutimiza maishani. Kuhitimu elimu ya juu ndio ilikuwa ndoto yangu kubwa. Na sasa nilikuwa nasoma Chuo Kikuu cha Harvard, chuo ambacho watu mashuhuri duniani wamehitimu katika darajia mbalimbali. Barrack Obama na John F. Kennedy, ambao ni marais wa zamani wa Marekani, ni miongoni mwa watu mashuhuri waliohitimu katika chuo hiki kikubwa zaidi duniani. Kwa hivi, huwa najihisi faraja na wa thamani, wakati mwingine hujiona mtu muhimu zaidi ulimwenguni. Ninaamini kuwa watu wengi hasa vijana walio shule za msingi na sekondari wana ndoto ya kusoma katika chuo hiki kikubwa na mashuhuri duniani.

Punde tu, baada ya kumaliza muhula wa kwanza wa masomo nchini Marekani, nilifunga safari kurudi nyumbani, Tanzania, kwa mapumziko ya miezi mitatu. Nilipofika Uwanja wa Ndege wa Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam, nilistaajabu kutomuona mwanafamilia wa kunipokea. Niliudhika. Yamkini, sikufurahishwa na hali hiyo. Nilitafakuri kwa muda halafu nikaamua kupanda taksi kwenda moja kwa moja nyumbani, Masaki. Nyumbani, nilimkuta dada wa kazi. Alinisalimu kinyenyekevu. Halafu alinisaidia kushusha mizigo butini na kuingiza ndani. Nilimlipa dereva taksi stahiki yake. Alinishukuru kisha aliniuliza iwapo nimeridhishwa na huduma yake.

“Naam! Iwe hivyo na wengine pia!” Nilijibu.

Dereva taksi alishukuru, tukaagana.

Niliingia ndani na kufikia kujirusha sofani. Dada wa kazi alinijia pale na kunipa ufunguo wa chumba huku akinibembeleza nisiwe mpweke na kujihisi halijojo. Alinipa ujumbe ambao sikuutegemea. Lakini, niliridhishwa na ujumbe huo. Niliona yote yalistahili. Nilinyanyuka kichovu na kwenda chumbani kwangu. Nilibonyeza kitufe cha taa. Taa iliwaka, shwaa! Chumba kilikuwa nadhifu, na kitanda kilikuwa kimetandikwa vema. Nilijirusha kitandani halafu nilichukua kikaratasi kilichokuwa pale kitandani. Nilikikunjua na kuanza kukisoma:

“Mwenetu mpendwa, tumesafiri kikazi kwa siku mbili. Tunatumaini umefika salama. Tunakupenda na tunakukumbuka. Daima, furahi. Tutarudi karibuni.”

“Nami nawapenda,” nilijibu kimoyomoyo.

Muda ulikuwa saa saba usiku. Nilikuwa sihisi usingizi kwa sababu ya mabadiliko ya majira. Nilitafakuri kwa kina, ‘nifanye nini?’ Ndipo nikaamua kuchukua gari la baba, Range rovers, na kwenda disko katika klabu ya Tips iliyopo Kinondoni-Mworoko. Huko halaiki ilikuwa na shamrashamra. Huwezi ‘amini kama ilikuwa usiku wa manane. Nililipa kiingilio na kuelekea moja kwa moja kaunta. Hapa, nilimkuta msichana mmoja amekaa juu ya stuli ndefu.

“Hey sister, mambo!” Nilimsemesha.

“Safi!” Alijibu kwa bashasha.

“Sorry, waitwa nani?”

“Esther; sijui wewe?”

“Morgan.”

“Wow! Good to see you!.”

“Don’t mention it!”

Wote tuliyafurahia maongezi. Nilimwita dada aliayekuwa akihudumu pale. Alikuja haraka na kusimama kando yangu.

“Nikusaidie nini mister?” Aliniuliza.

“Niletee Heineken moja moto na, Desperado kwa ajili ya malkia hapa.” Nilijibu kwa kujiamini.

Vinywaji vililetwa. Vinywaji vilinogesha maongezi yetu. Amini, ungeona jinsi maongezi baina yetu yalivyokuwa, utadhani tulifahamiana kitambo kilichopita. Iliwashangaza waliotuona. Tulifurahi na kucheka pamoja; kugongeana glasi, kukumbatiana na mabusu. Baada ya saa tulinyanyuka na kwenda kucheza muziki. Baada ya kucheza, nilijaribu kumshawishi tuende nyumbani pamoja. Kama kawaida, bahati huwa kwangu siku zote. Alikubali bila kudengua. Punde, tuliondoka na kurejea nyumbani.

***​

Mpaka sasa nilikuwa najilinda dhidi ya VVU[1] kwa kutumia kondomu kila nilipojamiana ingawa uelewa wangu kuhusu masuala ya [2]UKIMWI haukuwa mkubwa.

Katika utamaduni wa Kimagharibi huwa kuna imani kwamba Waafrika wote wana VVU. Na haya ndio nilikuwa nayawaza bongoni mwangu wakati najamiiana na Esther. Tulipomaliza, niligundua kuwa kondomu ilipasuka wakati wa msuguano. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kunitokea. Hofu ilinishika na nikahisi kwamba nimekwisha ambukizwa VVU. Nilifadhaika. Tangu siku hiyo niliishi maisha ya mashaka.

***​

Majuma mawili yalipita tangu nikutane na Esther kimwili. Mawazo na taswira za watu wanaoishi na VVU zilikuwa zikinibugudhi kila mara. Nilihisi ni jinamizi lililoamua kufisha mwelekeo wa maisha yangu. Furaha niliipoteza, nikawa mtu mnyonge.

Haikupita muda, nilishindwa kuvumilia unyonge ambao nilizoe kuuita, ‘Maisha Duni’. Ndipo sasa, niliamua kuwasiliana na Esther kwa njia ya simu, nikimshauri na kumnasihi tuende tukapime ili tujue afya zetu. Kwangu, lilikuwa jambo jema kujua afya yangu ili kuondoa jinamizi lililonifanya niwe na mfadhaiko na msongo wa mawazo. Bahati, Esther alikuwa muelewa. Siku moja, asubuhi na mapema, tulienda kupima katika Hospitali ya Aga Khan. Tulifika tukiwa na nyuso nyongefu.

“Vipi, mnataka kufunga ndoa?” Daktari alituuliza.

“Hapana! Tunataka kujua afya zetu.” Nilijibu kwa wasiwasi.

Tulikwenda maabara na kutolewa damu kwa ajili ya vipimo. Tulipomaliza tulirudi kwa daktari na kutupa maelekezo. Daktari alitutaka tusiwe na wasiwasi. Alituambia tukakae kwa muda wa saa moja hivi tusubiri majibu ya vipimo. Tulifuata na kuzingatia maelekezo.

Namna nilivyokuwa na hofu nilifikiri tumesubiri kwa mwaka mzima. Lakini muda wote huu Esther alinipa moyo ingawa alinilaumu kwa muda fulani. Aliniambia kuwa wasiwasi niliokuwa nao ulitokana na imani kuwa yeye alikuwa malaya. Nilimkatalia ingawa moyoni nilihisi hivyo. Alizijua fikra zangu.

Daktari alirejea na majibu mkononi. Nilishtuka. Hata hivyo tulikuwa tayari kumsikiliza. Alianza kutunasihi endapo tutakuwa na VVU. Nilizidi kupatwa hofu.

“Kwa nini hatuambii majibu yetu?” Nilijiuliza kwa hasira.

Kwa kweli nilianza kumchukia daktari ghafla. Lakini, taratibu nilipoa moto, Nikaanza kumsikiliza nasaha aliyokuwa akitoa.

“Vizuri kujua afya yako. Pengine, ukiwa na VVU uanze tiba mapema. Hapaswi kuogopa endapo utakuwa nao.” Alinyamaza kwa muda na kuangalia nyuso zetu dhoofu zilizoshindwa kumtazama machoni. Ndipo akaendelea kusema, “Hadi sasa majibu yenu ni hasi!”

“Wuuh..!” Nilipumua.

Tulifurahi na kushangilia kama washindi wa vita. Tulisimama na kukumbatiana. Kisha tulishikana mikono na daktari.

“Msifurahi. Bado mpo hati hati kwa sababu inachukua majuma kadha kuonesha kama una maambukizi ya VVU. Hivi basi, mnatakiwa kurudi hapa baada ya miezi miwili, kujiridhisha. Epukeni kufanya ngono zembe.” Daktari alitunasihi baada ya kumshukuru. Alitushika mikono halafu akamalizia kusema, “Hata hivyo, nawapongeza kwa hatua mliofikia. Mungu awabariki.”



[1] Virusi Vya Ukimwi—HIV
[2] Ukosefu wa Kinga Mwilini—AIDS
 

Attachments

Upvote 1
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…