Underthesea
JF-Expert Member
- Jul 8, 2021
- 327
- 882
Manga ni riwaya picha (Kwa Kiingereza comics au graphic novels) zenye mtindo wake wa kipekee kutokea nchini Japan. Manga ni maarufu sana nchini humo kiasi kwamba kuna mamia ya maktaba zilizojaa Manga tu. Maktaba hizi huitwa Manga Kissa
Manga Kissa nyingi ziko karibu na vituo vya treni.
Maktaba hizi ni tofauti na maktaba za kawaida, kwani pamoja na kuwa na sehemu ya umma ambapo watu wanaweza kujisomea, huwa kuna vyumba kwa ajili ya kujisomea. Vyumba vingi ni vidogo sana kwa ajili ya mtu mmoja tu, ingawa vipo vichache vya kuweza kutosha watu wawili au kikundi kidogo.
Vyumba hivi vidogo vina upana sawa na sehemu ya mtu mmoja kwenye Internet Café zetu huku Bongo. Huwa zinakuwa na kompyuta zenye internet na kunakuwa na headphones. Pia kwa juu huwa pako wazi.
Kwa sasa umezuka mtindo wa watu kuishi kabisa kwenye vyumba hivi. Baadhi ya watalii wanaongia nchini Japan wanaona ni bei nafuu kulala kwenye Manga Kissa kuliko kulala hotelini.
Hata wazawa wenyewe wamefanya Manga Kissa kuwa sehemu ya kwenda kupumzikia.
Kijana mmoja alisema kuwa wanaume wenye matatizo kwenye familia zao huwa wanakimbilia kwenye Manga Kissa kwa muda.
Kuhusu malipo, Manga Kissa, unaweza kulipia kwa saa au kwa siku.
Manga Kissa huwa zina huduma za bafu. Unaenda reception, unaacha funguo, unapewa sabuni ukaoge.
Kwa mfano hiyo inayoonyeshwa kwenye interview hapo chini, kuoga kwa dakika 15 za mwanzo ni bure. Baada ya hapo Kila dakika 10 unayoongeza unalipa dola 1.
Kila baada ya mtu kuoga lazima bafu lisafishwe na mfanya usafi kabla ya mwingine kuingia. Pia ni kawaida kukuta foleni.
Watu husifia sana usafi wa watu wa Japan kwenye Manga Kissa.
Pia Sheria kubwa kwenye Manga Kissa ni ukimya. Hairuhusiwi kuongea kwa sauti.
Kijana mmoja aitwaye Hagi mwenye umri wa miaka 31 alihojiwa akasema yeye bado anaishi kwao, lakini siku za kazi huwa anaona bora alale kwenye Manga Kissa kuliko kupoteza lisaa limoja kwenda ofisini na lingine kurudi nyumbani kwa treni. Hayo masaa mawili bora afanye kazi, kwahiyo mwisho wa juma ndo anarudi nyumbani.
Hagi anasema Manga Kissa ni kimbilio kwa watu wenye misongo ya maisha. Ameishasikia watu wakija na kulia kimya kimya kwenye vyumba vyao.
Tatizo moja la Manga Kissa ni kuwa vyumba vina uwazi kwa juu. Kwahiyo ni rahisi kuambukizana magonjwa, mmoja akipata mafua wote wanaugua. Hagi aliwahi kupata "Norovirus", akaamua tu kununua vyakula na kuchukua Manga kadhaa na kujifungia kwenye kachumba kake kwa siku kadhaa.
Pia Hagi anasema kuwa watu wengi wanaona kuwa watu wanaoishi kwenye Manga Kissa ni watu wasiojiweza kiuchumi. Lakini anasema sio kweli, wengine kama yeye inawarahisishia tu maisha na wanapenda tu mtindo wa maisha ndani ya Manga Kissa, na yeye ana mpango wa kuja kumiliki Manga Kissa yake.