MAISHA: Viumbe wote tunategemeana hapa duniani

MAISHA: Viumbe wote tunategemeana hapa duniani

Hell2Heaven

Senior Member
Joined
Mar 3, 2021
Posts
173
Reaction score
465
[emoji117]Duniani hapa kila kiumbe kipo kwa ajili ya kingine, yaani uwepo wako ni muhimu kwa ajili ya uwepo wa wengine. Ukiamka ahsubuhi lazima umtafute binadamu mwenzako alipo. Siku utakapoamka na kutembea siku nzima bila kuona mtu ye yote, lazima hofu ikukamate. Unaweza ukasema hauna shida na watu na ukaishi kwa lockdown ndani ya siku kadhaa, lakini siku ikifika utawatafuta tu watu. Na siku watu wasipokuwa na shida na wewe, hapo ndo utakiona cha mtema kuni. Heshimu watu.

[emoji117]Kila mtu ni muhimu. Watoto wanaweza wakawa na kelele sana na pengine ukawachukia kwa usumbufu wao. Watapasua hiki na kuchana kile, watavunja hiki na kuharibu kile, watauliza hiki na kujibu kile, lakini wakikosekana kwenye nyumba iliyozoea kelele za watoto, ndugu utalia na kusaga meno. Wapende watoto na jivunie uwepo wao.

[emoji117]Kila mtu ni mtaji wa mwingine, kama ilivyo kwa mpiga kura na mgombea, mgonjwa na daktari, askari na mhalifu, TAKUKURU na wala rushwa, mwalimu na mwanafunzi, mzazi na mtoto, muuzaji na mnunuzi na kadhalika. Kwenye "Ecosystem" kila kiumbe ni chakula cha mwenzake. Wewe unamla yule, yule analiwa na yule, lakini wewe pia unaliwa na yule. Unafanya kazi ili upate kula na kufanikisha haja zako, ukipata pesa unampelekea yule ili upate alichonacho ambacho wewe huna, na yeye atachukua pesa zako ili apate kile ambacho hana. Kila mtu ni muhimu. Tuheshimiane.

[emoji117] Upendo haulazimishwi lakini kutegemeana ni lazima. Umasikini mbaya lakini Mungu hakupi jaribu usiloweza kulishinda. Wapo watu wabaya na wenye fitina. Watakuroga na kukuombea mabaya. Uonapo hayo usishangae. Usiwe lege lege na mwoga, kakamaa na usikubali kufa kikondoo. Hata kama hauna nguvu usikubali kuonewa. Maisha ni vita, ukishindwa sharti ufe. Fanya chochote ili uishi, na usikae kusubiri maisha yakufuate. Yatafute na ujichotee kadri ya uwezo wako, usikubali kutafutiwa maana hautapewa kiwango chako. Kusaidiwa kupo, ila nawe jisaidie. Ukikubali kushindwa maisha, kubali kufa, ila kama umepewa mikono na akili, itumie. Ndo maana wanasema "Mungu ibariki kazi ya mikono yangu" lakini mikono yako yaweza kuwa hata miguu kwa wacheza mpira au kiuno kwa makahaba. Habari za dhambi ni wewe na Mungu wako, utakapopata hukumu yako pambana na hali yako, ila cha msingi usikubali kufa kikondoo. Pambana na utaishi hakika.

[emoji117]Uvumilivu ndo kila kitu, ukitaka vya haraka jiandae kuvipoteza haraka. Fanya kazi na Mungu atakubariki kwa hilo. Kazi yo yote inayoweka chakula mezani ni kazi njema. Umasikini hauna ustaarabu, kama hujapata pesa usihangaishwe na aibu. Changamkia fursa na usiogope watu kisa unafanya kazi mbaya. Nimekwambia chochote kiletacho chakula mezani ni kazi njema, hata kama ni kupakua choo. Ukijidai mtanashati huku hauna kitu, hata umasikini wako utakuona lofa. Usikate tamaa na kataa aibu. Usijitoe ufahamu kufanya kazi fulani, we ifanye ukiwa na timamu zako zote, na hao wanaokushangaa iko siku watakuomba hela ya kula. Maisha ni yako, kwanini uyaonee aibu? Mwenye hekima na mstaarabu akusaidie bure kama hataki udhalilike, ila vya bure ni gharama, hivyo tafuta vyako. Usife kikondoo.
______________________________
 
Back
Top Bottom