ukwaju_wa_ kitambo
Senior Member
- Sep 15, 2024
- 150
- 173
Unaweza kusema sanaa bila ubunifu ni sawa sifuri, maisha ya usanii yanahitaji bunifu zenye athari chanya kwa jamii kwa lengo la kuendelea kukuza majina na kazi zao kwa ujumla.
Katika kutafuta athari hizo hupelekea baadhi ya wasanii kujitengenezea utofauti katika mambo mbalimbali, ikiwemo maisha binafsi, ya usanii na hata jinsi ambavyo wasanii hao uonekana kwenye jamii.
Wengi wanaita kulinda brandi, yaani hapo ndipo wasanii hutengeneza picha kwa jamii kuwa wao ni watu wenye maisha mazuri, wasioijua njaa, shida wala taabu. Huku picha zao zikiwa zimepambwa mbele ya magari ya kifahari, pamba kali na hata majengo ya maana.
Licha ya kufanya hayo kwa mlengo wa kukweza kazi zao, huku wengine wakiwa tayari wameingiza sokoni kazi nyingi zenye kuvuma mjini, maswali huibuka kwa mashabiki pale ambapo msanii akipatwa na matatizo, kwani baadhi yao hurudi kwa mashabiki kuomba misaada, huku wengine wakigeuka maudhui kwa mapaparazi wakieneza picha zao wakiwa wametupiwa vyombo nje kwenye nyumba za kupanga baada ya kukosa kodi.
Hapo ndipo akili za mashabiki hucheza na kugundua kuwa yapo wanayoishi mitandaoni hayana uhalisia kwenye maisha yao na badala yake baadhi yao huangukia kwenye maisha duni licha ya kuwa ngoma zao hukita kwenye spika za bei mbaya na kwenye kumbi ambazo watu huponda mali wakiamini kufa kwaja.
Pamoja na hayo inaonekana uduni wa maisha siyo tu tatizo binafsi bali ni alama ya udhaifu wa mfumo mzima kiwanda cha burudani.
Ukwaju wa kitambo
0767 542 202
#funguka