Kutokwa na majimaji meupe yasiyo na rangi wala harufu mbaya (leukorrhoea) katika sehemu za siri (ukeni) ni jambo la kawaida kwa wasichana na wanawake wenye afya. Ila majimaji hayo yakiwa mengi sana kiasi cha kuchilizika mapajani na kulowanisha kabisa nguo za ndani, hali hiyo yaweza kuwa sio ya kawaida.
Majimaji ya ukeni yanayowasha au kuwa na harufu mbaya au yaliyoganda kama maziwa ya mgando au tui la nazi yanatokana na uambukizo wa fangasi (trichomonas vaginalis) au kisonono.
Unyevunyevu sehemu za siri kwa muda mrefu unaweza kutokeza harufu mbaya kutokana na kushambuliwa na bakteria wanaokaa na kuzaliana kwenye ngozi. Harufu mbaya mara nyingi husababisha usumbufu kwa msichana mwenyewe na watu wengine anaokuwa nao karibu.
Hali kama hii inapojitokeza msichana hana budi kunawa mara kwa mara kwa maji na sabuni isiyokuwa na kemikali kali na kujikausha kwa kitambaa safi cha nguo ya pamba au karatasi laini sana (Toilet paper).
Kuvaa nguo za ndani zinazonyonya na kukausha unyevunyevu au zinazopitisha hewa na kupunguza joto sehemu za siri kama vile ngu za ndani zenye matundu madogo madogo maalumu sehemu ya mbele, ni jambo linalosaidia kupunguza athari za majimaji yanayotoka ukeni.
Ni vema kuepuka uvaaji wa nguo za ndani zinazobana sana na zile zilizotengenezwa kwa kitambaa cheusi cha nguo aina ya polyster hasa katika maeneo ya joto jingi.
Utunzaji wa nywele zinazoota sehemu ya siri pia ni muhimu katika kukabiliana na tatizo la unyevunyevu na magonjwa katika uke. Nywele zilizonyolewa kwa mkasi na kubakia fupi hurahisisha usafi na kuweka sehemu za siri katika hali ya ukavu mara baada ya kujisaidia.
Wakati wa kujisafisha baada ya kujisaidia, hasa haja kubwa, ni vema kusafisha sehemu ya mbele kwanza kabla ya kusafisha sehemu za nyuma. Hii inasaidia kuepuka kuleta bakteria toka katika njia ya haja kubwa na kuwaingiza ukeni.
Kanuni hii isipozingatiwa mara nyingi huleta athari za uambukizo na magonjwa yanayoshambulia njia ya mkojo.
Ikiwa majimaji ya ukeni yanasababisha muwasho sehemu za siri ni vema kujisafisha kwa maji ya uvuguvugu yaliyochanganywa na maji ya limao. Mchanganyiko wa maji na maji ya limao pia unaweza kutumiwa kwa njia ya kuwekwa ndani ya beseni kubwa kisha mgonjwa akae ndani yake kwa dakika 15 kutwa mara mbili, asubui na jioni kwa muda wa wiki mbili mfululizo.
Kutumia maji ya moto sana kunaweza kuleta madhara ya kuungua kwa sehemu za siri ambazo ni laini sana na zenye miishio mingi ya mishipa ya fahamu (neva).
Muwasho wa ukeni pia unaweza kutibiwa kwa dawa asilia kwa kutumia vitunguu saumu ambapo unamenya punje moja ya kitunguu saumu kwa uangalifu usiitoboe, ifunge vizuri katia kitambaa au katika bendeji iliyo safi. Nawa mikono yako iwe safi, kisha ingiza ukeni kitunguu saumu ulichofunga ndani ya kitambaa.Fanya hivyo kila siku usiku baada ya kuoga na kabla ya kulala kwa kipindi cha wiki mbili mfululizo.
Kumbuka kuondoa dawa ukeni kila asubuhi na kuweka mpya kila siku usiku.
Kunywa juice iliyotengenezwa kutokana na mchanganyiko wa karoti, kitunguu saumu, matango na majani ya kabichi au kunywa maji ya matunda kiasi cha bilauri (glasi) moja kutwa mara tatu kwa kipindi cha majuma matatu mfululizo kunaongeza nguvu na kinga ya mwili ya kupambana na fangasi wanaoleta muwasho sehemu za siri.
Hadi hapo utakuwa umejifunza namna nzuri na yenye tija kwa ajili ya kukuondolea hadha ya harufu inayotokana na majimaji ukeni ambayo kwa namna moja ama nyingine uweza kukusababishia muwasho na kushindwa kufurahia mazungumzo pindi uwapo na mashoga zako.