SoC02 Maji na uchumi wa Tanzania

SoC02 Maji na uchumi wa Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

Michael B Masasi

New Member
Joined
Aug 14, 2022
Posts
1
Reaction score
0
Maji na uchumi wa Tanzania

Maji ni unyevunyevu usio na rangi wala harufu, Na Uchumi ni jumla ya shughuli zote za binadamu zinazolenga kutosheleza mahitaji yao, Maji yana nafasi kubwa katika kujenga uchumi wa taifa kupitia mchango wake katika maisha yetu haswa katika ufanyaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Maji yanatumika kwenye sekta ya usafirishaji wa watu na mizigo kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kama vile Mwanza kwenda Kagera kupitia Ziwa Victoria, Pia hata kutoka Tanzania kwenda nchi nyinginr duniani kama vile Uganda, Somalia, Kenya, Malawi, India, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Afrika Kusini. Kwa kiasi kikubwa maji yamewezesha wafanyabiashara kusafiri na kusafirisha mizigo yao kwa gharama nafuu. Hii inatokana na Tanzania kuwa na vyanzo vingi vikubwa vya maji kama vile Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, na Bahari ya Hindi.

Maji yamewawezesha vijana wa kitanzania kujiajiri katika sekta ya uvuvi na uuzaji wa samaki, Na wengi wao wakiwa ni vijana ambao wana elimu pia ambao hawana, Uvuvi kama sekta imechangia kwa kiasi chake katika ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini, Pia usambazaji wa maji kupitia taasisi za serikali kama vile DAWASA, MWAUWASA, AUWSA na RUWASA kumeiwezesha serikali kujiongeze vyanzo vya mapato na kutoa ajira kwa wasomi ambao wangeishi bila kazi yoyote mitaani.

Lakini pia usambazaji huo unasaidia uendeshaji wa shughuli mbalimbali za wajasiriamali wakubwa na wadogo nchini.

Kupitia kilimo cha umwagiliaji,Maji yamekuza uchumi kwa kuwasaidia wakulima katika kuyaepuka madhara ya ukame, Pia kuwafanya kuweza kulima mazao yanayokomaa kwa miezi michache kama vile nyanya, vitunguu, matunda na mbogamboga viweze kulimwa katika vipindi vyote vya mwaka, Hii inafanya maji yawe yameisaidia Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa kiasi kikubwa yameleta baa la njaa kwenye nchi zenye uchumi wa chini duniani.

Shirika la Umeme Tanzania linatumia maji kuzalisha umeme unaotumiwa na Watanzania katika kazi zao ambazo zinachangia ukuaji wa uchumi, Mfano viwanda ambavyo vinatengeneza bidhaa tofauti ambazo zinauzwa ndani na nje ya Tanzania, Pia kutoa ajira za kudumu na za muda kuweza kuyatimiza mahitaji yao muhimu ya kila siku. Mabwawa yanayotumika katika uzalishaji wa umeme kutumia maji ni Mabwawa ya Mtera, Hale, Kidatu na Nyumba ya Mungu.

Sekta ya utalii nayo imenufaika kupitia maji kuifanya iongeze vivutio vya utalii nchini Tanzania, Kwani Bahari ya Hindi pamoja na kuwa kivutio cha utalii pia inayo Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Visiwa vya Zanzibar na Mafia ambavyo vinapokea wageni kutoka nchi mbalimbali duniani. Ziwa Victoria linazo Hifadhi za taifa za Kisiwa cha Rubondo na Kisiwa cha Saanane, na Ziwa Manyara lenyewe pia ni hifadhi ya Taifa ambayo ina moja kati ya vivutio adimu vilivyoandikwa na kuonyeshwa katika makala mbalimbali ambao ni Simba wanaopanda miti, Pia kwenye upande wa mito, Mto Ruaha nao umepitiwa na Hifadhi ya taifa ya Ruaha. Vivutio hivi vyote kwa ujumla wake kila kimoja hupokea wageni wengi na kusaidia katika kuongeza pato la taifa kupitia shughuli za kitalii nchini, Pia hutoa fursa ya ajira na biashara kwa watanzania waishio karibu navyo pia wasimamizi na wataalamu waliosomea mambo ya utalii nchini.

Pia maji yanatumika katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini, Kama vile Maji safi ya kunywa yatengenezwayo na Kampuni mbalimbali kama vile Azam, Cocacola, Water Com na Metl kupitia bidhaa zake kama vile Uhai, Dasani, Kilimanjaro, Afya na Masafi, Pia maji hutengeneza bidhaa nyingine kama juisi na mvinyo katika viwanda mbalimbali huku pia yakiwa na kazi ya kupiza injini na mitambo ya viwandani pamoja na magari ,Ambapo kutokana na hili maji yamefanikisha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazouzika nje ya nchi pia kutoa ajira kwa wanajamii, Mambo ambayo yanachangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Kutokana na mchango mkubwa wa maji kwenye uchumi wa Tanzania, Uhifadhi wa mazingira hasa vyanzo vya maji kama vile maziwa na mito ni moja kati ya vitu vitakavyoweza kuchangia au kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania, Mfano wavuvi wanapaswa kuachana na uvuvi haramu haswa ule wa kutumia sumu au milipuko ili kulinda usalama wa maji na ukuaji wa samaki ili ajira iwaletayo kipato iweze kusaidia mpaka vizazi vijavyo, Pia wakulima pamoja na kushauriw kutumia kilimo cha umwagiliaji bado wanapaswa kuhakikisha wanapanda mazao yao katika umbali ambao ni salama kwa ajili ya utunzaji wa vyanzo hivi vya maji.

Na mbali na utunzaji na usimamizi wa vyanzo hivi vya maji, Pia taasisi na mashirika yanayoshughulika na usambazaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini yanahitaji kuwezeshwa katika kudhibiti upotevu wa maji bila kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa, Wananchi wanapaswa kutoa taarifa pale wanapoona uharibifu wa miundombinu ya usambazaji wa maji nchini. Hii itasaidia kuongeza ufanisi wa taasisi zinazojihusisha na usambazaji wa maji, Pia serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo ndani na nje ya nchi wanaombwa kutoa misaada kwa namna mbalimbali kama vile kuongeza bajeti ya matumizi ya fedha kwenye sekta ya maji, Pia kutoa nafasi za ajira kwa wataalamu wanaotengenezwa na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi ambao kuna nafasi yao ya kutoa mchango kwenye huduma za maji nchini

By Michael Masasi
 
Upvote 0
Back
Top Bottom