Makapuku Forum

Bunge limepitisha muswada wa marekebisho ya Sheria mbalimbali namba tatu wa mwaka 2023, unaolenga kuondoa mapungufu ya utekelezaji katika sheria mbili.

Sheria hizo ni ile ya Kanda Maalumu za Uwekezaji kwa ajili ya mauzo nje ya nchi, na Sheria ya Kanda Maalumu za Kiuchumi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Feleshi ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 6, 2023 wakati akiwasilisha marekebisho ya sheria mbalimbali namba tatu za mwaka 2023.

Amesema lengo la kurekebisha sheria hizo ni kuhakikisha kuwa sheria husika zinatekelezwa na waziri mwenye dhamana na masuala husika, kwa mujibu wa hati ya mgawanyo wa majukumu ya mawaziri ambayo inatolewa na Rais.

Amesema kuwa kwa sasa sheria hizo zinamtafsiri waziri mwenye dhamana ni Waziri wa Viwanda ili hali jukumu la usimamizi wa masuala hayo limehamishiwa Ofisi ya Rais Uwekezaji na Mipango.

“Hatua hii itaondoa ulazima wa kufanya marekebisho katika sheria kila inapotokea mabadiliko katika wizara,” amesema.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Florent Kyombo, amesema kamati imeridhika na kwamba marekebisho yanayopendekezwa yatasaidia utekelezaji bora wa sheria zinazohusika.

“Kamati imekubaliana na mapendekezo ya muswada yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa kuwa yanalenga kuhakikisha sheria zinazorekebishwa zinaendana na muundo wa majukumu, kulingana na hati idhini ya mgawanyo wa majukumu,” amesema.
 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, amejitosa kushughulikia migogoro ardhi, huku akiomba ushirikiano toka kwa wabunge, na kwamba atazunguka nchi nzima lengo likiwa ni kuhakikisha migogoro hiyo inakwisha.

Silaa ametoa kauli hiyo bungeni leo Septemba 6, 2023, wakati wa majibu ya swali la nyongeza la Mbunge wa Mbomba (CCM), Condester Sichalwe, ambaye ameuliza ni lini migogoro ya ardhi itakwisha nchini.

“...Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo nawaomba wabunge wawe watulivu na watupe ushirikiano, baada ya bunge hili, kuanzia wiki ijayo tutaanza ziara nchini nzima kwa ajili ya kuangalia na kutatua migogoro ya ardhi na kuimaliza,” amesema Silaa.

Waziri huyo pia ameagiza wakuu wa mikoa kote nchini kuendelea kutatua migogoro ya ardhi kama ilivyoagizwa na Kamati ya Mawaziri nane, ili wananchi waendelee na shughuli zao.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Stela Fiyao, ameuliza Serikali ina mpango gani wa kutoa hati kwa maeneo yote ya umma katika halmashauri za Mkoa wa Songwe ili kuondoa migogoro.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gofrey Pinda, amesema katika halmashauri tano za Mkoa wa Songwe, jumla ya maeneo ya umma 1, 679 yanatumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo shule, zahanati, vituoa vya afya na hospitali
 
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewashukuru watu mbalimbali waliofanikisha mikutano ya Operesheni +255 Katiba mpya Kanda ya Serengeti yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara.

Operesheni hiyo kwa kanda ya Serengeti inayofikia mwisho leo Jumatano, Septemba 6, ilizinduliwa Agosti 26, mkoani Shinyanga kwa Mbowe na timu yake inayotumia helkopita na timu ya pili ya makamu wake-Bara, Tundu Lissu inayotumia magari.

Katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Mbowe ameandika ujumbe huo wa shukrani akisema;

“Leo, natoa shukrani zangu za dhati kwa watu wote waliowezesha mikutano yetu ya Chadema katika Mikoa ya Simiyu, Shinyanga, na Mara kuwa mafanikio makubwa. Msaada wenu usio na kifani na uaminifu wenu umetuhamasisha sana.

“Nguvu na hamasa iliyodhihirishwa na wafuasi wetu katika maeneo haya ilikuwa ya kuvutia, na inathibitisha azma yetu kwa tunu na maono yetu. Pamoja, tunajitahidi kuleta mabadiliko chanya na mustakabali bora kwa taifa letu,”ameongeza.

“Napenda kutoa shukrani za dhati kwa waandaji, wajitoleaji, wale waliotoa michango, wale waliotukirimu kwa chakula na malazi, wale waliotutia moyo, wale waliotuombea, wale waliosambaza ujumbe wetu kuwafikia watu wengi, na wote waliofanya kazi kwa bidii nyuma ya pazia kuhakikisha mikutano hii inafanikiwa kwa kishindo.

“Michango yenu kwa mafanikio yetu ni yakutukuka. Tuendelee katika safari hii pamoja, tukiungana kwa malengo yetu ya pamoja,”ameandika.

“Safari inayofuata inaweza kuwa ngumu, lakini kwa msaada wenu, naamini tunaweza kushinda vikwazo vyovyote vinavyojitokeza. Asanteni sana kutoka moyoni mwangu. Msaada wenu usio na kifani unachochea azma yetu ya kuleta mabadiliko chanya ambayo taifa letu linastahili,

“Hatua inayofuata, Nyasa Zone. Tutaonana kazini,”amenalizia

 
Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), imesema mchakato wa ununuzi wa mashine za kuchakata Mkonge (korona) kwa wakulima umefikia hatua nzuri na wakulima zaidi ya 1,000 watanufaika na mashine hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Saddy Kambona amesema hatua zote zimekamilika kilichobaki ni kuwakabidhi hati ndogo ili kukamilisha taratibu za kibenki.

“Kwa upande wa serikali umeshaagiza korona tano, lakini upande wa wakulima ambao wanataka kununua kupitia mikopo ya benki tumeshafikia mazungumzo na Benki ya NMB tayari ngazi za juu zote tunachotakiwa sisi ni kukamilisha nyaraka ikiwamo kuwapatia wakulima hati ndogo kwa ajili ya kuwasaidia taratibu za kibenki.

“Malalamiko mengi ya wakulima yalikuwa ni kukosekana kwa mashine ya uchakataji, kwa hiyo Mkonge wa wakulima umekuwa unaharibika shambani, wanachakata Mkonge mara moja wakati wanatakiwa kuchakata mara mbili kwa mwaka lakini hata hiyo mara moja yenyewe kuna wakulima Mkonge wao hauchakatwi,” amesema Kambona.

Amesema jambo hilo limeathiri vipato vya wakulima na kupunguza kasi, nguvu na mitaji ya wakulima lakini pia inaathiri takwimu za uzalishaji ndani ya nchi kwa sababu wanalo lengo la kuzalisha tani 80,000 ifikapo 2025/26 kwa mujibu wa ilani ya chama lakini kuna lile la kuzalisha tani 120,000 2025/26 kwa mujibu wa maelekezo ya serikali.
 
Bei ya mahindi katika masoko mbalimbali katika Mkoa wa Songwe imeporomoka katika kipindi cha mwezi mmoja ikilinganisha na bei zilizokuwepo mwezi Juni na Julai mwaka huu.

Irine Nahaonga, Mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Sumbaluwela, Kata ya Ihanda, wilayani Mbozi, ameiambia Mwananchi Digital kuwa amestaajabishwa nan a kushuka kwa bei ya mahindi kutoka Sh85000 hadi 66,000 kwa gunia la kilo 100.

Aidha katika kipindi cha mwezi Juni na Julai mwaka huu, mahindi yalikuwa yakiuzwa kwa bei ya kati ya Sh80, 000 na Sh84, 000 kwa gunia lenye ujazo huo.

Katika soko la mazao Mlowo, wilayani Mbozi, Tumaini Enson, amesema kushuka kwa bei hizo mwezi Agosti, kunatokana na wanunuzi kutofika, jambo lililosababisha kuwa na mahindi mengi na bei kushuka.

"Kuanzia juzi walau bei imeanza kuongezeka kidogo kutoka Sh66, 000 hadi Sh72, 000 siku ya leo, hivyo kuna nafuu kidogo,” amesema Tumaini.

Meneja wa Soko la Kimataifa la Mazao Katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Edward Silwimba, amesema sokoni kwake bei ya mahindi kwa gunia ni kati ya Sh72, 000 na Sh78, 000.

Silwimba amekiri kuwa, kukosekana kwa wanunuzi kumechangia hali hiyo japo ana matumaini kwani sasa wanunuzi wameanza kufika sokoni hapo.

Kwa upande wake Johnson Kayange, Mkazi wa Ihanda, analaumu kuyumba kwa bei ya mahindi akisema: “...kipato kupunguza sana, tukienda kuuza, tunapata fedha kidogo ukilinganisha na siku za nyuma bei zilipokuwa juu.”

Hata hivyo bado anakiri kuwa, japo bei ni ndogo, haziwezi kulinganishwa bei za kuanzia 2019 kurudi nyuma, kwani kipindi hicho, gunia la kilo 100, liliuzwa kati ya Sh36, 000 na Sh42, 000.

Kutoka Kijiji cha Itaka wilayani Mbozi, mkazi wa Kijiji hicho Aida Mwasenga, amesema wanunuzi kutoka maeneo ya mjini wanafika kijijini hapo na kununua mahindi kwa bei ndogo ya kati ya Sh54000 na 60000 kwa gunia.

Ili kupata kauli ya Serikali, Mwananchi Digital imewatafuta viongozi wakuu wa Wizara ya Kilimo, ambao ni pamoja na Waziri Hussein Bashe, naibu wake Davidi Silinde, na Katibu Mkuu Gerald Mweli, hata hivyo simu zao ziliita bila majibu.

 
Waandishi wa habari wametakiwa kupisha usikilizwaji wa shauri la makosa ya kimaadili yanayomkabili Mathew Mbaruku, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga.

Jaji anayesimamia uendeshaji wa mashauri hayo, Rose Teemba ametoa zuio hilo kwa waandishi wa habari leo Jumatano Septemba 6, 2023 kuwa shauri hilo lina mambo 'sensitive' na hivyo kuwataka wanahabari kuondoka katika kikao hicho.

"Mkutano wa leo hatutakuwa na waandishi wa habari kwa sababu kutakuwa na mambo sensitive, hivyo kama kuna waandishi naomba mtupishe mpaka baadaye, ikiwa tutaona kuna umuhimu wa kutoa briefing," amesema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu Septemba 4, 2023 na Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Sivangilwa Mwangesi, ilieleza uwepo wa kikao cha baraza hilo, katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ili kusikiliza shauri la makosa ya kimaadili kwa viongozi wawili, ambapo wananchi walikaribishwa kusikiliza.

Viongozi hao wawili wanaotuhumuiwa kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, mkoani wa Morogoro, Dk Julius Ningu, na Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.

Wakati Dk Ningu akisomewa maelezo ya makosa ya kimaadili jana Agosti 4, 2023; ambapo waandishi wa habari waliruhusiwa kusikiliza mwenendo mzima wa shauri hilo, leo ni zamu ya Mbaruku, ambapo wanahabari wamezuiwa.

Kutokana na maelezo aliyosomewa DC Ningu, anatuhumiwa kwa makosa ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka na vitisho dhidi ya watumishi wa umma alipokuwa katika ziara za ukaguzi wa miradi mbalimbali kinyume cha sheria.

Kiujumla, taarifa ya Jaji Mwangesi, imeeleza kuwa, viongozi hao wawili, wanatuhumiwa kwa ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa vifungu vya 6 na 12 vya Sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…