Raia tisa wa Marekani wameripotiwa kuuawa katika vita vinavyoendelea Israel, huku idadi ya vifo ikiripotiwa kuvuka 1,300.
Israel ilishambulia ukanda wa Gaza kwa mashambulizi ya anga leo Jumatatu, wakati ikiendelea kujibu mashambulizi ya kushtukiza ya kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas yaliyoanza Jumamosi asubuhi.
Mawaziri wa Israel wameamuru kuzingirwa kabisa kwa Ukanda wa Gaza ambao tayari umezingirwa na kukata usambazaji wa chakula, maji na umeme kwa wakazi wake takriban milioni mbili.
Shambulio la Hamas, ambalo halijawahi kushuhudiwa, ni shambulio kubwa kuwahi kushuhudiwa na Israel katika kipindi cha miaka 50.
Zaidi ya Waisraeli 700 wameuawa katika kile Hamas inachokiita Operesheni ya Mafuriko ya Al Aqsa, huku Wapalestina wasiopungua 560 wakiuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Zaidi ya raia 100 wa Israel, wanajeshi na raia wa kigeni pia wamechukuliwa mateka na Hamas, jambo ambalo limemfanya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kutangaza kuwa nchi yake iko vitani.