Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Ndanga Kata ya Mbuyuni wilayani Songwe hawana mahali pa kuishi baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko yaliyoharibu zaidi ya nyumba 100 na miundombinu ya barabara.
Mvua hizo zilizoanza Januari 30, 2024 zimesababisha adha kwa wakazi hao huku baadhi wakianza kuhamia vijiji jirani ili kuokoa maisha yao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda amesema mvua hizo zimeharibu nyumba za wakazi wa kijiji hicho na miundombinu ya barabara.
"Baada ya kupata taarifa ya mafuriko kupitia diwani tumeamua kuja kujionea wenyewe. Viongozi tuna jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanaishi mahali salama lakini tuna jukumu kubwa kuwafariji wanapokutana na changamoto hii ya mafuriko,’’ amesema Itunda ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songwe.
“Maeneo ambayo yamekumbwa na changamoto hii katika wilaya yetu ni mengi. Maeneo mengine ya miundombinu ya barabara imekumbwa na changamoto ya mafuriko, tumepita na meneja wa Tanroads mkoa ili kuhakikisha barabara zote zinapitika. Kule Mheza juzi basi lilisombwa na maji lakini tunamshukuru Mungu watu wote walikuwa wameshashuka.”
Itunda ambaye alilazimika kupanda bodaboda kilomita zaidi ya tano ili kufika katika eneo hilo baada ya gari kushindwa kupita, amesema: “Naomba niwape pole sana ndugu zangu, nimejionea mwenyewe adha na changamoto mnayokumbana nayo.
Nimewaona mama zangu wamebeba watoto na wengine wamebeba mizigo wanavyopita kwenye eneo hili kama wanaogelea kwa sababu njia zote zimejaa maji.”
Hata hivyo, ameagiza wananchi ambao bado wanaendelea kuishi katika eneo hilo kuhama ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza wakati kamati ya usalama ya wilaya hiyo ikiendelea kufanya tathimini ya athari hiyo.
Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua zinazoendea kunyesha katika Wilaya ya Songwe kuanzia Januari 30, 2024 huku maeneo mengi katika kata za Mbuyuni na Magamba yakiwa yamejaa maji.