KLHN Wire
Mbunge wa Mtera Mhe. John S. C Malecela amevunja ukimya wake wa muda mrefu na kuzungumza na waandishi leo hii kuhusu masuala mbalimbali yakitaifa hususan hali ya kisiasa ndani ya chama hicho, bungeni na katika hadhara ya Watanzania. Mzee Malecela ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM (Bara) amefanya hivyo leo nyumbani kwake na kufanya kile ambacho watu wengi walikuwa wanajiuliza msimamo wa mzee huyo katika hali ya mgongano wa kisiasa unaoendelea ndani ya CCM. Akizungumza mbele ya vyombo vichache vya habari ambavyo alivikubalia kuwepo, Mzee Malecela alijadili kwa kirefu kuhusu malumbano yanayoendelea nchini hususan kati ya wana CCM. Akionekana kuzungumzia mgongano kati ya kambi ya Mwakyembe na ile ya Rostam katika sakata la Richmond/Dowans na mjadala wa mgongano wa maslahi mzee Malecela alisema kuwa malumbano hayo ni ya kipuuzi, hayana wala ufanisi kwa taifa.
Alielezea kushangazwa kwake na malumbano hayo kati ya wana CCM kwani wanavyovyombo vya kutosha kabisa kuzungumzia tofauti zao au hoja zao kuliko wanavyofanya sasa kupitia magazetini. Alitaja baadhi ya vyombo ambavyo anaamini vingeweza kutumika kuwa ni pamoja na vikao vya chama, Bunge, na taratibu za serikali.
Mzee Malecela amesema ameamua kuzungumza kama Mjumbe wa Kudumu wa Kamati Kuu ya CCM na miongoni mwa wazee wa CCM ambao wanasauti katika chama hicho. Amesema kuwa endapo malumbano hayo yataendelea basi ataenda hatua mbele zaidi ya kuzungumza kwenye vikao vya chama akitahadharisha kuwa CCM haitosita kumtimua mtu yeyote ambaye chama kinaona haendani nacho. Alitoa mifano ya huko nyuma jinsi CCM ilivyoshughulikia uasi ndani ya CCM ambapo baadhi ya viongozi wake (wabunge) walichukuliwa hatua.
Akikumbushia maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuwa "upinzani madhubuti utatoka CCM" mzee Malecela aliwahakikishia wananchi kuwa bado CCM kina muda mrefu wa kutawala na hakuna mtu au kikundi ambacho kinaweza kutoka na kusababisha chama hicho kumeguka.
Japo alijaribu kukwepa kuzungumzia suala la kashfa ya Richmond/Dowans moja kwa moja au kumtaja mtu yeyote kwa jina Mzee Malecela alisema kuwa kuendelea kuzungumzia suala la Dowans wakati serikali, tanesco na wizara wameshatoa msimamo wao ni sawa na "kuuchapa viboko mzoga wa mbwa". Alisema kuwa kama kuna mtu yeyote mwenye jambo ambalo anataka lizungumzwe basi lizunguzwe kwenye Bunge au vikao vya chama.
Yeye naye kama alivyofanya Dr. Mwakyembe karibu wiki moja iliyopita alivilaumu baadhi ya vyombo vya habari kuwa vinatumiwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao na ameoneshwa kukerwa na ubora wa vyombo vya habari. Alionesha kutokufurahishwa na utitiri wa vyombo vya habari ambavyo vinatumia pia nafasi yao katika jamii kurushiana matusi hata yale "ya nguoni". Alisema haitoshi tu kuwa na wingi wa vyombo vya habari bali ni lazima viwe na maadili na vinavyofanya kazi kwa kanuni zinazoeleweka. Alitoa wito kwa Wizara ya Habari kuingilia kati hali hii iliyojitokeza ambayo kwa kiasi kikubwa alionesha wazi kukerwa nayo.
Alipoulizwa kuhusu mipango yake ya kisiasa ya baadaye na hasa kama ataingia tena katika kinyang'anyiro cha kugombea Urais Mzee Malecela alisema kuwa imekuwa ni utamaduni ndani ya CCM kwa Rais aliyeko madarakani kuachwa kukamilisha vipindi viwili vinavyoruhusiwa kikatiba na hivyo mpango huo kwake kwa mwakani haupo.
Hata hivyo ameonesha nia ya kuendelea kiti chake cha Jimbo la Mtera.