DOKEZO "Mamayao" wadhibitiwe kunusuru uvuvi Ziwa Victoria

DOKEZO "Mamayao" wadhibitiwe kunusuru uvuvi Ziwa Victoria

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'

Samwel Marwa

New Member
Joined
Jan 14, 2019
Posts
1
Reaction score
1
Na Samwel Marwa (Mwandishi wa Habari na Mtaalam wa Mawasiliano ya Umma).

"Naishauri serikali kuchukua hatua za pamoja na za haraka zaidi ili kukomesha vikundi hivi vya maharamia 'Mamayao' ili kulifanya Ziwa Victoria kuwa eneo salama zaidi kwa watu wote wanaojishughulisha na uvuvi."

Tanzania imebarikiwa kuwa na maeneo mengi ya uvuvi, ikiwemo Ziwa Victoria lenye ukubwa wa kilometa za mraba 68,800 huku Tanzania ikimiliki kilometa za mraba 35,088 sawa na asilimia 51 ya ziwa lote.

Aidha, maendeleo ya sekta ya uvuvi ni muhimu sana katika kuliendeleza taifa, mathalani katika mwaka 2023/2024, sekta ya uvuvi ilikua kwa asilimia 1.9 na ilichangia asilimia 1.8 ya pato la Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, bajeti ya 2024/2025 iliyowasilishwa Mei 14, 2024 bungeni jijini Dodoma na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Abdallah Ulega, ilibainisha kuwa sekta ya uvuvi imetoa ajira kwa Watanzania zaidi ya milioni 6 pamoja na ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 198,475.

Ajira hizo zimewezesha familia kupata kipato na kuongeza usalama wa chakula. Kwa kutambua umuhimu wake, serikali nchini inazidi kujitahidi kukuza sekta ya uvuvi ili iweze kuchangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa kuuza samaki na mazao ya uvuvi ndani na nje ya nchi ili kusaidia nchi kupata fedha za kigeni na kuboresha maisha ya Watanzania.

Mbali na jitihada za serikali, kwa muda mrefu sasa kumekuwepo na taarifa za matukio ya uharamia katika Ziwa Victoria ukitajwa kutekelezwa na watu wanaodaiwa kutokea nchi jirani.

Watu hawa wanatambulika kwa jina maarufu la 'Mamayao', wamekuwa wakifanya unyang'anyi wa samaki kwa wavuvi wa Kitanzania wanapovua samaki aina ya sangara. Aina hiyo ya samaki kwa sasa inasemekana kuwa na thamani kubwa na kuonekana kama dhahabu kwa wavuvi wa Ziwa Victoria.

Pengine ni kutokana na thamani ya aina hii ya samaki kuongezeka na kufanya uhitaji wake kuwa mkubwa, watu hao hutekeleza matukio hayo kwa kufanya unyang'anyi wa samaki na vifaa vingine vinavyotumiwa na wavuvi, ikiwemo mafuta yanayotumiwa kuendesha mashine za mitumbwi.
Inaelezwa kuwa maharamia hao wanapouona mtumbwi wa wavuvi kutoka Tanzania, huufuata kwa haraka huku wakiwa wamevalia mavazi yanayoashiria kuwa ni maofisa wa usalama wa mataifa jirani huku wakiwa wamejizatiti kwa silaha za moto.

Huwataka wavuvi wawapatie 'mamayao' wakimaanisha samaki wakubwa zaidi na ikitokea wakakaidi au kuchelewa kutekeleza maagizo hayo basi hufanyiwa mateso, vipigo na hata wengine kupoteza maisha au kusababishiwa ulemavu wa kudumu.

Hivyo, 'mamayao' limekuwa jina ambalo hutumiwa na wadau wa uvuvi Ziwa Victoria wakimaanisha maharamia wa sangara.

Naishauri serikali kuchukua hatua za pamoja na za haraka zaidi ili kukomesha vikundi hivi vya maharamia vilivyojizolea umaarufu ili kulifanya Ziwa Victoria kuwa eneo salama zaidi kwa watu wote wanaojishughulisha na uvuvi.

Kufanya hivyo kutafanya eneo hilo kuwa salama kwa shughuli za uvuvi na kuvutia wawekezaji kuwekeza katika sekta ya uvuvi Ziwa Victoria.

Natoa rai kwa mamlaka zinazohusika vikiwemo vyombo vya usalama pamoja na wadau wote wa uvuvi, washirikiane kikamilifu na nchi watumiaji wa Ziwa Victoria kukomesha vitendo hivyo.

Ni muhimu kuwa na vikao vya kimkakati pamoja na kufanya doria za mara kwa mara katika eneo lote la Ziwa Victoria au watumie teknolojia ili kurahisisha ufuatiliaji na udhibiti wa eneo linalomilikiwa na Tanzania ili kuinusuru sekta ya uvuvi katika eneo hilo.

Nionavyo, kuimarika kwa usalama Ziwa Victoria kutawavutia wawekezaji wazawa na wageni kuwekeza katika sekta ya uvuvi. Hata walioacha kujihusi sha na uvuvi kwa kuwahofia maharamia hao, watarejea na kuwavuta wengine ambao walikuwa hawajajiunga na shughuli hizo.

Hii itasaidia kuongeza mapato ya nchi kutokana na uvuvi wa samaki pamoja na mazao ya uvuvi kupitia tozo na kodi mbalimbali.

Ikiwa juhudi za kiusalama zitachukuliwa, hali ya usalama kwa wavuvi wa sangara itaimarika, uchumi utaongezeka na tutaweza kudhibiti mamayao katika Ziwa Victoria na kulifanya kuwa eneo salama zaidi kwa shughuli za uvuvi.

Mwandishi wa makala haya ni Mwandishi wa Habari na Mtaalam wa Mawasiliano ya Umma. Pia Makala haya yalichapishwa katika Gazeti HabariLeo Jumatano Januari 29, 2025.
 
Back
Top Bottom