SoC02 Mambo ambayo elimu haiwezi kukupa

SoC02 Mambo ambayo elimu haiwezi kukupa

Stories of Change - 2022 Competition

Diwani

JF-Expert Member
Joined
Oct 25, 2014
Posts
2,680
Reaction score
2,779
Amani iwe nanyi.

Kwa maana yake, Elimu ni mchakato mzima wa kuhamisha ama kufundisha ujuzi, maarifa, taarifa za msingi na utamaduni kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine.

Tangu kuanza kwa mapinduzi ya pili ya viwanda, miaka ya 1850s, Mchakato huu umepewa kipaumbele na familia na hata Serikali zote za Ulimwengu huu, Elimu imegawanywa kwenye makundi makuu mawili, yaani ILIYO RASMI na ISIYO RASMI.

Bandiko letu litahusu mambo ambayo, Elimu rasmi, yaani ambayo inatambulika na mamlaka na kuidhinishwa na serikali kwa kuweka utaratibu Maalumu wa kuendesha pamoja na mitaala haitaweza kukupa ama kukuongezea; bali mambo haya hutokana na Malezi, Utamaduni na Hali mbali mbali alizowahi kupitia mtu.

Elimu uliyopata Shuleni; mathalani chuoni haiwezi kukupa juzi zifuatazo;

1. UWEZO WA KUISHI NA KUINGILIANA VIZURI NA WATU.

Uwezo wa kuingiliana "Interact" na watu mara nyingi huchagizwa na malezi ambayo mtu amepewa. Kwa mara nyingi, Elimu huja na kiburi cha usomi, yaani "Intellectual arrogance " hii ni pamoja na mtu aliyesoma anahisi hana cha kujifunza kutoka kwa wale ambao hawakupata kusomaa aidha kama yeye, ama aliyewazidi elimu au watu wa Taaluma tofauti na ile. Kuishi na watu kunahusishwa sana na tabia ya mtu kujishusha na kuthamini kidogo walicho nacho watu wengine. Kwa nafasi kubwa sana, Shule mathalani shule za bweni (Boarding Schools) zinafifisha uwezo huu wa kuchangamana na watu, hivyo mtu hupoteza uwezo wa kuthamini maisha ya watu wengine hususan wale walio nje ya Mazingira ya shuleni.
Shughuli za kijamii kama, Misiba, sherehe na mikutano, vinahitaji moyo wa kuthamini maisha ya mtu mwingine, bahati mbaya, Elimu inaweza kumfanya mtu akahisi amejitosheleza kwa kila taarifa, hivyo akawa mbali.
images%20(31).jpg


2. UWEZO WA KUISHI VIZURI NA MWENZA

Elimu haitakupa kila taarifa kuhusu mahusiano, hata kama utakuwa na ujuzi wa taaluma ya mahusiano, mambo kama ndoa, yanahitaji ukomavu wa HISIA na AKILI, mambo ambayo huwezi kupata vitabuni, haya ni mambo yanayotaka uyaishi.

Utafiti usio rasmi unaonyesha; ndoa zinazofungwa na wasomi, hazina maisha marefu tofauti na zile zinazofungwa na wenza wawili wanaotofautiana sana kwenye kiwango cha elimu. Malezi, Imani na haiba ndizo zitaamua ndoa ama mahusiano yadumu ama yasidumu, kwa kuwa elimu huja na "Intellectual arrogance" basi ni sawia na kusema "Mafahari wawili hawakai zizi moja"

images%20(32).jpg


3. NIDHAMU YA FEDHA NA UWEKEZAJI.

Kwa bahati mbaya hata wale ambao husomea masomo ya fedha na Mipango, ama benki pia wako mbali na ujuzi huu. Nidhamu ya fedha mara nyingi hujengwa na makosa ya kimatumizi afanyayo mtu, na si taarifa za vitabuni, Elimu itakuonyesha kwa nadharia namna mambo huenda, na mara nyingi Lengo lake kubwa huwa ni kukuandaa kuwa mfanya kazi, ama mtumishi wa jumuiya ama taasisi fulani, na si kuishi kile ulichojifunza. Wasomi wengi hujikuta matatani na suala la uwekezaji na nidhamu ya fedha kwa sababu, linapokuja suala la "uhakika wa fedha " kupitia mishahara basi humpa tumaini, na hata wakati mwingine, wasomi huamini Elimu ndio uwekezaji mkubwa waliofanya maishani.

images%20(33).jpg


4. HALI YA KUJIAMINI (CONFIDENCE)

Mifumo yetu ya Elimu duniani imesukwa kwenye namna ya kupima yale anayopatia mtu, na si anayokosea, na ndio mana makosa huambatanishwa na uwezo mdogo wa kufikiri, ama kutokuwa na akili, ndio maana kukosea ni aibu. Siri iliyojificha katika mafanikio ya maisha yetu ni "Makosa" Yes, Makosa ndiyo mambo yanayofanya dunia izinguke. Elimu imejenga wasomi wengi wanaogopa kuthubutu jambo kwa hofu ya kukosea, kwa sababu walifundishwa kupatia, na Kupatia ndio kufaulu, ni nani hasa atakaye kufeli? Kimsingi hakuna, ila sasa, kufeli ndio kujua kwa kutokea, kwa sababu kufeli kunaashiria kwamba mtu alijaribu. Wazungu husema "Failure is not the opposite of Success, it is the part" ili ufanikiwe, hatua moja ni kufeli, roho ya uthubutu haifundishwi shuleni.
images%20(34).jpg


5. ELIMU HAIPANDIKIZI AKILI NA HEKIMA

Akili, kwa maana ya "Intelligence" haitokani ma Elimu, ila, elimu husaidia binadamu kutambua akili yake, ila kila mtu anayo. "Education is not intelligence". Akili huonekana sana katika maamuzi, sio katika mambo kama uchambuzi, nini mtu anaamua hutokana na uwezo asilia alionao au kwa sababu za kimazingira.

Hekima; kwa namna moja hakima huakisiwa na maamuzi pia, hekima ni ubora wa maamuzi afanyayo mtu, ama ubora wa namna mtu afikiriavyo. Elimu itakusaidia kutafuta maamuzi yenye ubora/busara, lakini mara myingi Busara hutokana ma uzoefu ambao mtu kapitia..

6. UTAMBUZI BINAFSI (SELF DETERMINATION)

Katika moja kati ya vibao vyake vilivyo rindima mwishoni mwa muongo wa kwanza wa miaka ya 2000, Kanye Omar West (Ye) kwenye wimbo wa "Good Morning" kuna mstari anasema "Some people graduated but be still stupid", ndio, wahitimu wengine ni wapumbavu, hapa alimaanisha, si kila muhitimu anajua nafasi yake ama anajielewa, kwa mantiki hiyo basi, tumeona wahitimu wengi mtaani wakiwa katika hali ya kutojitambua, aidha kwa kufanya mambo yasiyo akisi usomi wao, ikiwamo Umalaya, Ulevi uliopindukia, Utumwa wa Kifikra, uvivu, kushindwa kuhoji, kutoweza kuchanganua jambo linalomuhusu na mengineyo.
images%20(35).jpg



NINI KIFANYIKE?

Ikiwa Umeelimika kwa kiwango fulani, mathalani Shahada; zingatia yafuatayo.

1. Linapokuja suala la maisha binafsi, weka madaha ya elimu na vyeti pembeni; fanya lile litakalokusitiri wewe na maisha yako, aibu, majigambo na uvivu vina nafasi kubwa ya kukufanya kuwa masikini ambayo kimsingi ni fedheha, hususan kwa mtu msomi mithili yako.


2. Wasililize sana uliowazidi kuliko waliokuzidi kielimu; kupitia kundi la watu kama hawa, kuna nafasi ya kujifunza mengi, kwa sababu "Mtazamaji huona fursa ya ushindi kuliko mchezaji" mara nyingi anachozungumza yule uliyemzidi ni yale ambayo angefanya kama angekuwa wewe; chukua hayo yawe sehemu ya maisha yako.


3. Kubali kujishusha panapostahili; Kwenye kijitabu chake cha "Searching for God" bwana Alister McGrath anasema "Watu hupenda kwenda juu ikiwa kama kuna chochote zaidi ya angahewa tu hakuna kitu kule, kila kitu kipo chini, hivyi shuka chini"


4. Hudhuria na jichanganye kwenye shughuli za kijamii; tunaishi kwenye jumuiya za kijamaa, hivyo, fursa kubwa ni pamoja na kuishi na watu vizuri kwa kuhudhuria misiba, sherehe, tafrija na shughuli nyinginezo. Kuwa sehemu yazo.

5. Heshimu watu bila kuzingatia kipato, hadhi, muonekano ama kiwango cha elimu yake. Hii itakuongezea thamani, kwa sababu heshima inatabia ya kurudi kwa anayeitoa.

Kwa kusema hayo, niwatakie wakati mwema.

Amani iwe nanyi.

Nawasilisha.

Diwani D.A


(Picha kwa udhamini wa mtandao)
 
Upvote 8
Shukrani ndg muandishi kazi nzuri sana endelea kutuelimisha sababu ni kweli tunaelimika.
 
Back
Top Bottom