SoC01 Mambo kumi muhimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu

SoC01 Mambo kumi muhimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Mar 13, 2013
Posts
5
Reaction score
5
Habari Vijana wa Tanzania, kokote mlipo Duniani! Nina furaha kubwa kupata fursa hii kuandika ujumbe huu kwenu. Hii ni kuhusu Elimu ya Juu na Maisha Halisi. Kama niwashaurivyo ninyi, nami pia najishauri!

1. Elimu ni msingi wa maisha. Hili ni jambo muhimu sana tukalijua na tukatambua ni kwanini. Lengo kubwa la sisi kuwa wanafunzi wa fani mbalimbali ni kutengeneza msingi ili tuweze kujenga maisha yetu.

Kwa msemo huu, ni maana kwamba elimu ni nyenzo mojawapo ya kutupa mwanga wa kufika sehemu. Kwa kusema hivyo ninamaanisha kwamba elimu si kila kitu, bali ni nyenzo tu! Inawezekana ukasoma mambo yanayohusu uhandisi wa majengo lakini ukajikuta umekuwa meneja wa mgahawa.

Unaweza ukasomea fani ya mambo ya biashara ila ukajikuta umeingia jeshini ukipiga kwata kila siku! Hayo yote yanawezekana na ukajiuliza kwanini ulisomea uhandisi lakini upo kwenye umeneja. Hapo ndipo inabidi utambue kwamba Elimu uliyoisoma ni nyenzo tu na itabidi ujue jinsi ya kuitumia ili ifanikishe ujenzi wa nyumba nzima. Kumbuka kuwa msingi mbaya katika maisha kutaiporomosha nyumba unayoijenga.

2. Mfumo wa Elimu yetu si rafiki ambao unaweza kuturuhusu sisi kufanya mambo mengine kama vile ya kutuingizia kipato, ila Ukweli ni kwamba bado hautufungi kujifunza vitu zaidi ya fani tunazosoma au kuwa sehemu ya wafanyakazi wasio rasmi.

Kwa kusema hili, ninamaanisha kuwa hudhuria matamasha ya kukujenga na kukufurahisha; fanya bidii katika kutengeneza mifumo saidizi ambayo itakufanya hata mara baada ya kumaliza chuo utapata nafasi ya kujiendeleza au kupata sehemu ya kujishikiza mahala popote, fanya biashara halali isiyovunja sheria za nchi.

Jihudhurishe katika midahalo ya kimaendeleo, kiuchumi, ukuaji wa teknolojia na sayansi kwani midahalo hii itakupa mwanga kuhusu ni nini kinachotokea duniani katika uhalisia wenyewe. Kwani ni kweli kuwa elimu na mitaala na vitabu tunavyovisoma wengi haitupi hali na picha halisi ya ukuaji wa dunia yetu katika mambo yote. Hivyo, "Jishughulishe, ukibweteka mwisho wa Siku utarudisha mpira kwa golikipa."

3. Katika elimu, usiendekeze starehe zaidi. Kuwa na kipimo sahihi katika kila unachokifanya (iwe katika masomo au starehe). Maisha yako yanategemeana kwa namna moja ama nyingine. Ukizidisha upande mmoja unaua upande mwingine. Jiandae, jikabili na jitunze katika mambo yote.

Huwezi ukazidisha kitu kimoja na kukisahau kingine kwa maana kila kitu kina nafasi yake. Jua jinsi ya kuikabili starehe yako unayoihusudu sana ili kufanya kila kitu kiwe katika mlinganyo stahiki ambao hautakufanya upoteze malengo yako! Inabidi ujue kuwa leo na kesho zinategemeana kwa asilimia kubwa sana.

4. Kundi ulilokuwa nalo chuoni, kwa asilimia kubwa linakusahilisha wewe kwa maisha yako hata baada ya chuo. Hivyo hakikisha unakuwa na kundi ambalo linakujenga, linakupa motisha ya kwenda mbele, linakuonya na kukusikiliza.

Kama unataka kutengeneza umoja katika kazi, kundi ulilokuwa nalo linakutafsiri mbele ya jamii ni nini hasa utakachokijenga maishani mwako. Kuna msemo wa kiingereza unaosema, "You choose your business partner in college." Vile vile tambua kuwa, unapoenda njia moja na kipofu ilihali na wewe ni kipofu lazima utumbukie shimoni.

5. Usiogope kufeli katika masomo, ogopa kuwa na hofu ya kutofikia malengo yako. Ni kweli kuwa unapokuwa chuo, moja kati ya vitu vya msingi ni kufaulu masomo. Ila ukweli ni kwamba wengi wanapofika chuo ndipo wanapoweza kujipambanua ni nini wanachotaka- yaani malengo wanayotaka kuyafikia.

Hivyo wengi wanahofu ya kufeli katika masomo kuliko kufeli katika malengo yao. Tambua kuwa kufaulu masomo bila kuwa na malengo au kutofikia malengo yako ni sawa na kulipa nauli ya ndege kubwa halafu ukashindwa kusafiri kisa umekosa nauli ya kukutoa nyumbani mpaka uwanja wa ndege.

Yatafakari malengo yako na pia liangalie jambo unalolifanya chuoni kama kweli vinaendana na kama haviendani ni kheri ukatafuta njia mbadala ya kuyafikia malengo yako. "Usihofu katika jambo lolote, hofu ni kifo cha mtu aliyekosa maarifa."

6. "Fanya maamuzi sahihi, si kila jambo linawezekana kwa wakati ule ule." Maisha yako chuoni si zaidi ya miaka mitano (yamkini kuna wengine wanaosoma zaidi ya miaka hiyo). Hivyo tambua kuwa unapokuwa mwanafunzi wa chuo si kila jambo au wazo linalokuja katika akili yako ulipaparikie.

Fanya uchambuzi yakinifu, jiridhishe, jisadikishe na upange kwa usahihi kila jambo unalolifanya. Na pia usitende jambo kwa sababu umeambiwa na mtu fulani ulifanye. Kumbuka kuwa mwisho wa siku kila jambo unalolifanya litakurudishia majibu chanya au hasi.

Unaweza ukapata wazo la biashara, jiulize kama ni wazo sahihi kwa wewe kulifanya. Tambua kuwa haya ni maisha yako unayoyajenga kwa ajili yako na kizazi chako. Lakini pamoja na hayo yote, usiogope kuchukua au kukamata fursa pale inapojitokeza.

7. Jifunze zaidi kuhusu akiba, tafuta vyanzo vya mapato. Hata ukifanikiwa kuweka kiasi kidogo cha pesa, kitakusaidia katika siku ambazo una uhitaji zaidi ya leo. Wengi wa wanafunzi wa chuo ni wafujaji wazuri zaidi ya kuwa wawekezaji. Simaanishi kuwa hautakiwi kuwa na matumizi mengi, kuwa na matumizi yenye tija na kiasi kidogo utakachoweza kukiweka akiba, weka katika 'Fixed Deposit' na kitaweza kukusaidia pale utakapohitaji zaidi.

Kwa maana mkopo ulio nao leo, kesho unaweza usiwepo; msaada wa kiuchumi unaoufaidi leo kesho utaisha, je utafanya nini iwapo ulitumia vyote na hukujua kuwekeza. Kuwa mjasiriamali wa pesa zako, zitengenezee namna ambayo zitakuheshimu na hazitakufanya uwe na mihemko katika kuzitumia.

8. "Cheti kizuri sio kufanikiwa katika maisha." Sikuvunji moyo unayetafuta kuwa mwanafunzi bora au kuwa na cheti cha 'first class' au 'highest GPA’, bali ni kukujulisha kuwa 'utashi katika mafunzo ya vitendo ni jambo ambalo uchumi wa karne ya ishirini na moja inahitaji.' Jitahidi ujue soko lako linahitaji nini na sio kuwa na matokeo mazuri katika maandishi ila ubovu katika vitendo.

Iwapo itatokea hivyo, ni wazi kuwa unaishusha hadhi yako, hadhi ya elimu yako na hadhi ya mahali kote ulipopitia. Ofisi za siku hizi, ziwe za Uhasibu au Uhandisi, sio za kujizungusha kwenye kiti cha ofisi, bali ni za vitendo na kulielewa soko linalokuzunguka.

9. Usimdharau mtu yeyote kwa muonekano wake, au udhaifu wake katika vipindi kadhaa, usiwe mpiga umbea kwa kujiaminisha kuwa wewe ni bora zaidi, au wewe ni mwenye uwezo zaidi ya wengine. Na usipende kuwasema wengine kwa kuwalinganisha na mafanikio uliyoyafikia au kwa kufaulu kwako katika masomo au jambo lolote. Kwa maana ni hakika kuwa unajua ni wapi mtu atokapo, ila hujui aendako.

Kama una shaka na mtu yeyote kuhusu mwenendo wake, msahihishe kwa maana hayo ni maisha ya muda mfupi tu, yamkini utakutana na mtu huyu akiwa juu yako. Wazungu wanasema, "Humble yourself, never exalt yourself above anyone else. Just let others exalt you. For the world is still spinning."

10. "Bado hujachelewa." Hata kama umebakiza muda mfupi kumaliza masomo yako, tengeneza sehemu ya kutokea. Wengi wamekosea ila walipojua ni wapi walikosea, waliinuka na kujua wapi wanaanzia. Tafuta njia sahihi ili upate kile ambacho unakitaka.

Kwa vyovyote vile ulivyo, usijaribu kujilinganisha na mtu mwingine halafu wewe ukajiona mjinga, unachotakiwa ujue ni kwamba umechelewa tu na bado una nafasi ya kusimama ili kufikia malengo yako. Jitahidi, simama na hata ukianguka, jua jinsi ya kusimama.

AHSANTE
Nikutakie wakati mzuri wa masomo yako!
Wako katika ujenzi wa Jamii Bora

Jovitus Justus
 
Upvote 4
Back
Top Bottom