Mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuingia kwenye ubia wa biashara

Makirita Amani

JF-Expert Member
Joined
Jun 6, 2012
Posts
1,915
Reaction score
3,422
Kwenye makala iliyopita tuliona jinsi ilivyo muhimu kufanya biashara kwa ubia. Tuliona faida tano za kufanya biashara kwa ubia na jinsi ambavyo unaweza kunufaika nao.

Katika makala ile pia tuliona tahadhari ambayo ni ubia unaweza kuwa chanzo cha biashara kufa pia. Kama hutakuwa makini kwa kuchagua mtu mzuri wa kuingia naye kwenye ubia wa biashara, basi utakuwa unajiandaa kushindwa kwenye biashara.

Kwenye makala hii ya leo utapata nafasi ya kujifunza mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuingia kwenye ubia wa biashara.

Hii ni muhimu sana hivyo soma na fanyia kazi kwa sababu usipofanya hivyo utakuja kujuta baadae pale ambapo utajikuta kwenye matatizo makubwa.

Angalia maono na malengo ya mbali.
Kabla hujaingia kwenye ubia wa biashara na mtu au watu wengine, ni vyema kujua maono yao na hata malengo yao ya mbali. Angalia kama vitu hivi vinaendana na wewe na kama mtaweza kwenda pamoja.
Wewe unaweza kuwa na maono ya kukuza biashara iwe ya kitaifa na kimataifa wakati wenzako wanataka wapate tu fedha ya kuendesha maisha. Kwa maono haya tofauti hamtaweza kwenda pamoja.

Chagua watu ambao wana maono na malengo makubwa ya baadae, kwa watu wa aina hii mtasukumana ili kuweza kufikia malengo hayo. Ila kama watu watakuwa na malengo madogo na wewe unayo makubwa, watakurudisha nyuma.

Angalia ujuzi na uzoefu.
Kama mnataka ubia wenu uweze kudumu na kuleta thamani kubwa kwenye biashara, basi ni vizuri mkawa na ujuzi na uzoefu tofauti tofauti kwenye maeneo ya biashara yenu. Kama wote mna ujuzi wa aina moja, maeneo mengine ya biashara yatakosa usimamizi mzuri na hili litawarudisha nyuma.

Unapochagua watu wa kufanya nao biashara, hakikisha kuna kitu cha tofauti wanakileta kwenye biashara hiyo ili iweze kufanya vizuri.

Angalia mtu anayeweza kujitoa.
Kuendesha biashara sio kazi rahisi, inahitaji kujitoa sana na hata wakati mwingine mtu kujisukuma kwenda hatua ya ziada. Unapochagua wabia wa kufanya nao biashara zingatia sana swala hili.

Kama mtu ana majukumu mengi tayari, atakuwa kikwazo kwenye kujitoa kwenye biashara hiyo. Kama mtu anapenda kutoa sababu kwa nini anashindwa kukamilisha majukumu yake atakuwa kikwazo kwenye kuweza kusonga mbele.

Angalia mtu au watu ambao wapo tayari kufanya chochote kilichopo ndani ya uwezo wao kuhakikisha biashara unastawi.

Angalia maadili.
Maadili ni muhimu sana kwenye biashara. Japo wengi hawazingatii hili, lakini hakuna biashara inayoweza kukua na kufanikiwa kama wamiliki hawana maadili mazuri. Na chanzo cha biashara nyingi kufa ni kukosekana kwa maadili baina ya waendeshaji wa biashara.

Unapoamua kuingia kwenye biashara na mtu au watu wengine, zingatia mambo haya matatu kwenye maadili; uaminifu, uadilifu na nidhamu binafsi.

Kama mtu anakosa kimoja tu kati ya hivyo, ni hatari sana kwenye biashara yenu. Biashara yoyote inajengwa kwa misingi ya uaminifu. Ni vyema kuhakikisha nyinyi wamiliki mna uaminifu kwenu wenyewe na kwa wateja pia.

Angalia uwezo wa kifedha.
Katika kuchagua mbia au wabia wa biashara, angalia watu ambao wako vizuri kifedha, yaani hawana matatizo ya fedha. Tunaposema wapo vizuri kifedha hatumaanishi awe tajiri ila aweze kuwa na usimamizi mzuri wa fedha zake binafsi ili asiingilie shughuli muhimu za kibiashara.

Kama mtu kusimamia fedha zake binafsi kunamshinda, ana madeni mengi na hawezi kupangilia matumizi mazuri ya fedha zake binafsi, ni hatari kuingia naye kwenye biashara. Kwani ataendelea na tabia zake kwenye fedha na itakuwa tatizo kubwa kwenye biashara yenu.

Ni muhimu sana kujiridhisha na tabia za wale unaotaka kuingia nao kwenye ubia kabla hata hamjaanza biashara. Kama una wasiwasi wowote ni vyema usiendelee na ubia huo. Kama mtu tabia zake hazikuridhishi sasa usijidanganye kwamba baadae atabadilika.

Pata mtu sahihi wa kuingia nae kwenye biashara na mtaendesha biashara yenye mafanikio makubwa.
Kwa ushauri na kupata mwongozo wa biashara andika email kwenda biashara@napendabiashara.co.tz au piga simu 0713 666 445.

PENDA BIASHARA, JIFUNZE BIASHARA.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…