SoC02 "Mambo nchini Lwambo"

Stories of Change - 2022 Competition

Msafiri Haule

Member
Joined
Aug 6, 2018
Posts
28
Reaction score
18
Mwendapole hajikwai ndivyo wanenavyo wahenga, salamu kwa wasomaji ndiyo sifa yangu njema.

Jioni kabla ya jua kuacha kutuandama, wanakoo hujikusanya barazani kwa mzee Ndama. Watoto hujaa mapema hasa tangu hadithi ya Malkia Lidya kuanza kusemwa. Siku hiyo Bibi ajulikanaye kwa jina la Msenga alikuwa zamu kusawili na kuhariri yote yaliyosemwa juu ya Malkia mwenye enzi katika nchi ya Lwambo.

Bibi Msenga alianza kwa kusema, “Hadithi- hadithi” kwasauti ya kiimbo nao wasikilizaji barazani kwa Mzee Ndama wakasema; “Hadithi njoo uongo njoo ukweli utamu kolea”. Kwasauti yenye usiri wa karipio na onyo Bibi Msenga alisihi kwa kusema “linitokalo ni hariri za Malkia Lidya na siyo hadithi za mtalii..hivyo, ninenayo ni Ukweli Utamu Kolea na Si Uongo Utamu Kolea”, wakaitikia kwa kutahayari.

Kwa heshima iliyotangulizwa na hekima, Bibi Msenga alianza kusema;
Hapo enzi paliketiwa na Mfalme aliyesifika kwa kukosa ukame kuzaa watoto wakiume. Mfalme huyo hakuwahi thamini penzi mujarabu la mke wa kwanza. Bibiye Zuhura, alipokea heshima yenye dharau kwa kukosa kumletea mfalme taadhima, yaani mtoto. Majuto ya mwanamke kukosa mtoto ni zaidi ya mjukuu, alijikongoja bila mfanikio ili kushinda mwaliko wa mumewe apate kumtahabaruku. Si yote waliyonena wahenga ni sahihi, kwa maana, Kisicho ridhiki kililika kwa mfalme.

Tazama, jioni siku ya mwisho wa juma, mfalme alijikuta akihitaji joto la Zuhura, hakika, usitusi mamba ungali bado kuvuka mto, Zuhura alishika Mimba aliyojifungua kabla hata ya miezi tisa kusawili. Mfalme alijaaliwa utajiri wa watoto nane wanamume, isivyo bahati kwa Malkia Zuhura alipata binti njiti na alikosa kujiamini kumweleza mumewe kwakuwa heshima kwa mke wa mfalme ilikuwa kumzalia mtoto mwanamume.

Kwa kadili ya desturi za mfalme, Zuhura na Mwanaye hakutakiwa kuendelea kuishi na mtoto Binti katika hema la kifalme, hivyo alilazimika kuondoka na damu ya kifalme hadi visiwa jirani na nchi ya mbali. Kwa unjiti wa kiumbe kile, Zuhura alikibatiza jina “Lidya”, kama sehemu ya kumbukumbu kwa marehemu Dada ya mfalme ambaye Zuhura alifurahi sana uwepo wake angali hai kwakuwa walipendana. Lidya alipokea tiba za kiasili naye akakua kimwili bila ya kuchelewa akili.

Gharika la homa za ngozi hazikutosha kuacha kutoa chozi familia ya kifalme. Isivyo bahati, dhiki hiyo iliondoka na vijana wanne wa mfamle, watatu mke wa pili, mmoja mke wa tatu. Nchi ya Lwambo ilighubikwa na jinamizi la vifo si tu kwa wazee hata vijana na kinamama. Kadhalika mke wa pili wa mfalme hakufua dafu, hata kile cha kujivuna yaani yule mtoto mmoja naye kwa uchungu wa kumlilia mamaye moyo wake ulishindwa vumilia, akakata roho.

Ni muongo mmoja tangu Zuhura aondoke hemani kwa mfalme, lakini mfalme alikumbuka “damu kuwa nzito kuliko maji”, alitamani kumwona Zuhura na mwanaye wakimpa faraja baada ya kugubikwa na maswaibu ila hawakuwepo. Alitamani apate tulizo la dhiki iliyomkumba alizidishiwa karaha. Wahenga waliwahi sema, Mwaka wa dhiki daima majanga hayaishi, vita vilijongea katikati ya mji, wana wa mfalme walikuwa vinara kutetea taifa lao ili hata baadae wawapo enzini kuaminiwa uzalendo wao kwa taifa.

Kwa jinsi miungu ilivyomcharukia mfalme, hata wale watoto watatu wakapungukiwa na ndugu mmoja vitani, na ndipo idadi yao kubakia wawili.

Raia wachache walisalimika na vita vikatulia. Nguvu kazi isiyo na tija katika kuleta ziada, ikarejea kazini. Kwa kukosa maarifa yenye maono watu hawaachi kujizuia, Nchi ya Lwambo ilighubikwa na wapenda starehe si kazi, wapenda sifa hata zisizo na tija, viongozi wasio na ilimu, rasilimali zisizoleta mali na sheria zisizo fananishwa na msumeno.

Lidya na Mama yake (Zuhura), hawakupatwa na ghasia za maradhi hata vita, walipokea msaada kutoka kwa wadau wakaishi kwa kusahau yote ya awali. Akiwa na umri wa miaka 15, Lidya akazidi nawili kiakili, mawazo yake yalisawili hata eneo kubwa la nchi. Alionekana binti mwenye asili ya familia ya wenye akili, hakutaka kujisifu kwa kejeli kwakuwa alitambua yeye si kitu bila ya jumuiya watu.

Akiwa na umri wa miaka 17, jamii ya kwenye kisiwa haikuona sababu kumnyima uongozi katika safu yao ya utawala. Akawa msaidizi wa tatu wa Liwali wa eneo hilo, fikira zake katika kutafsiri desturi, sheria, matatizo na kutoa suluhu zilizidi uwezo wa Liwali, hata mwaka uliofuata wakazi wa eneo husika wakampendekeza kuwa Liwali kamili licha ya kukithiri kwa mifumo kandamizi kwa wanawake lakini haikufua dafu kumdidimiza Bibiye Lidya aliyepokea kudra za uongozi tangu angali tumboni mwa mamaye.

Wahenga hunena kuwa “aanzaye kupiga miluzi, mwishoe huimba”, ndicho kilichojiri kwa damu hii ya kifalme. Uwezo wake kufafanua na kutatua kero kongwe za wakazi wa eneo hazikumshinda. Alipendekeza uanzishaji wa "elimu yenye manufaa” kwa eneo lake. Kilimo kilipata nafuu, mifugo ikapata malisho bora, mbegu sawia na eneo, wafugaji kwa wakulima kwa sheria zilizochagizwa na uwepo wa bibiye Lidya migogoro yao ikapata pumziko la kudumu. Hiari ya Bibiye Lidya ilishinda utumwa kwa eneo husika. Malkia Zuhura akapata heshima aliyokuwa akiingojea enzi zote za ugumba, na ndipo “mvumilivu hula mbivu” ikaaminiwa.

Taaarifa juu ya umaridadi wa Lidya hazikufua dafu pasi na kumfikia Mfalme, na kwa hakika, umaridadi wa binti Lidya katika kufungua fahamu za kutatua kero za eneo lake zilimpendeza sana mfalme kiasi kutamani binti huyo kumuozesha kwa Kijana wake mmoja kati ya wawili walio salia. Kwa kukosa maono, akatuma vijakazi wake kuelekea katika visiwa vilivyo jirani na nchi ya mbali.

Ujumbe wa mfalme ulimuhitaji Bibiye Lidya kuonana ana kwa ana na mfalme wa nchi ya Lwambo. Kwa kipindi hicho, Malkia Zuhura alikuwa mbali na mwanaye, kwakuwa tayari Lidya alikuwa katika hema za Liwali mkuu ili kutatua kero za jamii kwa uharaka. Bibiye Lidya hakuwahi pia kumfahamu Baba yake, na kila alipowahi kumuuliza mamaye, aljikuta akiambiwa “palipo mimi na wewe ni furaha na amani”. Lidya aliitikia wito, na alitamani kama angelandana na familia yake yaani Mama yake na jirani.

Kwa sababu hiyo, ujumbe ulimfikia Malkia Zuhura kuwa mwanaye karidhia kuonana na Mfalme, na angefurahi kwenda na familia yake, Malkia Zuhura alilia sana kwa uchungu kuwa leo hii “jiwe alilolikataa Mwashi lageuka kuwa jiwe kuu la pembeni?" Akataka shauri na mwanaye ili amjuze kuwa wito huo ndiyo wito wa Baba yake aliyekuwa akimuulizia kila uchao.

Kwa taarifa ile, licha ya bibiye Lidya kuwa na maarifa mengi lakini hisia zilizidi maarifa kwa nyakati hizo, na kwasababu hiyo alilia kwa chozi lisilo na mwisho. Hata safari ilipokuwa ukingoni bado chozi la kurejea nyumbani halikukaa likajifuta.

Safari huwa na mwisho, ujumbe wa mfalme uligonga geti, tazama mfalme akiwa na shauku ya kumpokea Binti maridadi aliyejijengea umaarufu wa masuala ya uongozi na asijue kuwa ndiye mwanaye. Pasi na taarifa, alishikwa na butwaa kuona sura ya mkewe Malkia Zuhura ikiambatana na binti wa makamo wa miaka ishirini. Kwa kipindi cha dakika sitini, yaani saa moja, Mfalme alizimia.

Hata alipozinduka kuona uso ya Malkia Zuhura na kwakuwa vijakazi wengi hawakumtambua ikawa ngumu kumpa heshima kama mke wa Mfalme yaani Malkia wa kwanza. Mfalme akapatwa na aibu kiasi kutotamani kuona kijakazi yeyote mbele yake isipokuwa wageni wake. Alitamani kumjua binti aliyeambatana na Malkia Zuhura naye akamjuza kuwa ni Lidya, mtoto aliyesababisha yeye kufukuzwa hemani, na ndiye Liwali aliyevuma duniani kote katika hicho kisiwa. Kwa heshima kubwa Mfalme aliwapigia magoti kama ishara ya kuhitaji msamaha kwani yaliyopita si ndwele. Malkia Zuhura hakuwa na choyo, alibarikiwa siha njema, akamtaka mwanaye amwinue babaye kwakuwa mtoto hakui mbele ya mzazi, hata hivyo jamii ikiona tukio la mfalme kupiga magoti atadharauliwa.

Ujio wa ugeni ule, Licha ya nchi ya Lwambo kuwa katika taabu nyingi za kiuchumi, mfalme aliwataka vijakazi wake kuwaita watoto wake wote wawili waliobakia, ndugu jamaa na viongozi wengine, akaandaa tafrija kubwa ya kuwalaki wageni walioheshimika sana. Ndugu wakafahamiana, mipango ya kuchumbiana ikafia hapo. Wakafahamiana, wakapendana, wakasemezana, kwa hakika siku njema hazionekani asubuhi tu bali hata jioni.

Kiumri mfalme alikuwa tayari amekula chumvi nyingi, hakumudu kufanya mambo mengi kunusuru nchi dhidi ya Umasikini , Ujinga na Maradhi. Na kwa mwonekano wa jicho la mvi zenye busara aliona Binti Zuhura, mwana wa mfalme pekee anamudu kuvaa viatu kuongoza gurudumu la ustawi wa nchi ya Lwambo.

Kwa sababu ya umaarufu wa Lidya, haikuwa kazi ngumu kushawishi baraza la mawaziri kumpitisha Bibiye Lidya kuwa Malkia wa Kwanza (mkuu wa nchi) kuwahi kuongoza nchi. Licha ya Lwambo kuwa masikini kwasababu ya maradhi na vita vilivyotokea, watu wake walikuwa waelewa.

Lidya akawa Malkia, sherehe za kusimikwa kwake zilihudhuliwa na watu wengi hata wa visiwani ambao walitokwa na machozi ya furaha na huzuni ila Malkia Lidya aliwasihi wasihofu atafanya vema ili aliyoyaanzisha kule visiwani yaenziwe na yasife.

Malkia Lidya, aliwapenda wazazi wake, akatamani waishi kwa amani na furaha. Ndugu zake hawakuwahi kuwa wenye wivu naye kimadaraka, wala chuki nafsi kwakuwa wote waliitakia mema nchi yao. Hata hivyo, Malkia Lidya aliwasihi ndugu zake kwakuwa wote hutamania yaliyo heri kwa nchi yao, ni vema wakasaidia katika kutoa fikra pevu hata zile kinzani, ili tu Lwambo izidi stawi.

Akaanza kazi kwa kutengeneza mifumo isiyokandamizi kisheria hasa kwa watu wake waliokesha “wakilazwa hoi” kwakuwa aliamini penye watu kuna vitu. Hakufumba macho kuangazia mfumo wa elimu, kwakuwa aliamini ukombozi wowote huanzia katika fikra.

Alitamani wakulima wapewe kipaumbele cha kwanza katika bajeti, kwakuwa alijua kilimo ndiyo uti wa mgongo kwa nchi ya Lwambo. Alikemea mianya yote ya rushwa, kwakuwa alijua ndiyo adui mkubwa kwa haki za MAKABWELA.

Aliaminisha umma juu ya kuona thamani ya maoni yao hasa katika kustawisha maisha yao, demokrasia iliota matawi katika maeneo yote ya nchi ya Lwambo. Wana Lwambo waliweka nia katika imani zao ziwapazo majibu, wakaheshimiana bila ya kubaguana, wakaoana, watoto wakapewa kipaumbele katika vyombo vya usafiri nakadhalika, walistawisha usawa bila ubaguzi kijinsia na kwa hakika Lwambo iligubikwa na raha isiyo pambwa kwa karaha.

Malkia Lidya alimudu kuistawisha Lwambo, hata nchi nyingi ulimwenguni zilitamani kumpata kiongozi aliyependa SIASA na siyo MADARAKA, hakutaka sifa ila alipenda kujisomea kujiongezea maarifa. Alipokea ushauri hata kwa wale walimfikishia kwa siri, kwa hakika LWAMBO IMESIMAMA hali yake ni SHWARI.

Bibi Msenga alihitimisha kwa kusema, hekima na busara za kuongoza si umri wala jinsia bali ni utu uliojazwa na tunu. Ili kupata maendeleo ya kweli, ukombozi wa kifikra ni nguzo imara, “demokrasia ya kweli yenye kuamini vitu ni bora lakini bila watu hakuna vitu”, ni mbinu mbadala kuelekea maendeleo ya kweli.

Hadithi ilikwamia hapo, watoto walioketi pale barazani kwa Mzee Ndama walilengwa lengwa na machozi, kwa mapito ya malkia wakipekee kuwahi kutokea licha ya maswaibu yaliyomfika tangu kuzaliwa kwake.
 
Upvote 0
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…