Mambo Ya Kuzingatia Kabla Hujatoka Kwenye Biashara Iliyoshindwa Na Kuingia Kwenye Biashara Mpya

Mambo Ya Kuzingatia Kabla Hujatoka Kwenye Biashara Iliyoshindwa Na Kuingia Kwenye Biashara Mpya

Makirita Amani

JF-Expert Member
Joined
Jun 6, 2012
Posts
1,915
Reaction score
3,422
Sio kila biashara unayofanya itafikia mafanikio makubwa unayotarajia. Biashara inaweza kusua sua na kukusumbua sana. Na wakati mwingine biashara inaweza kwenda kwa hasara na mwishowe kufa kabisa.

Biashara inapokufa wafanyabiashara hufikiria kukufua biashara ile au kuingia kwenye biashara nyingine. Ni mawazo mazuri sana kwani hupaswi kukata tamaa. Kushindwa ni sehemu ya mafanikio ya biashara yako.
Lakini wafanyabiashara wengi hufanya kosa kubwa sana pale wanaporudi tena kwenye biashara baada ya kuondoka kwenye biashara iliyoshindwa.

Kosa kubwa wanalofanya ni kuingia kwenye biashara mpya kabla ya kutumia muda kutafakari biashara iliyoshindwa au kufa. Hivyo huingia kwenye biashara mpya wakiwa na mawazo na makosa yale ambayo waliyafanya kwenye biashara iliyopita. Hivyo hujikuta matatizo yaliyotokea kwenye biashara iliyopita ndio yanajirudia kwenye biashara hiyo mpya.

Kama wewe ni mfanyabiashara unayerudi kwenye biashara mpya, baada ya awali kufa, au upo kwenye biashara lakini unataka kuingia kwenye biashara nyingine, leo utajifunza mambo muhimu ya kuzingatia.

Yafuatayo ni mambo muhimu sana ya kuzingatia kabla hujaingia kwenye biashara mpya baada ya kushindwa kwenye biashara ya zamani;


  1. Jua chanzo cha biashara kufa.
Hakuna biashara inayokufa bila ya chanzo. Kuna kitu kilisababisha biashara yako ya kwanza kufa. Jua kitu hiki na jinsi ambavyo kilichangia biashara hiyo kufa. Jua dalili za biashara hiyo kufa zilianzaje ili wakati mwingine ujue. Pitia kila chanzo ambacho kilichangia biashara yako kufa.


  1. Jua makosa uliyofanya wewe mpaka biashara hiyo ikafa.
Hata kama utasema kwamba wewe hukuwa chanzo cha biashara kufa, jua ya kwamba umehusika sana katika kuua biashara yako. Kuna makosa ambayo uliyafanya tangu awali ambayo yalichangia biashara yako kufa. Hata kama ni mabadiliko ya sheria yamepelekea biashara yako kufa, huenda ungekuwa makini zaidi ungeweza kuchakua hatua.

Ni muhimu sana ujue mchango wako kwenye biashara kufa. Huenda hukuwa na usimamizi mzuri, huenda hukuwa makini. Huenda uliamini watu kupita kiasi, na mengine mengi. Jua udhaifu wako ulikuwa wapi ili usiupeleke kwenye biashara mpya.


  1. Jua ni kipi kingeweza kuzuia biashara ile kufa au usipate hasara kabisa.
Baada ya kujua chanzo na mchango wako kwenye kuua biashara, jua ni hatua gani kama zingechukuliwa mapema biashara ile isingekufa. Au ni hatua gani zingechukuliwa ungeweza kuondoka kwenye biashara hiyo mapema kabla ya kufikia kufa.

Kwa vyovyote vile kuna kitu kingeweza kufanyika na kikaleta mabadiliko makubwa. Hujiulizi hivi ili kujilaumu, bali unajiuliza ili kuhakikisha kwamba unajifunza na hurudii makosa uliyofanya awali.


  1. Ni somo gani unaondoka nalo kwenye biashara ile ambalo utatumia kwenye biashara yako mpya.

Werevu wanasema ukitaka kuendelea kupata matokeo unayopata sasa, endelea kufanya kile unachofanya sasa. Na wewe kama utataka kuua tena biashara mpya kama ulivyoua ya zamani, basi endelea kufanya biashara hii mpya kama ulivyokuwa unafanya ya zamani.

Ni lazima utoke na azimio kutokana na kilichotokea kwenye biashara iliyokufa ili kuhakikisha hakitokei tena kwenye biashara hii mpya.

Kushindwa kwenye biashara sio mwisho wa safari, lakini kama utashindwa kwenye biashara ya kwanza, na ukaenda kwenye biashara ya pili bila ya kutafakari umejifunza nini, utakuwa unajiandaa kushindwa tena kwenye biashara hiyo mpya. Chukua muda leo na uitafakari biashara yako iliyopita ili ujue ni yapi ya kuzingatia kwenye biashara mpya.

Kwa ushauri na mwongozo wa biashara piga simu 0713 666 445.

JIFUNZE BIASHARA, PENDA BIASHARA.
 
Nimejifunza kitu kutoka kwako ndugu, umetoa ushauri mkubwa sana
 
Back
Top Bottom