Wagonjwa wakwama porini Loliondo
Send to a friend Sunday, 20 March 2011 21:37 0diggsdigg
Mchungaji Ambilikile Mwasapile
Mussa Juma, Arusha
MAMIA ya wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, ambao walikuwa wanakwenda kupata matibabu kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapile wamekwama njiani kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jana na kuharibu barabara.
Barabara ya kwenda katika Kijiji cha Samunge aliko mchungaji huyo inayochepukia eneo la Kigongoni na Selela, Engaruka na Ngaresero, sasa haipitiki kutokana na kuharibika.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali alisema jana kwamba kuharibika kwa barabara hiyo kumesababisha mamia ya wagonjwa na jamaa zao waliokuwa wakielekea Samunge kukwama porini hivyo kukosa huduma muhimu za kijamii ikiwamo chakula na hata usalama wao. Kutokana na hali hiyo, amekiomba Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu, kuingilia kati na kufika eneo hilo kutoa msaada... Hali ni mbaya sana. Idadi ya watu sasa ni kubwa kuliko kipindi kingine chochote
Lali aliwataka viongozi wa mikoa inayopakana na wilaya yake kuweka udhibiti wa watu wanaokwenda Samunge kutokana na uharibifu huo wa miundombinu... Nawaomba wadhibiti watu hadi hawa waliokwama na waliopo Samunge watakapopungua.
Kukwama kwa wagonjwa hao, kumekuja takriban siku tatu tangu, Mchungaji Mwasapile alipoiomba Serikali kuharakisha kukarabati barabara hiyo akihofia kukatisha mawasiliano ya kumfikia.
Magari mbalimbali ya abiria yakiwapo mabasi na mengine madogo ya kukodi yamekwama kati ya Vijiji vya Engaruka na Ngaresero na hivyo kutishia afya za wagonjwa wengi.
Mmoja wa madereva waliofanikiwa kupita katika njia hiyo, Jonathan Mrema alisema Serikali isipokarabati barabara hiyo sasa, wagonjwa wengi watakwama hata kupoteza maisha.
Alisema kutokana na ubovu wa barabara hiyo na hivyo wagonjwa kukaa muda mrefu kabla ya kufika kwa mchungaji huyo, amewashuhudia wanne waliofariki dunia juzi na jana.Watu wanakufa barabarani. Hali ni mbaya sana tunaomba Serikali ikarabati barabara hii japo kwa kiwango cha changarawe, alisema Mrema.
Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya kukodi magari yanayokwenda Samunge, Saidi Kakiva alisema kutokana na barabara kuharibika nauli zimepanda kwa kiwango kikubwa.Tunaomba Serikali iwajali hawa wagonjwa. Sasa gharama ya usafiri imefikia kati ya Sh120,000 na 150,000 kwenda na kurudi wakati bei ya awali ilikuwa ni kati ya 35,000 na 80,000, alisema Kakiva.
Jijini Arusha, nyumba nyingi za kulala wageni zimejaa wateja wengi wakiwa ni wagonjwa na jamaa zao ambao wanataka kwenda huko Samunge Loliondo kwa Mchungaji Mwasapile.
Baadhi ya wagonjwa kutoka mikoa mbalimbali nchini wamelazimika kuhifadhiwa katika hospitali na vituo binafsi vya afya wakisubiri usafiri wa kwenda Samunge ambao umekuwa mgumu baada ya baadhi ya magari yaliyokuwa yakiwapeleka kusitisha huduma kutokana na ubovu wa barabara.
Tangu kuanza kutolewa kwa tiba hiyo ambayo imewavutia wananchi wengi wakiwemo viongozi waandamizi wa Serikali, wanasiasa, wananchi na watu wa mataifa mbalimbali, kumekuwa na kilio cha huduma za jamii na miundombinu vitu ambavyo vimekuwa vikikwamisha upatikanaji wa huduma hiyo.