Sijapata maelezo ya kina kwamba nini kilimsibu Dr Idris huko TANESCO? Je ni majungu au kashindwa ku deliver?
Mkuu Jibu lako hili hapa chini na kwa wengine wenye utata na mabadiliko makubwa yanayokuja ndani ya shirika:
---------------------------------
Ufisadi TANESCO wamtisha Ngeleja
Source: Tanzania Daima
WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amesema ameshtushwa na taarifa za ufisadi mwingine unaodaiwa kufanyika ndani ya Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO), na kwamba anakusudia kuunda tume kuchunguza tuhuma hizo, huku akiahidi kuchukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuhusika.
Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalumu, Waziri Ngeleja alisema taarifa za ufisadi huo amezipata kupitia vyombo vya habari na kuahidi kuzifanyia uchunguzi wa kina mara moja na baadaye kutoa matokeo kamili.
"Nilikuwa safari jimboni kwangu, ndiyo nimerudi, nitalifuatilia kwa kina na kulitolea majibu haraka, kama ni kweli wamejiingiza katika mkataba kama huo ni kosa.
"TANESCO inafanya kazi kupitia bodi na mkono wa serikali, pale ni hiyo bodi, kama kuna maamuzi yamefanyika nje ya maamuzi ya kikao halali cha bodi, tutajua," alisema Ngeleja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyoripotiwa hivi karibuni, mmoja wa wajumbe wa bodi ya TANESCO anadaiwa kuwa ni mkurugenzi katika Kampuni ya Strategies Insurance Limited and PharmaAccess International iliyopewa zabuni nono.
Taarifa hiyo ilidai kuwa kuna harufu ya ufisadi ndani ya shirika hilo wa sh bil 1.4, ambapo TANESCO imeingia mkataba wa bima ya afya wenye thamani ya sh bilioni 3.7 na kampuni hiyo kwa ajili ya wafanyakazi wake kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Taratibu zinataka kama mjumbe wa bodi ana mahusiano na shirika au taasisi inayoomba zabuni ya kutoa huduma au mali, atoe taarifa kwa maandishi ya kuelezea maslahi yake ili asihusishwe na mchakato unaohusu kampuni yake.
Mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dk. Idris Rashid na Sanjay Suchak kwa niaba ya Kampuni ya Strategies Insurance Limited na Consortium of Alexander Forbes (T) Ltd.
Baadhi ya watu walioshuhudia utiaji saini mkataba huo, ni pamoja na mwanasheria wa TANESCO, Godson Makia na Dominic Osumo, ambaye aliiwakilisha Strategies Insurance Limited and PharmaAccess International.
Hii itakuwa tume ya pili kundwa ndani ya shirika hilo baada ya ile inayoendelea kuchunguza tuhuma zilizoanikwa na Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa kuwa kuna ubadhirifu wa zaidi ya sh bilioni 1.4 ndani ya shirika hilo la umma.
Ndasa alisema shirika hilo limetumia kiasi hicho kikubwa cha pesa kwa ajili ya kukarabati nyumba 17 zilizopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, fedha ambazo kimahesabu, zinatosha kujenga nyumba kama hizo zaidi ya 20.
Alizitaja nyumba hizo zenye harufu kali ya ufisadi kuwa ni pamoja na ile iliyopo katika kiwanja namba 13, Mtaa wa Pore ambayo ilikarabatiwa kwa sh milioni 600 na imeuzwa kwa kigogo mmoja wa TANESCO kwa sh milioni 60.
Nyumba nyingine ni namba 89 iliyopo katika barabara ya Guinea, ambayo imekarabatiwa kwa sh milioni 250, nyumba namba 65 iliyopo Oysterbay iliyokarabatiwa kwa zaidi ya sh milioni 195 na nyumba namba 459 iliyopo katika Mtaa wa Mawenzi ambayo imekarabatiwa kwa zaidi ya sh milioni 130.