Maofisa hawa waliochakachua ajira za walimu wawajibishwe

Maofisa hawa waliochakachua ajira za walimu wawajibishwe

ndiyomkuusana

JF-Expert Member
Joined
Aug 2, 2012
Posts
666
Reaction score
426
Na Editor


21st February 2013





Katika toleo la jana ukurasa wa tatu wa gazeti hili, tulichapisha habari yenye kichwa cha habari `Ajira mpya za walimu zaibua mapya wizarani.'

Tulieleza kwamba ajira hizo mpya za walimu zilizotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, zimeibua kashfa mbaya katika wizara hiyo baada ya kubainika kuwa maofisa wa kitengo cha idara ya sekondari wizarani hapo wameingiza majina ya walimu waliokwisha kuajiriwa tangu mwaka jana katika orodha ya walimu walioajiriwa mwaka huu.

Aidha, hali hiyo iliwasukuma walimu 200 wa mkoa wa Dar es Salaam Ijumaa iliyopita na Jumatatu wiki hii, wengine zaidi ya 300 kutoka mikoa mbalimbali, kuandamana kwenda katika ofisi za Wizara hiyo.

Walimu hao waliamua kuandamana kutokana na kukosa ajira katika ajira mpya za walimu zilizotangazwa na wizara hiyo hivi karibuni licha ya kuwa walikuwa na sifa zinazostahili baada ya kuhitimu masomo katika vyuo mbalimbali nchini.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kuwa walimu hao wamekosa ajira mwaka huu kutokana na uzembe uliofanywa na maofisa wa kitengo cha Idara ya Elimu ya Sekondari kilichopo wizarani hapo.

Baadhi ya maofisa wa wizara hiyo waliozungumza na gazeti hili wizarani hapo, walisema maofisa wa kitengo cha Idara ya Elimu ya Sekondari, eti waliingiza majina ya walimu waliokwisha ajiriwa tangu mwaka jana.

Baadhi ya walimu hao waliongizwa katika ajira mpya imeelezwa kwamba wapo masomoni wakijiendeleza.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philipo Mulugo, alipoulizwa alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo na wizara yake imeanza kufanya uchunguzi kubaini kama wapo maofisa waliohusika na uzembe huo waweze kuchukuliwa hatua.

Hakika kitendo hiki si tu kimetushangaza bali pia kimetushtua na kutufanya tujiulize maswali mengi yasiyo na majibu.

Ni kwanini maofisa hao wa Idara ya Sekondari wawapange walimu wa zamani katika ajira mpya? Je, ni hujuma, uzembe ama makusudi kwa malengo wanayoyafahamu wao?

Hatupati jibu sahihi kwa maswali hayo lakini kwa ujumla kitendo hiki kinapaswa kilaaniwe na kila Mtanzania anayelitakia Taifa hili mema.

Walimu hao wapya, wamevuta subira kwa kipindi kirefu kusubiri serikali iwapangie vituo vyao vya kazi, lakini katika hali ya kushangaza, wanajikuta wameachwa na kupangwa wengine ambao tayari wana ajira zao.

Sisi tunashauri kwamba maofisa waliofanya kitendo hiki ama kwa uzembe ama kwa makusudi, hakika wawajibishwe maana wanataka kuleta usumbufu kwa walimu wapya na matokeo yake waitupie lawama serikali.

Tuna uhakika kwamba maofisa walihusika katika kashfa hii si kwamba walikuwa ndiyo wanaanza kazi, tuna imani kuwa ni wazoefu na wanaojua wajibu wao.

Kwa msingi huo, kufanya uzembe ama kama tulivyosema makusudi, ni hakuwezi kuvumiliwa kwa namna yoyote ile.

Mbali ya kuleta usumbufu kwa walimu hao wapya, pia ni kuchezea kodi za Watanzania kwa kuwa zoezi hilo lazima lifanyiwe masahihisho kwa kuhakikisha kwamba walimu wapya wanapata haki yao ya ajira.

Kufanya hivyo hapana shaka kutahijika rasilimali watu, fedha na vifaa ambavyo vyote hivyo, ni jasho la mlipa kodi Mtanzania!

Kwa hakika tunashauri mamlaka husika iwachambue kwa makini maofisa waliofanya madudu hayo na hatimaye wapewe `kile wanachostahili.

Aidha, tunamuunga mkono Naibu Waziri Mulugo aliyelihakikishia Taifa hili kuwa wanafanya uchunguzi wa suala hilo na wakibaini wapo maofisa waliohusika na uzembe huo wa kuingiza majina ya walimu wenye ajira atamshauri waziri wake wawawajibishe.

Mulugo alisema inashangaza kujitokeza kwa tatizo hilo ambalo ni la kizembe kwasababu maofisa wa wizarani kama walikuwa hawana takwimu za walimu walioajiriwa mwaka jana ambao wamekwenda kusoma wangepata takwimu hizo kutoka kwa maofisa elimu wa mikoa.




CHANZO: NIPASHE
 
Sasa kuna haja gani kupoteza muda wa kuunda tume ya kuwachunguza hao maafisa wasio waadilifu wakati walimu wasiopata ajira wapo na wanajilikana, kwahiyo mi naona ni bora walimu wasiopata ajira waajiriwe kwanza na ndipo hatua zingine za kuwawajisha hao maafisa ianze mara moja
 
Back
Top Bottom