Maoni ya mabaraza ya katiba kuhusu rasimu ya Katiba Mpya

Maoni ya mabaraza ya katiba kuhusu rasimu ya Katiba Mpya

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Heshima kwenu wakuu,
maoni1.PNG

Baada ya kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Awali ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilichapisha na kusambaza Rasimu ya Katiba katika maeneo yote nchini na katika tovuti na mitandao mbalimbali ya intaneti. Madhumuni ya hatua hiyo ilikuwa ni kuwawezesha wananchi kupitia mikutano ya mabaraza ya katiba kuichambua na kuitolea maoni Rasimu ya Katiba kwa lengo la kuiboresha. Tume iliwajibika kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 18 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, kuunda mabaraza ya katiba katika kila wilaya, ngazi ya mamlaka za serikali za mitaa. Hata hivyo, kwa kuzingatia changamoto za kijiografia za mkoa wa Dar es Salaam na idadi kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam, Tume iliona umuhimu wa kuongeza idadi ya Mabaraza ya Katiba na kuamua kuwa na mabaraza mawili kwa kila halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam. Hali hiyo ilifanya jumla ya mabaraza ya wilaya, ngazi ya mamlaka ya serikali za mitaa kuwa 177 ikiwa ni mabaraza 164 kwa Tanzania Bara na mabaraza 13 kwa upande wa Zanzibar.

Mabaraza ya Wilaya yaliwakutanisha wawakilishi wa wananchi katika makundi yao mbalimbali. Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya walijumuisha wawakilishi wa wananchi waliochaguliwa kupitia kata zao kwa Tanzania Bara na shehia kwa upande wa Zanzibar. Uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ulifanywa na wananchi wenyewe kwa kuzingatia uwakilishi wa watu wazima, wanawake, vijana na jiografia ya kata au shehia husika. Wajumbe wengine wa mabaraza walikuwa ni madiwani wote waliopo katika wilaya husika. Mabaraza haya yaliwawezesha wawakilishi wa wananchi kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba mpya katika mikutano iliyokuwa imeitishwa na Tume.

Tume pia ilipokea maoni juu ya Rasimu kutoka kwa mabaraza ya Katiba ya asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana. Mabaraza hayo yaliundwa kwa mujibu wa kifungu cha 18 (6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kinachoiwezesha Tume kuruhusu asasi, taasisi au makundi ya watu yenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume. Mabaraza hayo yalijiendesha yenyewe kwa kuzingatia mwongozo uliokuwa umetolewa na Tume. Hata hivyo, Tume iligharamia uendeshaji wa mabaraza mawili ya watu wenye ulemavu. Baraza la kwanza liliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania Bara (SHIVYAWATA) na baraza la pili liliandaliwa na Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA). Mabaraza hayo yaliwashirikisha watu wenye ulemavu wa aina zote.



Miongoni mwa asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana yaliyounda mabaraza ya Katiba ni pamoja na:

(1) Jumuiya za Kidini.

(2) Vyama vya Siasa.

(3) Asasi za Kiraia.

(4) Jumuiya za Wakulima.

(5) Jumuiya za Wafugaji.

(6) Taasisi za Elimu ya Juu.

(7) Jumuiya za Wanahabari.

(8) Taasisi za Wafanyabiashara.

(9) Jumuiya za Wanawake.

(10) Jumuiya za Vijana.

(11) Jumuiya za Kitaaluma.

(12) Jumuiya za Wafanyakazi..

(13) Wizara, Idara na Taaasisi za Serikali

(14) Jumuiya za Waajiri.

(15) Jumuiya za Wanasheria

(16) Jumuiya za Watanzania waishio nje ya Nchi (Diaspora).

(17) Jumuiya za Watu wenye Ulemavu.

Mabaraza hayo yaliwawezesha wananchi kupitia asasi, taasisi au makundi yao mbalimbali kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba. Kwa ujumla, kulikuwa na mabaraza 614 yaliyoundwa na asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana.

Baada ya kupokea maoni na mapendekezo kuhusu Rasimu ya Katiba mpya, Tume ilipitia na kuchambua maoni ya wananchi na kuyaweka katika maeneo mbalimbali sambamba na ibara husika za Rasimu ya Katiba. Tume ilifanya tathmini ya maoni na mapendekezo ya Mabaraza ya Katiba kwa namna ambayo yanakubaliana na au kutokubaliana na masharti ya Ibara za Rasimu ya Katiba. Katika uchambuzi huo wa maoni ya Mabaraza, Tume ilizingatia uzito wa hoja zilizotolewa na hadidu za rejea zilizowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika kuamua kubadilisha ama kubakiza vifungu vya ibara husika za Rasimu ya Katiba. Pia, Tume iliyapa hadhi sawa maoni na mapendekezo kutoka kwenye mabaraza ya aina zote mbili, kwa kuwa yote ni maoni ya wananchi.



Taarifa hii inaonyesha muhtasari wa maoni ya wananchi, kupitia mabaraza ya katiba juu ya Rasimu ya Katiba kuanzia na Utangulizi na Ibara zote 240. Taarifa inakusanya mawazo yote kwa muhtasari baada ya kuangalia kiini cha ujumbe uliokusudiwa katika maoni yaliyotolewa. Pia, taarifa hii inajumuisha sababu zilizotolewa na wananchi walipotoa maoni yao katika sehemu na Ibara husika. Hata hivyo, kuna baadhi ya vifungu ambavyo wananchi walitoa maoni bila kuainisha sababu. Ieleweke kwamba, wananchi katika mabaraza mengi ya katiba walitoa maoni katika maeneo ambayo waliona yanahitaji maboresho na hawakutoa maoni kwa maeneo walioyoona kuwa hayahitaji mabadiliko. Aidha, ingawa maoni ya wananchi yaligusa kila sehemu ya Rasimu, maoni mengi yalikuwa juu ya vifungu vinavyohusiana na mamlaka ya serikali ya muungano, mamlaka ya serikali za nchi washirika, uraia na uhamiaji, muundo wa muungano na mambo ya muungano. Maeneo mengine yaliyotolewa maoni kwa wingi na wananchi ni pamoja na maadili ya viongozi na miiko ya viongozi, haki za binadamu, masuala ya fedha, mikopo na madeni. Taarifa hii inaonyesha pia vifungu vilivyofanyiwa marekebisho kutokana na maoni ya mabaraza ya katiba. Marekebisho hayo ni pamoja na kubadili baadhi ya masharti ya ibara za Rasimu ya Katiba kwa kuondoa baadhi ya maneno, kuongeza maneno au kuandika upya vifungu vya ibara husika katika Rasimu kama inavyojionyesha katika taarifa hii. Baadhi ya vifungu vilivyorekebishwa viko kwenye ibara zinazohusu mamlaka ya wananchi, utii na hifadhi ya katiba. pamoja na utambulisho wa Jamhuri ya Muungano, ukuu wa katiba, maadili ya viongozi wa umma na miiko ya viongozi, utumishi katika Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, baada ya kutathmini maoni ya wananchi yaliyounga mkono ibara zibaki kama zilivyo na yale yaliyokuwa tofauti na baadhi ya vifungu vya Rasimu ya Katiba, Tume iliona ni vyema vifungu hivyo vibaki kama vilivyo.

Habari zaidi, fungua kiambatanisho
 

Attachments

Back
Top Bottom