Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, masjala ndogo ya Dar es Salaam, ambao ni Jaji Dunstan Nduguru, Jaji James Karayemana na Jaji Ferdinand, wametupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na Tundu Lissu kwenye kesi ya uhaini na kusema kuwa hayawezi kuifanya mahakama hiyo kukosa mamlaka, leo Septemba 14, 2025.
Mahakama imesema kwamba Mahakama ya Kisutu ilikuwa na mamlaka ya kutumika kama Mahakama ya Ukabidhi (Committal Court), hivyo hoja ya Lissu kuwa haikuwa na mamlaka haina uhalali wa kisheria kwa kuzingatia vifungu vya 186, 187 na 261 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Kuhusu hoja nyingine kwamba mwenendo ulikuwa na dosari kwa Mahakama ya Ukabidhi kushindwa mara kadhaa kutoa sababu za kuahirisha shauri hilo, Mahakama imeeleza kuwa mahakama hiyo ilikuwa kwa ajili ya proceedings, hivyo kulikuwa na baadhi ya mambo ya kisheria ambayo yalikuwa yamefungwa mikono. Mahakama imetupilia mbali hoja hiyo na kueleza kuwa jambo hilo halikuathiri haki za mshtakiwa.
Pia, kuhusu hoja ya kuwaficha mashahidi, ambapo upande wa Jamhuri ulidaiwa kushindwa kuzingatia maelekezo ya Mahakama Kuu, jopo hilo limesema kuwa suala hilo halikuathiri haki za mshtakiwa, hivyo nalo limetupiliwa mbali.
Kuhusu hoja ya kutopewa nyaraka kwa ukamilifu za kutoka kwenye Mahakama ya Ukabidhi, Mahakama imesema Lissu ana haki ya kupewa nyaraka hizo kama alivyodai. Hata hivyo, imeeleza kuwa kwa kuwa bado suala hilo lipo ndani ya muda, basi bado kuna nafasi ya kupewa nyaraka hizo.
Hoja ya Lissu kwamba hakupewa nafasi ya kutoa maelezo mbele ya Mahakama ya Ukabidhi, Mahakama imesema kwamba kumbukumbu zinaonesha kuwa alipewa nafasi ya kusema, lakini baadhi ya mambo hayaonekani kama aliweza kujieleza. Hata hivyo, Mahakama imesema kuwa suala la kupewa nafasi ya kueleza ni ''option", hivyo mshtakiwa hajanyimwa haki ya msingi inavyoweza kubadili uhalali wa proceeding.
Kuhusu madai kwamba mashahidi wake hawakuwekwa kwenye committal proceedings, Mahakama imesema kuwa kumbukumbu zinaonesha nafasi ya kutaja mashahidi wake ilitolewa ingawa mashahidi hawakuorodheshwa, Mahakama imesema kuwa kwa kuwa mshtakiwa alionesha nia, bado kuna nafasi ya kuleta mashahidi wake. Hivyo hoja hiyo haiwezi kubadili uhalali wa mwenendo wa committal proceedings.