Tatizo letu inaonekana tunaangalia sana muonekano wa nje zaidi ya undani wa mtu.
Ndiyo maana inakuwa rahisi sana kuibiwa na majambazi waheshimiwa wanaovaa suti, halafu kuna watu wana roho safi sana wasuka nywele na wenye tattoo tunawaogopa sana.
Habari hii inanikumbusha mzee mmoja, msomi wa zamani, mtu wa principles zake.
Yule mzee pale jirani na kwake kulikuwa kuna kijiwe wanakaa vijana, kwa mtazamo wake yule mzee, aliwaona wale vijana ni wahuni, wavuta bangi tu, si watu wazuri. Watu wanaokaa kijiweni watakuwaje wazuri? Ni wavivu wasio na kazi tu hawa, alijifikiria.
Siku moja, mzee alikuwa anatoka na gari yake, anawahi mikutano muhimu, gari ikamuharibikia getini kwake.
Sasa, pale getini kwake , upande wa pili wa mtaa ndiyo kuna kijiwe cha wale vijana. Vijana hawakujua kama mzee kiundani anawaona wahuni, wao walimuona huyu mzee wetu wa mtaani tu.
Mzee alikuwa ni wale wazee fulani hawalijui gari zaidi ya kujua kuendesha tu. Kumbe katika wale vijana kuna mpaka mafundi wa magari, wakamsaidia kutengeneza gari chapchap, wakamsukuma, gari likawaka, akawashukuru sana. Akataka kuwapa fedha kidogo, wale vijana wakamkatalia, wakisema kwamba angekuwa mtu mwingine wangechukua, lakini yeye mzee wao wa mtaani wamemfanyia hisani za ujirani tu.
Kuanzia siku hiyo, mzee akawa anasema ameacha kuwadharau watu kwa muonekano wa nje, kwa sababu ameona muonekano mwingine unaficha mambo mengi ya ndani ya mtu.