Hivi karibuni, Marekani, Uingereza na Australia, chini ya uongozi wa Marekani, zilitangaza kuanzisha ushirikiano mpya wa usalama wa pande tatu, huku lengo kuu likiwa ni kuisaidia Australia kuanzisha vikosi vya nyambizi za kinyuklia. Australia ikavunja makubaliano yake na Ufaransa kuhusu kununua nyambizi za Ufaransa zenye thamani ya dola bilioni 60 za Kimarekani, na wakati huohuo, Ufaransa ni nchi na mwenzi wa kirafiki wa Marekani. Kitendo hiki kimethibitisha tena kuwa, urafiki hauna maana yoyote kwa Marekani mbele ya masilahi yake.
Baada ya tukio hilo, serikali ya Ufaransa ilitangaza mara moja kuwarudisha mabalozi wake wa nchini Marekani na Australia, huku Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian akiilaani Marekani kwa kufanya kitendo cha “kimwamba cha upande mmoja”. Amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Ufaransa kumrudisha nyumbani balozi wake wa nchini Marekani katika historia ya uhusiano wa nchi hizo mbili, hali ambayo imeonesha uzito wa mvutano huo. Le Drian amesema, awali, Marekani iliondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan bila ya kujadiliana na washirika wake ambao pia walipeleka wanajeshi nchini humo.
Ili kufufua uhusiano kati ya Marekani na nchi za Ulaya ulioharibiwa na sera ya “Marekani Kwanza” wakati wa utawala wa Donald Trump, Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden alipoingia madarakani mapema mwaka huu, alitangaza kwa sauti kubwa, “Marekani imerudi, wacha tutazame mbele pamoja”. Lakini mara hii kunyakua oda kubwa mno ya Ufaransa ya mradi wa nyambizi ni pigo lingine kwa uhusiano kati ya pande hizo mbili.
Ili kupata maslahi zaidi, kwa muda mrefu uliopita Marekani imekuwa ikipigania faida na washirika wake wa Ulaya kwa njia zote. Kulingana na wataalam wa silaha wa Ufaransa, mara kwa mara Ufaransa inalazimika kuacha mauzo yake ya silaha kutokana na shinikizo la Marekani. Ripoti iliyotolewa na vyombo vya habari vya Denmark pia inaonesha kuwa, ili kuzisaidia kampuni za Marekani kushinda zabuni ya ndege za kijeshi katika soko la kimataifa, Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (CIA) lilizindua shughuli za ujasusi dhidi ya serikali ya Denmark na kampuni husika. Mbali na mauzo ya silaha, Marekani pia inawatendea vibaya washirika wake wa Ulaya katika nyanja za uchumi na biashara. Ili kuisaidia Kampuni ya General Electric ya Marekani kununua Kampuni ya Alstom ya Ufaransa, serikali ya Marekani iliweka mitego na kumkamata mkurugenzi wa Alstom. Zaidi ya hayo, ili kuongeza mauzo ya gesi yake kwenye soko la Ulaya, Marekani iliikataza Ujerumani kushiriki kwenye mradi wa bomba la gesi ya Russia “Nordstream 2”, na hata kuweka vikwazo dhidi ya kampuni zilizoshiriki kwenye mradi huo.
Marekani si kama tu inawatendea vibaya washirika wake wa Ulaya, bali pia inapuuza maslahi ya wenzi wake wengine. Kwa miaka 20, Marekani ilifanya vita nchini Afghanistan, mwishowe iligundua kuwa haiwezi kupata faida tena kutoka kwenye nchi hiyo, ikaamuru kuondoa vikosi vyake vyote nchini Afghanistan, bila kujali serikali ya nchi hiyo iliyoanzishwa chini ya msaada wa Marekani, na washirika wake waliotuma wanajeshi pia nchini Afghanistan. Kitendo hicho kilisababisha kuanguka kwa serikali ya Afghanistan mara moja, na usumbufu kwa wanajeshi wa nchi nyingine nchini humo.
Marekani imezoea “kuchoma kisu” washirika wake ghafla. Kama tabia nyingine nyingi za kushangaza za nchi hiyo, kitendo kama hiki pia kinatokana na ubinafsi na umwamba wake. Kama ncha pekee duniani, Marekani hufanya mambo yake bila kujali maslahi ya nchi nyingine, hata washirika wake. Hivyo nchi zinazoisaidia Marekani kupinga China, zikiwemo Lithuania, Uingereza na Australia, lazima zitafakari ikiwa Marekani itazichoma kisu ghalfa, kwani kutokana na maslahi, hakuna nchi ambayo Marekani haiwezi kuiacha.