Maridhiano ya muswada katiba mpya yadumishwe

Maridhiano ya muswada katiba mpya yadumishwe

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Jumanne ijayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete atakutana na viongozi wa vyama vikuu vya upinzani nchini kujadili kuhusiana na muswada wa katiba mpya.

Viongozi hao wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR Mageuzi wamekuwa wakiupinga muswada huo uliopitishwa na wabunge wengi wa chama tawala (CCM) kwa kudai kuwa una kasoro nyingi na hivyo kumtaka Rais Kikwete asiusaini.

Katika kuupinga muswada huo, viongozi hao wa upinzani walitangaza kuitisha maandamano makubwa ya nchi nzima. Walitangaza pia kufanya mikutano ya pamoja ya hadhara, nia ikiwa ni kumtaka Rais Kikwete asisaini muswada huo.

Hata hivyo, wakati akizungumza na taifa wiki iliyopita kupitia hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema kuwa hakuna haja kwa wapinzani kuandamana kwani madai yao yanazungumzika. Siku chache baadaye, ikulu ikatoa taarifa ya kuwaalika viongozi hao wa CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi. Taarifa hiyo iliwataka waende wakakutane na Rais Kikwete ili kuzungumzia jambo hilo.

Juzi, viongozi hao wa upinzani wakatangaza kusitisha maandamano na mikutano yao na kueleza kuwa wako tayari kukutana na rais. Na jana, ndipo ikatangazwa rasmi kuwa kikao hicho baina ya rais na viongozi wa upinzani kitafanyika ikulu Jumanne, kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Sisi tunapongeza pande zote kuhusiana na uamuzi wao huu wa kukutana. Tunaamini kuwa hatua hii ni mwendelezo wa dhamira safi ya kutaka kuhakikisha kuwa mwisho wa siku, tunapata katiba nzuri itakayozingatia maoni ya Watanzania walio wengi.

Si kusudio letu kujadili ubora wa muswada huo ambao Rais Kikwete amepelekewa baada ya wabunge wengi wa CCM kuupitisha huku wapinzani wakiupinga na kutoka nje ya Bunge. Na wala siyo lengo letu pia kuchambua kasoro zinazolalamikiwa. Bali, tunapongeza hatua hii ya kutoa nafasi ya mazungumzo, tukiamini kuwa tofauti zilizojitokeza zitafanyiwa kazi na hivyo kutoa fursa kwa mchakato huo wa kuwa na katiba mpya kuendelea pasi na vikwazo.

NIPASHE tunaamini kuwa siku zote, njia bora ya kumaliza tofauti za kimtazamo miongoni mwa vyama vya siasa na hata makundi mengine ya kijamii ni kuketi pamoja na kujadiliana juu ya namna ya kufikia muafaka kwa manufaa ya taifa.

Tunatambua kuwa maandamano ni njia mojawapo halali ya kidemokrasia katika kufikisha ujumbe. Lakini tunadhani kwamba njia hiyo inapaswa kuwa ya mwisho baada ya taratibu nyingine zote kushindikana.

Hekima, busara na uvumilivu vinapaswa kuwekwa mbele katika kushughulikia masuala nyeti kama haya ya kuandikwa kwa katiba mpya. Kamwe kutunishiana misuli hakuwezi kutuletea matunda mema.

Sisi tunaamini kuwa serikali, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, CCM na vyama vingine vyote vya siasa havina nia mbaya. Bali, vyote vinataka kuona kuwa Tanzania yetu inaendelea kujivunia hali ya amani na utulivu.

Na kwamba, mwisho wa mijadala yote inayoendelea kuhusiana na katiba mpya ni kuona kuwa kwa pamoja, Watanzania wanasimama imara katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa lao.

Tunaamini vilevile kuwa serikali (rais) na viongozi hawa wa vyama vya upinzani ni kama wajenzi. Wote wangali msituni wakitafuta fito kwa ajili ya kukamilisha nyumba ambayo mwisho wa siku, wote watanufaika nayo.

Bila shaka, serikali inalijua jambo hili. Viongozi wa vyama hivi vya upinzani wanaujua ukweli huu. Kwamba wote wanajenga nyumba moja.

Ni kwa kuzingatia msingi huo, ndipo NIPASHE tunapoona kuwa hakuna sababu ya kugombana baina yao. Hakuna sababu ya kutunishiana misuli. Na wala hakuna sababu hata moja ya kutokubali kukutana ili kujadili kasoro zinazolalamikiwa.

Tunatambua vilevile kuwa kama angetaka, Rais Kikwete asingetoa nafasi ya kukutana na wapinzani. Angesaini muswada huo na kuwaacha wapinzani wakilalamika.

Na wapinzani pia, kama wasingetanguliza maslahi ya taifa, ni wazi kwamba wangekuwa wepesi wa kubuni sababu ya kutoridhia rai ya kutakiwa waende kukutana na rais. Badala yake, wangeng'ang'ania kuandamana, kuitisha mikutano na kutoa kauli kalikali ambazo pengine zingetia doa mchakato wa kuandaa katiba mpya.

Hata hivyo, Rais Kikwete ameendeleza uungwana wake, viongozi wa Chadema, CUF na NCCR pia wamekuwa waungwana. Ndiyo maana wote wamekubaliana kukutana Jumanne.

Sisi tunawapongeza na kuwakumbusha kuwa maridhiano ya namna hii ndiyo tunayoyataka. Ni kwa sababu yanatoa ishara njema kwa mchakato unaoendelea wa kuandika katiba mpya. Yadumishwe.




CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom