Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
MASACHE KASAKA: TUNATAKA TUONE MPANGO WA MAENDELEO YA TAIFA UNABORESHA MAISHA YA WATANZANIA
"Mipango ya Serikali imekuwa ikipangwa kila mwaka, kuna ya miaka 25 na kuna ya miaka 5. Ni Mipango mizuri na utekelezaji wake tumeuona, Watanzania wote ni mashuhuda namna ambavyo miradi mingi ya kimkakati imefanyika nchini kote. Tunaipongeza Serikali, Tunampongeza Rais Samia kwa kuhakikisha hakuna kilichosimama" - Mhe. Masache Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa
"Ili Mipango ya Serikali iweze kutekelezwa vizuri, Tume ya Mipango na Wizara ya Mipango huwa zinapanga vizuri lakini tunashuka chini bado kuna changamoto ya Taasisi kuweza kusomana. Mahali penye miradi ya TARURA utakuta kuna miradi mingine ya REA, Kilimo, RUWASA"
"Watu wa TARURA wanapotengeneza miradi hawahusishi watu wa Maji na matokeo yake wanaharibu miundombinu ya Maji pamoja na miundombinu mingine. Hii hupelekea kuleta changamoto ya miundombinu mingine inayoharibiwa wakati wa ujenzi wa barabara"
"Mpango wa Serikali wameeleza namna ambavyo Serikali imepanga kutumia Shilingi Trilioni 16 katika Miradi ya Maendeleo. Lakini bado fedha hii ni kidogo. Tunategemea kodi kupata hizi fedha, misaada na mikopo mbalimbali, naomba tuone namna ya kuongeza walipa kodi wengine ili fedha ziweze kupatikana"
"Leo hii TRA pamoja na Serikali bado inazidi kuwakamua walipa kodi walewale Watanzania, tunazibadilisha kodi kwa majina tofauti. Naomba Serikali itengeneze mazingira ili kutengeneza wafanyabiashara wapya walipe kodi mpya ili tuongeze mapato nchini"
"Tuna wafanyabiashara ambao mitaji yao ni kidogo sana, Serikali ione namna ya kuwasaidia kuwainua ili tuwatengeneze wafanyabiashara wakubwa pamoja na Mabilionea wapya katika nchi yatm Tanzania, hii itasaidia Kuboresha mazingira ya wafanyabiashara"
"Pamoja kwamba sasa tuna umeme wa kutosha ni wakati muafaka Serikali iwekeze nguvu kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa Umeme maana kuna maeneo bado umeme unakatikakatika na changamoto kubwa ni miundombinu ya Umeme ambayo imeshachoka"
"Baadhi ya maeneo ya Lupa, Chunya, Makongorosi umeme umefika lakini umeme ni mdogo wananchi wanashindwa kunufaika na umeme. Naomba Serikali ijenge Vituo (Substations) ili tuweze kupata umeme wenye nguvu ili wananchi waweze kunufaika na umeme wao"
"Umeme ni biashara, tutumie nafasi hii kupeleka umeme kwenye uhitaji mkubwa. Chunya kuna wachimbaji wengi wadogo wadogo wanauhitaji mkubwa sana wa umeme. Serikali iwekeze nguvu za kutosha kuhakikisha umeme unawafikia wachimbaji wengi kwenye maeneo yao ili waweze kuununua na kuutumia kuzalisha"
"Sekta ya Madini Serikali imeboresha ambapo imefikia zaidi ya asilimia 9 kwenye mchango wa Pato la Taifa. Asilimia 40 ya Pato hilo imetoka kwa wachimbaji wadogo. Tuwawekee wachimbaji wadogo mazingira mazuri ili waendelee kuzalisha vizuri zaidi na tuendelee kuwekeza kwenye Utafiti" - Mhe. Masache Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa
Kauli Mbiu: Mpango wa Maendeleo Unalenga Kuboresha Hali ya Maisha ya Watanzania na Kujenga Uchumi Imara na Shindani.