Mimi binafsi nashangazwa sana na mchakato mzima wa vitambulisho vya raia wa Tanzania na umuhimu wake, hasa kwa kuwa ni wiki chache tu kabla ya sensa. Ninasikia harufu ya ulaji mkubwa sana ambao unafichwa kupitia zoezi hili.
Sioni kwa nini watu wapange foleni kutwa nzima ili kujaza fomu ambazo baadaye watapatiwa vitambulisho, na huku mwezi huu huu wa nane kutakuwa na zoezi la kuwahesabu watu. Kwa nini kama suala la vitambulisho vya raia wa Tanzania lilikuwa/au ni muhimu, wahusika wa kuandikisha watu wasiwe walewale watakaopita kila nyumba kuhesabu watu? Hapo serikali itakuwa imeua ndege wawili kwa jiwe moja, na kero ya kupanga foleni na hatimaye kuambiwa rudi kalete barua ya mjumbe n.k vitaondoka.
Pili, kwa mtazamo wangu ni rahisi zaidi kujua nani ni raia na nani si raia kwenye kaya zetu. Ninaamini bado wajumbe wa nyumba kumi wapo, hata kama wanaitwa kwa jina lingine, sijui ndiyo wenyeviti wa serikali za mitaa. Hawa watu tunao mitaani mwetu, na ninavyoelewa wao wanawafahamu (au wanatakiwa kuwafahamu) vizuri watu wao. Wangewezeshwa wao kuwa na madaftari ya orodha ya kila mtu anayeishi kwenye mitaa yao.
Kila mtu aende kujiandikisha kwa mjumbe wake, akiwa na taarifa zake kamili. Mjumbe atafahamu mtu huyo anafanya kazi gani (ya kuajiriwa ama ya kujiajiri, ama mkulima n.k.), amezaliwa wapi, kama si mwenyeji wa eneo hilo basi anatokea wapi (mkoa gani au kijiji gani), umri wake, jinsia, ameoa/ameolewa, ana watoto wangapi, elimu yake, na ikibidi hata suala la imani (dini) ambalo limeleta kizungumkuti sana kwenye sensa litapatiwa ufumbuzi. Mwenyekiti wa serikali ya mtaa anawajua watu wake, hata kama kuna mkimbizi kajichimbia katikati ya watu wa eneo lake atajulikana. Na kama kuna mhamiaji halali au asiye halali atajulikana.
Miaka ya mwanzoni mwa 80 kulikuwa na uhaba wa bidhaa mbalimbali nchini, tukawa na orodha za kaya ili kudhibiti upatikanaji wa bidhaa adimu kama sukari, unga, mchele n.k. Nakumbuka kabisa wenyeviti wa serikali za mitaa enzi hizo tukiwaita wajumbe wa nyumba kumi ndiyo waliopewa jukumu la kuandikisha watu. Zoezi lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa mjumbe alikuwa na orodha ya kila mkazi wa nyumba zilizo chini ya eneo lake. Tuliandikisha mpaka wafanyakazi wa majumbani. Nia ilikuwa mtu yeyote asife njaa, na chakula kipatikane kutosheleza idadi ya watu. Ilikuwa ukienda dukani kununua bidhaa unaenda na kitabu chako kinachoonyesha ukubwa wa kaya yako. Na ukipata mgeni ilikuwa lazima utoe taarifa kwa mjumbe ili ijulikane ya kuwa kaya imeongezeka ukubwa na idadi ya mahitaji yako pia imeongezeka. Nakumbuka kuna kaya kubwa zilikuwa zinaweza kupata kilo 3-4 za sukari kwa wiki, lakini kama kaya yako ni ndogo unapewa kilo mbili kwa wiki. Na orodha yote alikuwa nayo mjumbe wa nyumba kumi (mwenyekiti wa serikali ya mtaa)
Nimeurudia mfano huu kuonyesha ya kuwa 'system' ilikuwepo na bado ipo. Kama kweli nia ni kupata vitambulisho vya uraia ingeweza kufanyiwa kazi ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha na kuondoa mianya inayoweza kutumiwa na wajanja kupata vitambulisho ambavyo hawastahili. Vilevile hii ingepunguza kero na usumbufu uliojitokeza wa watu kupanga foleni kutwa nzima, kwa kuwa mjumbe angeweza kwenda majumbani mwa watu wake kwa nafasi zao na kupata taarifa zote.
Kwa huu utaratibu unaotumika sasa hivi zoezi zima ni mchezo wa kitoto.